Fina na January Makamba baada ya kipindi cha Makutano
----
Mbunge wa Bumbuli na Naibu waziri wa mawasiliano sayansi na
teknolojia Mhe January Makamba amesema hana mpango wa kugombea Urais. Makamba
aliyasema hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha Makutano kinachoendeshwa na
Fina Mango. Alisema anaamini nafasi ya urais inahitaji mtu ambaye amejiandaa
Kisaikolojia, Kisiasa na Kifikra na kumalizia kwa kusema kuwa Urais sio uamuzi
wa mtu mmoja kwa sababu nchi haiendeshwi na mtu mmoja na inahitaji watu ambao
wanashauriana, kuandaa dira ya pamoja na kupeleka ujumbe wa kuwaunganisha
Watanzania.
Alipoulizwa Rais anayekuja anatakiwa aweje alisema anatakiwa awe ni
mtu atakaewaunganisha Watanzania huku akisema mianya ya ukabila, udini na
rushwa ambayo baba wa taifa Mwalimu Nyerere aliitaja imeanza kuonekana. Pia
Makamba alisema rais ajaye anatakiwa asiwe mtu mwenye hulka ya visasi na
atakiwa awe na uwezo wa kuwaambia
wananchi kuwa yeye sio masiha wa kuyafanya maisha yao yabadilike papo kwa hapo
kwa kuwa nchi ni ya watu wote, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutumia nafasi
yake kuleta mabadiliko
Alipoulizwa katika wanasiasa wa upinzani ni yupi anamkubali,
alimtaja Zitto Kabwe kwa sababu ana uwezo wa kusema na kusimamia kile
anachokiamini, ujasiri wa kuomba ushauri kama kuna jambo ambalo halielewi na
pia anapenda kusoma na kujifunza. Pia alitaja kuwa anamheshimu sana Profesa
Ibrahim Lipumba.
Mheshimiwa Makamba
alimalizia kwa kusema kuwa atagombea ubunge wa Bumbuli kwa kipindi cha
pili na baada ya hapo atajikita katika shughuli za Shirika la Maendeleo ya
Bumbuli (Bumbuli Development Corporation) alilolianzisha likiwa na lengo la kuleta
washirika wa maendeleo ili kuwawezesha kiuchumi wananchi bila kutegemea miradi
ya serikali
Post a Comment