Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

CCM YAJIPIMA KWA CHADEMA

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa chama hicho kujaribu kukabiliana na upinzani wa CHADEMA mikoani, ambapo mwaka jana baada ya mkutano wao wa maazimio ya kujivua gamba, walijitahidi kuzunguka baadhi ya mikoa bila kufua dafu.

Operesheni zinazofanywa na CHADEMA za Sangara na sasa Vuguguvu la Mabadiliko (M4C), zimeitikisa CCM na hivyo wajumbe wake kutumia muda mwingi kwenye mkutano mkuu wao uliomalizika mjini Dodoma, kujitapa kuwa lazima wafanye mashambulizi ya kuwasambaratisha.

Akitangaza mkakati huo mpya jana kwa waandishi wa habari wa kuchanja mbunga kwa kutumia anga kwa helikopta kama CHADEMA, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema wameanda ziara ya siku nne katika mikoa minne.

Alisema ziara hiyo itaongozwa na sekretarieti mpya chini ya Katibu wake Mkuu, Abdullahman Kinana, na kuwashirikisha baadhi ya mawaziri.

Nape alisema kuwa ziara hiyo ni ya chama na sio ya kiserikali na kwamba itaanza kesho hadi Novemba 24 katika mikoa ya Mtwara, Arusha, Geita na Rukwa.

Akifafanua zaidi alisema Kinana ataanzia Mtwara ambako atakuwa na mawaziri husika wanaoshughulikia masuala ya kilimo ili kuzungumzia zao la korosho na waziri wa uchukuzi atakayezungumzia bandari na miundombinu.


Nape aliongeza kuwa wakiwa Sumbawanga watazungumzia miundombinu na kwa Geita watafuatilia migogoro ya migodi na kumalizia Arusha kwa kuangalia harakati za kufufua viwanda kwani vinaathiri ajira.

Nape alisema kuwa lengo la kuongozana na baadhi ya mawaziri ni kutoa maelezo ya papo hapo hasa kwa mambo yanayosuasua ikiwemo kuwawajibisha bila kusubiri Bunge kufanya hivyo.

“Lengo tunasukuma spidi ya utekelezaji wa maendeleo na ilani ya uchaguzi na tunajikita kwa baadhi ya mambo na kuendeleza mageuzi ndani ya chama na ndio azimio tuliloondoka nalo katika mkutano mkuu wa nane,” alisema.

Akizungumzia kung’atuka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama, Nape alisema kiongozi huyo ameondoka ili akasimamie uanzishwaji wa chuo cha uongozi cha CCM, ambacho kitasaidia makada kuwa na nidhamu na uwajibikaji.

Akijibu hoja za CHADEMA zinazodai CCM imetekeleza ilani ya chama hicho hususan katika suala la elimu na kupunguzwa kwa bei za vifaa vya ujenzi, Nape alisema kuwa suala la elimu bure ni la CCM.

“Suala hilo lilianza wakati wa TANU chini ya Mwalimu Julius Nyerere na hata hao kina Dk. Slaa wamesomeshwa bure na TANU,” alisema.

CHADEMA wajiimarisha

Wakati CCM ikianza ziara mikoani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeanza kujiimarisha kwa kuendesha mafunzo ya darasani na vitendo, kwa lengo la kuwajengea uwezo wenyeviti na makatibu wa mikoa 32 ya kichama.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Benson Kigaila, alisema kuwa mafunzo hayo yatafanyika Novemba 22 hadi 23, mwaka huu, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.

Kigaila alisema baada ya mafunzo hayo wataingia kwenye vitendo ambapo makatibu na wenyeviti hao watasambaa kushambulia vitongoji na vijiji vyote vya wilaya ya Karagwe, kwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo hayo.

Alibainisha kuwa mafunzo hayo ya vitendo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya ujenzi na uimarishaji wa chama, hususan operesheni ya M4C ambayo imesaidia viongozi kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya ndani na hadhara.

Kuhusu M4C, Kagaila alisema wakati viongozi hao waliopata mafunzo wakiendelea, chama kitatoa ratiba ya operesheni hiyo kubwa itakayoendelea kufanyika kwa nchi nzima.

Habari hii imeandaliwa na Happiness Mnale na Shehe Semtawa

Chanzo; Chadema.blog
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top