Aliyekuwa Kocha wa Yanga,Tom Saintief
1.Kocha ni mkaidi
"Kocha amekuwa mkaidi na mtu asiyetii maagizo halali ya uongozi wa juu. Tulikubaliana kwamba timu ikitoka Mbeya kucheza na Prisons ifikie kambini Morogoro siku mbili kabla kujiandaa na mechi inayofuata dhidi ya Mtibwa, kocha akakataa akaamuru timu irudi Dar es Salaam.
"Sisi tuliona hakukuwa na sababu ya msingi ya kuleta timu huku halafu unaachia wachezaji wanakwenda mtaani halafu siku inayofuata unawakusanya tena unawarudisha Morogoro ni kupoteza pia muda," alisisitiza Sanga.
2.Wachezaji kulewa
"Baada ya mechi na Prisons aliruhusu wachezaji waende klabu kulewa na tukamwuliza akakiri kwamba aliwaruhusu. Hilo ni kosa, huwezi kuruhusu wachezaji waende kulewa wakati siku chache baadaye una mchezo mwingine mgumu dhidi ya Mtibwa Sugar.
"Kwa utaratibu na wachezaji wetu wa Kitanzania ukiwaruhusu waende klabu ni kama unawaambia wakafanye wanachokitaka halafu siku inayofuata timu inasafiri umbali mrefu kurudi Dar es Salaam halafu huko nako unawaachia tena waende nyumbani. Huo si utaratibu," alisema Sanga.
3.Nidhamu
"Alishindwa kudhibiti nidhamu za baadhi ya wachezaji mambo yalikuwa yanakwenda tu ilimradi na hii ndiyo imechangia hata timu kufanya vibaya kwenye hizi mechi za kwanza za ligi, sasa sisi hatuwezi kuendelea kuvumilia ili baadaye tuje kulaumiwa na wanachama," alisisitiza.
4.Hataki kambi
"Uongozi tunataka timu ikae kambini angalau wiki moja ili kudhibiti wachezaji na utendaji wao na tufanye vizuri kwenye ligi lakini yeye anakaidi anakwambia hata Barcelona, Manchester United hazikai kambini wiki nzima.
"Anataka wachezaji wakae kambini siku mbili au tatu kitu ambacho kwa mazingira yetu hakiwezekani. Huwezi kuleta mambo ya Ulaya kwa wachezaji wa mazingira kama yetu, utavurunda kila siku.
"Lakini ulikuwa ni ugomvi na malumbano ya kila mara, kocha hataki kambi, ameikuta Yanga ikiwa na utaratibu wake wa kuweka kambi na ilikaa kambini muda mrefu mpaka ikatwaa na ubingwa wa Kagame. Lakini huo utamaduni hautaki anataka kuufuta na sisi hatuafiki. Hii ni Yanga bwana si Barcelona, ukisema umwachie mchezaji azurure mtaani siku zote ni matatizo tutakuwa tunafungwa kila siku hapa."
5.Anakiuka maadili
"Yanga ina miiko yake na ina taratibu zake za kufanya kazi za kila siku, kocha ana mamlaka yake ambayo hayaingiliwi na mtu yeyote lakini anapaswa kufuata maadili ya Yanga ukiambiwa hiki hakifai ni kweli hakifai, msikilize mkuu wako, huu mvurugano wa hapa na pale ulikuwa unaiingiza klabu kwenye gharama zisizo na maana.
Mambo mengine ni ya ndani alikuwa anafanya ambayo hatuoni kuna haja ya kuyaweka kwa umma. Amefikia mpaka hatua ya kutoa siri za wachezaji hadharani."
6.Hashikiki
"Kocha amekuwa na nguvu kubwa sana kuliko mtu yeyote yule yaani amekuwa hashikiki, amekuwa kama mtu ambaye kila mtu yuko chini yake na kila anachosema hataki kupingwa, hatuwezi kufanya kazi hivyo lazima kocha awe na nguvu kama ya mwajiriwa yeyote wa Yanga.
Hatuwezi kuendelea kukaa na kocha ambaye hatuwezi kumdhibiti itatuletea matatizo siku zijazo na kwanini tufike mbali kiasi hicho wakati tunaweza kumdhibiti mapema? Ndiyo maana tumesitisha mkabata wake aondoke na hata kama akija mwingine akiwa na tabia kama zake tutamtoa, hatuwezi kukubali kuwa na mtu ambaye hatummudu."
7. Alivunja sahani Mbeya
"Kwenye hoteli tuliyofikia kule Mbeya alifanya vitu vya ajabu sana kagombana na watu na amevunja vifaa ikiwamo sahani na sasa Yanga ina deni kule Mbeya, kwanini tufikie huko? Kama kocha unashindwa kujiheshimu wachezaji watakuwaje?"
8.Visingizio vingi
"Hatujaridhishwa na kiwango cha timu na jahazi linazidi kuzama, lakini ukiangalia kwa upande mwingine visingizio ni vingi. Mbeya alisingizia kwamba wachezaji walilala mzungu wa nne ndiyo maana timu haikushinda, tukakubali.
Morogoro tukamwonyesha kila kitu na akaridhia, hatimaye tukapigwa mabao tatu akaanza kusema hawana bahati na mambo mengine kibao ambayo sisi tulivyosoma ripoti yake hatukuridhika na hali ya mambo inavyokwenda na tumemwita tukazungumza naye kumueleza."
9. Anaongea hovyo
"Alianza kutoa siri za klabu na wachezaji tukamuonya na tumeshukuru kidogo kwamba alishaanza kuelewa lakini tumeona kwamba hakuna haja ya kuendelea kuwa naye."
10. Kujibizana na viongozi
Ingawa Sanga hakutaka kuingia kiundani, Mwanaspoti linajua kwamba kauli za matusi na majibizano makali kati yake na kigogo mmoja wa juu wa Yanga ndivyo vilivyochangia kumwondoa.
Aliamuru hapo hapo kwamba mkataba wake usitishwe kuanzia siku inayofuata ambayo ni jana Jumamosi.
Hata hivyo Sanga alitetea kuwa: "Kulikuwa na majibizano ya kawaida ambayo ni mambo ya ndani ya kikao."
Chanzo:Mwanaspoti.
Post a Comment