Adai
serikali haijalenga wafanyabiashara waliosaidia upinzani kwenye
kampeni. Asema hataki kuwa waziri ombaomba kwa madai nchi nyingine
zinalazimisha kukubali ndoa za jinsia moja ili upate msaada
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.
.....................
Januari Mosi, mwaka huu, akitoa salamu za mwaka mpya katika Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Monduli, Lowassa
alisema amepokea malalamiko ya kuwapo kwa uonevu na vitisho kwa wadau
walioonekana kuunga mkono vyama vya upinzani wakati wa kampeni.
Alisema hali hiyo ilitokea ilhali hatua ya wafanyabiashara hao
haikukiuka Katiba, hivyo kuzitaka idara zinazohusika kuchukua hatua ili
kuepusha matatizo yasiyo ya lazima.
“Imeanza kutokea tabia ya kuwalaumu na 'kuwa-harass' (kuwasumbua)
wale waliounga mkono vyama vya upinzani. Wanawa-harass kwenye kodi,
nasikia wanawa-harass kwenye miradi na hata mitaani, hili si jambo
zuri,” alisema Lowassa.
DK. MPANGO AMJIBU
Jana, Dk. Mpango akizungumza na wafanyabiashara kwa lengo la
kufahamiana na kuelezana mikakati ya serikali, alisema operesheni
iliyoendeshwa bandarini kwa wafanyabiashara waliokwepa kulipa kodi,
haikuwa na lengo la kuwabana wale waliosaidia upinzani wakati wa
uchaguzi mkuu.
Alisema hatua ya serikali ya kukusanya kodi kwa nguvu kwa wafanyabiashara hao haikuwa na lengo la kuwanyanyasa.
“Dhana iliyopo sasa kuwa hatua iliyochukuliwa na serikali bandarini
ya makontena kuwa iliwalenga baadhi ya wafanyabiashara waliousaidia
upinzani, si ya kweli,” alisema.
Kauli hii ya Dk. Mpango inatafsiriwa ilikuwa ikimjibu kumjibu
Lowassa kwa kuwa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu ni kiongozi huyo
pekee aliyekuwa akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), ndiye alijitokeza hadharani na kulalamikia kunyanyaswa
kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiunga mkono upinzani wakati wa
kampeni.
Akizungumza na wafanyabiashara hao jana, Dk. Mpango alisema
serikali ya awamu ya tano inatambua mchango wa wafanyabiashara hivyo
itashirikiana nao katika kujenga uchumi wa nchi.
Alisema dhana kuwa hatua iliyochukuliwa na serikali bandarini
iliwalenga wafanyabiashara waliowasaidia wapinzani wakati wa kampeni si
ya kweli.
“Serikali ya Rais Dk. John Magufuli inatambua umuhimu wa uwekezaji
katika uchumi wa nchi. Dhamira yangu ni kufanya kazi na wafanyabaishara
wakubwa na wadogo,” alisema Dk. Mpango.
Alisema serikali ya Rais Magufuli haitawavumilia wafanyabiashara
wachache ambao wanakwepa kodi na kuwataka waache tabia hiyo mara moja
kwa kuwa itatumika sheria na hakuna mfanyabishara yeyote atakayeonewa.
Alisema kama kutakuwa na mfanyabishara atakayeonewa na mfanyakazi
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), atoe taarifa wizarani haraka.
Aliongeza kuwa hapendi kuwa waziri ombaomba kwa kuwa amechoka
kuwasindikiza wengine na kusema masharti ya kuomba misada ni makubwa na
mengine hayatekelezeki, akitolea mfano wa kukubali sheria ya ndoa ya
jinsia moja.
Alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwahudumia wanachi
kwa kuwapa huduma bora za kijamii pamoja na kuwa na uchumi imara, kuziba
mianya ya ukwepaji kodi na kukusanya mapato.
Katika hatua nyingine, Dk. Mpango aliwaambia wafanyabiashara hao
katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, serikali itafuta ushuru na tozo
ndogo ndogo ambazo zimekuwa kero kwa wafanyabiashara.
Kadhalika, alisema bajeti hiyo itajielekeza katika kujenga uchumi
imara wenye viwanda, miradi mikubwa itakayoleta matokeo makubwa na ajira
nyingi pamoja na maeneo wezeshi kwa ajili ya kujenga viwanda kama vile
uwapo wa umeme wa uhakika, bandari na ardhi.
Dk. Mpango alisema serikali imeziagiza taasisi zake zinazojihusisha
na tozo kuorodhesha na kuleta aina zote za tozo ambazo wanatoza ili
kuzifuta.
Alisema serikali ya awamu ya tano inatambua umuhimu wa uwekezaji
katika uchumi, hivyo itashirikiana na wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
Waziri huyo alisema katika bajeti ijayo serikali itajielekeza
katika viwanda ambavyo malighafi zake zinapatikana nchini kama vile
misitu, uvuvi, madini na kilimo.
Dk. Mpango alisema kutajengwa viwanda vikubwa vitakavyoweza kuajiri
idadi kubwa ya watu kama vile kiwanda cha nguo, viatu na mafuta ya
kupikia.
Alisema kwa sasa msajili wa hazina ameshaelekezwa na ameanza
kufanya uchambuzi kwa viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyi kazi
inavyotakiwa.
Dk. Mpango alisema serikali itawanyang’anya wamiliki wa viwanda hivyo na kuwapatia wabia ambao wanaweza kuviendeleza.
Alisema bajeti ijayo pia itajielekeza katika ujenzi wa reli ya kati
ya kisasa ambayo inahitaji Sh. trilioni nane hadi tisa kukamilisha
ujenzi wake, na serikali haiwezi kujenga kwa fedha za bajeti.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri na Sera kutoka Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Felix Mosha, alisema serikali inapaswa
kutafuta mfumo ambao utalinda viwanda vya ndani, pamoja na utaratibu wa
kuwekeza katika kilimo.
Alisema hakuna taifa litakalokuwa kiuchumi bila ya kuwekeza katika kilimo.
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen
Ngatunga, alisema tozo nyingi ambazo wafanyabishara wanatozwa, hazina
umuhimu wowote.
Alisema bandarini kuna majangili wengi wa ushuru na kodi, huku
akipendekeza malipo yote kulipwa kwa shilingi badala ya dola na kuongeza
kuwa TRA inapaswa kukusanya tozo ya kuhifadhi mizigo bandarini badala
ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment