Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

AJIRA MPYA ZA WALIMU ZAIBUA MAPYA WIZARANI


Naibu Waziri wa Wizara ya elimu, Philip Mulugo
Ajira mpya za walimu zilizotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zimeibua kashfa baada ya maofisa wa kitengo cha idara ya sekondari cha wizara hiyo kubainika kuingiza majina ya walimu waliokwishaajiriwa tangu mwaka jana.
 
Kutokana na kashfa hiyo, walimu 200 wa Mkoa wa Dar es Salaam na wenzao zaidi ya 300 kutoka mikoa mingine kuandamana, kwenda katika ofisi za wizara hiyo, Ijumaa ya wiki iliyopita na Jumatatu wiki hii.
 
Walimu hao walichukua hatua hiyo baada ya kukosa ajira katika ajira mpya za walimu zilizotangazwa na wizara hivi karibuni licha ya kuwa na sifa zinazostahili baada ya kuhitimu masomo katika vyuo mbalimbali nchini. Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa walimu hao walikosa ajira mwaka huu kutokana na uzembe uliofanywa na maofisa wa kitengo hicho.
 
Baadhi ya maofisa wa wizara hiyo waliozungumza na NIPASHE wizarani hapo, walisema maofisa wa kitengo hicho waliingiza majina ya walimu waliokwishaajiriwa tangu mwaka jana, ambao baadhi wapo masomoni wakijiendeleza.
 
Walisema kasoro hiyo imetokea kutokana na kutokuwa na takwimu za walimu waliopo kazini.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philip Mulugo, alipoulizwa alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo.
 
Alisema wizara yake imeanza kufanya uchunguzi kubaini kama kuna maofisa waliohusika na uzembe huo ili wachukuliwe hatua.
 
“Walimu kutoka Dar es Salaam na mikoani wameandamana kwa nyakati tofauti hapa wizarani kulalamika kukosa ajira. Tunafanya uchunguzi wa suala hili. Tukibaini wapo maofisa waliohusika na uzembe huu wa kuingiza majina ya walimu waliokwishaajiriwa na kuwaajiri upya, nitamshauri waziri wangu tuwawajibishe,” alisema Mulugo.
 
Alisema inashangaza kujitokeza kwa tatizo hilo, ambalo ni la kizembe kwa sababu maofisa wa wizarani kama walikuwa hawana takwimu za walimu walioajiriwa mwaka jana, ambao wamekwenda kusoma, wangepata takwimu hizo kutoka kwa maofisa elimu wa mikoa. Mulugo alisema tatizo lingine lililojitokeza ni kwa baadhi ya vyuo vikuu kutoleta orodha ya walimu waliohitimu katika vyuo vyao ili wapewe ajira. “Vipo vyuo, ambavyo havikuleta majina ya watihimu wa ualimu katika vyuo vyao ili waweze kuajiriwa.
 
 Lakini nao huu ni uzembe wa baadhi ya maofisa wa Wizara ya Elimu kwa kushindwa kufanya ‘follow-up’ (kufuatilia) vyuoni wakati wameajiriwa hapa wizarani kwa kazi hiyo,” alisema Mulugo.
 
Februari 13, mwaka huu, wizara hiyo ilitangaza ajira za walimu wapya 26,537 kwa mwaka 2012/2013 watakaosambazwa katika shule mbalimbali.
 
Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema kati ya ajira hizo, 13,527 ni kwa shule za msingi, 12,973 sekondari na vyuo vya ualimu na 41 shule za msingi za mazoezi zilizopo chini ya wizara.
 
CHANZO: NIPASHE
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top