JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII TAARIFA KWA UMMA
WATU WALIOVAMIA PORI TENGEFU LA KILOMBERO WAMETAKIWA KUONDOKA IFIKAPO TAREHE 31 AGOSTI 2012
Watu
waliovamia na kuishi katika Pori Tengefu la Kilombero wametakiwa kutoka
kwenye eneo hilo kwa hiari yao kabla ya tarehe 31 Agosti 2012. Watu hao
ni wale ambao hawajaondoka baada ya kutakiwa kufanya hivyo mara kwa
mara.
Azimio
hilo lilifikiwa katika kikao cha pamoja kati ya uongozi wa Wilaya za
Kilombero na Ulanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi
Maimuna Tarishi kilichofanyika Kilombero tarehe 14 Agosti 2012. Nia ya
kikao hicho ilikuwa ni kuweka mikakati ya kutekeleza azama ya Serikali
ya kuwataka wavamizi katika Pori Tengefu la Kilombero kuondoka katika
eneo hilo.
Wengine
waliohudhuria kikao hicho ni Ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Francis Miti,
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero Evarist Mmbaga, Mtendaji wa Wilaya
ya Kilombero, Azimina Mbilinyi na watendaji wengine kutoka Wilaya za
Kilombero na Ulanga.
Kikao
hicho kiliamua kuwa ifikapo tarehe 8 Septemba, 2012 kazi ya kuwatoa
wavamizi ambao bado watakuwepo katika pori hilo itaanza. Kazi hiyo ya
kuwaondoa itatekelezwa kwa pamoja na Kamati za Usalama ngazi ya Mkoa na
Wilaya za Ulanga na Kilombero, Kikosi Dhidi ya Ujangili, Askari Polisi
na Askari kutoka Pori la Akiba Selous.
Hadi
sasa wanachi wameelimishwa kuhusu umuhimu wa Pori Tengefu la Kilombero
na manufaa yatakayopatikana kama litaachwa wazi. Wanavijiji wanaopakana
na Pori hilo wameonyeshwa mipaka baina ya vijiji vyao na Pori.
Aidha
mipango imekamilika ya kuiwekea mifugo alama (brandas) kwa lengo la
kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyoko katika
Bonde la Kilombero. Kazi hii inaratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Vilevile
kazi ya kutambua mipaka, kufyeka, na kuweka alama (beacons) zinaendelea
kwa pamoja katika vijiji 105 vya Wilaya za Ulanga na Kilombero na
zinategemewa kukamilika tarehe 27 Agosti, 2012. Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na utalii aliahidi kuwa Wizara itachangia Shs. 106,500,000
ili kuharakisha utekelezaji wa kazi hiyo ya kuimarisha mipaka.Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii amevitaka Vijiji vinavyopakana na
Pori hilo kuanzisha Jumuiya za Kuhifadhi Wanyamapori (WMA) ili
kuimarisha ulinzi wa hifadhi hiyo dhidi ya wavamizi. Pia, kupitia WMA
jamii husika zitapata manufaa kiuchumi kutokana na matumizi ya
rasilimali za wanyamapori zilizopo.
Vilevile
kila kijiji kimetakiwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ambao,
pamoja na mambo mengine, utaonyesha maeneo ya malisho ya mifugo.
George Matiko
MSEMAJI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
MSEMAJI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Post a Comment