Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

Madaktari kufutiwa leseni mjadala kila kona(Mwananchi)

Waandishi Wetu
UAMUZI wa Baraza la Madaktari Tanganyika kuwafutia leseni madaktari 319, umepokewa kwa hisia tofauti miongoni mwa wadau ambao baadhi wamepinga hatua hiyo na wengine wakipongeza.
Juzi, Baraza hilo lilichukua uamuzi huo kutokana na mgomo wa madaktari nchini licha ya amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, kuwataka warejee kazini.

Wakati baadhi ya wadau wakisema haukuwa uamuzi sahihi kwa kuwa nchi inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wanataaluma hao wa afya, wengine wamesema ni sahihi kwani walikataa suluhu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdallah Katunzi alisema kufutiwa leseni kwa madaktari si njia sahihi ya kutatua tatizo na badala yake Serikali itakuwa inaongeza tatizo.

“Hii inachangia upungufu wa madaktari ukizingatia kuwa kabla ya kufutiwa leseni bado kuna tatizo la madaktari wa kutosha hapa nchini, sasa Serikali kwa kufanya hivyo itakuwa inaongeza adha ya matibabu kwa wagonjwa,” alisema Katunzi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu (DUCE), Profesa Simon Mbilinyi alisema kitendo cha kuwafutia madaktari leseni ni hatari kwa jamii na kuongeza kwamba idadi ya madaktari waliofutiwa leseni ni kubwa ikizingatiwa kuwa bado nchi haina madaktari wa kutosha.

Profesa Mbilinyi alisema ni vyema Serikali na madaktari wakarejea katika meza ya mazungumzo ili kuafikiana kuliko kuchukua uamuzi ambao utaiathiri jamii.

Maoni ya wabunge
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema kitendo cha kufukuzwa kwa madaktari 319 wa waliokuwa katika mafunzo ya vitendo nchini ni mpango wa Serikali kuwatisha akidai kuwa madaktari hao walikuwa na nia njema ya kudai maslahi yao.

“Sijafurahishwa kabisa na kitendo hicho. Hiyo ni ngao inayotumiwa na Serikali katika kushusha nguvu za wananchi wanapodai haki zao. Kwa nini imewafukuza wakati inajua kabisa walikuwa wana madai ya msingi?”

Mbunge wa Kikwajuni (CCM), Yusuf Masauni pia alisema hajafurahishwa na hatua hiyo ya madaktari hao kunyang’anywa leseni akisema imeharibu mustakabali wao kitaaluma na pia hatua hiyo imepunguza idadi ya watumishi katika kada hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rita Kabati alisema suala la mgomo wa madaktari ni la kisiasa zaidi: “Mimi mwenyewe mgomo wa madaktari umenigusa mno kwa sababu ndugu yangu alifariki katika kipindi ambacho wao walikuwa wanagoma. Ieleweke kuwa mgomo wao unapoteza roho za watu ambazo haziwezi kurudishwa tena.”

Mbunge wa Ole (CUF) Rajabu Mbaruku, alisema adhabu waliyopewa madaktari hao ni matokeo ya utawala bora na wa sheria... “Kwa hali ya kiubinadamu, adhabu hiyo ni nzito lakini kama wamekiuka taratibu hawana budi kuadhibiwa na wawajibike kwa uvunjaji wa kanuni.”
Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema Serikali haipaswi kutumia nguvu na jazba kuwaondoa madaktari ambao imewasomesha kwa fedha nyingi zinazotokana na kodi za wananchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Patric Boisafi alisema uamuzi wa Serikali ni fundisho kwa madaktari kwani wanalipiwa masomo yao na Serikali lakini pindi wanapomaliza hawataki kuisikiliza.
Wanaharakati

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Sikika, Irenei Kiria amekosoa uamuzi huo akidai kuwa ni udhaifu wa Serikali katika kushughulikia migogoro nchini.

“Serikali inaendelea kuonyesha kuwa haina uwezo wa kutatua migogoro iliyopo nchini na badala yake, inatumia vitisho. Jamii haiwezi kuendeshwa kwa namna hiyo,” alisema Kiria na kuongeza:

“Tanzania ina upungufu wa madaktari takriban asilimia 90 na daktari mmoja wa Kitanzania anahudumia wagonjwa 30,000 badala ya 10,000 kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).”

Mwanasheria Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema bado anafuatilia suala hilo na yupo kwenye hatua za kupitia vifungu vya sheria ili kujiridhisha kama hatua hiyo iko sawa kisheria na imefuata taratibu zote.

Mkazi wa Moshi, Spora Swai alisema uamuzi huo siyo sahihi hususan katika kipindi hiki ambacho nchi ina tatizo la wataalamu hao wa afya na kuishauri Serikali kutumia busara kumaliza tatizo hilo badala ya kukimbilia mahakamani na kuwafutia leseni madaktari hao.

“Hawa walikuwa wanalalamikia mazingira bora ya kazi kuwe na vitendea kazi, dawa na mambo mengine badala ya Serikali kulifanyia kazi jambo hilo, wao wanakimbilia mahakamani na kuwafutia usajili hao wengine hapa hawajengi, bali wanaendelea kuwakatisha tamaa,” alisema.

Mkazi mwingine, Ernest Matiku alisema: “Ukiangalia hili suala kwa umakini utagundua kuwa limekaa kisiasa zaidi, kwa kuwa huwezi kuwafutia madaktari wote hao leseni wakati nchi yetu haina madaktari wa kutosha. Kufanya hivyo si kuwakomoa wao pekee, bali na jamii inayowategemea.”
Kwa upande wake, Aloyce Minja aliipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua na kueleza kuwa ni funzo kwa wote wanaofanya migomo isiyokua na tija na yenye athari kwa jamii.

Huko Iringa, mkazi wa mji huo, Daud Butinini alisema kabla ya kuwafutia leseni madaktari hao, Serikali ilipaswa kupata kibali kutoka kwa wananchi kwa kuwa ndiyo waliowaajiri kwa kuwalipia karo walipokuwa vyuoni huku mkazi mwingine, Christopher Msigwa akisema Serikali lazima ikae na kutafakari suala la migomo ya watumishi inayoendelea nchini badala ya kuwatishia.

Mkazi wa Mjini Mwanza, Daud John alisema ingawa tayari madaktari hao wamefutiwa usajili wa muda, Serikali inapaswa kuangalia umuhimu wa sekta ya afya. Alishauri Baraza la Madaktari litumike kuwakutanisha madaktari hao na Serikali.

Mmoja wa madaktari wanafunzi waliofutiwa leseni zao, Dk Adrian George alihoji: “Kama Serikali ilipeleka jambo hili mahakamani inakuwaje tufutiwe usajili wakati shauri bado liko mahakamani?”

Soma zaidi hapa:www.mwananchi.co.tz

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top