Na Frank Leonard, Mafinga.
MBUNGE Mteule wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi ameanza
kuikumbuka jamii anayoiongoza kwa kutoa fedha taslimu na bidhaa
mbalimbali kwa wanafunzi walemavu wanaosoma shule ya msingi mchanganyiko
Makalala ya mjini Mafinga.
Bidhaa hizo ni pamoja na mafuta kwa ajili ya albino, na miwani, dawa
za meno, sukari, sabuni, shampoo, fagio, pipi, mikate, biskuti na Sh
100,000 zitakazotumika kununua nguo za ndani za watoto 23 walemavu
wanaosoma shuleni hapo.
Akikabidhi bidhaa hizo kwa wanafunzi hao, Chumi alisema; “badala ya
kuchinja mbuzi na kula na timu yangu ya kama wanavyofanya wengine katika
kusheherekea ushindi wao, mie nimeingia kazini, tuwakumbuka watoto hao
na tukaamua kuchangishana na kununua vitu hivi vichache kwa ajili yao.”
Chumi alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo jipya mkoani Iringa kwa
kupata kura 18,379 dhidi ya kura 12,834 alizopata mshindani wake wa
jirani, William Mungai wa Chadema na kura 208 za mgombea wa ACT
Wazalendo, Mwangiri Mwangiri.
“Nimeanza kwa kuwakumbuka watoto hawa walemavu wa shule hii,
nitaendelea kufanya hivyo kwao na kwa wengine kila ninapopata fursa ya
kuchangia mahitaji yao. Kazi hiyo itakwenda sambamba na kusimamia
utekelezaji wa Ilani yetu ya CCM ili zile ahadi zetu zote tulizoahidi
wakati wa kampeni zitekelezwe,” alisema.
Chumi alisema jimbo la Mafinga Mjini lina fursa nyingi za kiuchumi
ambazo kama zitatumika vizuri zitasaidia kupunguza changamoto mbalimbali
za kimaendeleo zinazowakabili watu wa jimbo hilo.
Kwa upande wake aliyekuwa kampeni meneja wa mbunge huyo mteule,
Albert Chalamila aliutaka uongozi wa shule hiyo kwa kushirikiana na timu
Chumi, kuandika andiko la mradi na kuliuza kwa wafadhili ili wasaidie
maendeleo ya wanafunzi walemavu wanaosoma shuleni hapo.
Akishukuru kwa msaada huo, Mkuu wa shule hiyo, Shem Muheni alisema;
“msaada huu unawaongezea faraja wanafunzi hawa kama mnavyowaona
wamefurahishwa na hivi vyote mlivyowaletea na kila mmoja anataka apate.”
Alisema wanafunzi hao wanaotoka katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma,
Njombe, Iringa na Morogoro wanahitaji misaada wa hali na mali kutoka
katika makundi mbalimbali ya jamii ili kukamilisha pale panaposhindwa
kukamilishwa na serikali kwa wakati muafaka.
“Watoto hawa wana mahitaji mengi, na baadhi yake ni ya gharama kubwa,
kwahiyo ni jambo la kheri pale wadau mbalimbali wa maendeleo
wanapojitokeza na kuwasaidia ili nao waweze kukamilisha ndoto zao za
kupata elimu wanayoihitaji,” alisema na kumshukuru Chumi kwa msaada huo.
Muheni alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 ilianza kwa
kupokea wanafunzi wasioona mwaka 1974 kabla ya kuanza kuchukua watoto
wenye mtindio wa ubongo na walemavu wengine miaka iliyofuata.
Post a Comment