Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini,Godbless Lema(CHADEMA) akipanda kwenye gari yake baada ya rufaa yake kuahirishwa tarehe 23/09/2012 ili kusomwa leo.(Picha na Maktaba yetu)
...................................
RUFAA ya kupinga kuvuliwa ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), inatarajiwa kusikilizwa leo na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande.
Majaji wengine waliopo katika kusikiliza rufaa hiyo inayovuta hisia za watu wengi ni pamoja na Jaji Natalia Kimaro na Salum Massati, wote wa Mahakama ya Rufaa nchini.
Rufaa hiyo ambayo ilipaswa kusikilizwa Septemba 23, mwaka huu, ilisogezwa mbele hadi Oktoba 2, kutokana na mawakili wa pande zote mbili kupatwa na dharura, ambapo jopo hilo liliridhika na hivyo kusogeza mbele tarehe.
Jopo hilo lilizingatia barua iliyoomba kusogezwa mbele kwa shauri hilo hadi Oktoba 2, kutokana na mawakili, Tundu Lissu, anayemtetea Lema na kaka yake, Alute Mughwai, anayewatetea walalamikaji kufiwa na baba yao mzazi.
Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), anashirikiana na Wakili Mwandamizi Method Kimomogoro katika kumtetea mrufani, Godbless Lema.
Kwa upande wake Wakili Mughwai anashirikiana na Wakili Modest Akida kuwawakilisha wadaiwa katika shauri hilo ambao ni wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo.
Wanachama hao walifungua shauri lililotengua ubunge wa Lema wakidai kuwa wakati wa kampeni alimdhalilisha aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian, kwa kutumia lugha za matusi.
Awali, Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, anayesaidiana na Lissu, aliwasilisha katika mahakama hiyo hoja 18 za madai, akipinga ubunge wake kutenguliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.
Katika baadhi ya madai hayo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, huku akiitaka mahakama hiyo imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.
Aidha, aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika shauri hilo walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na gharama za kesi iliyomalizika katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Katika madai mengine, Lema anamlalamikia Jaji Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo kuwa alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi, huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo
Chanzo: Mtanzania
Post a Comment