Na Ezekiel Kamwaga
MWENYEKITI
wa klabu ya Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, amepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa za msiba wa aliyekuwa msanii maarufu wa muziki na filamu, Hussein
Ramadhani Mkiety, maarufu kwa jina la Sharo Milionea, kilichotokea jana usiku
mkoani Tanga.
Kwa niaba ya
klabu ya Simba na kwa niaba yake binafsi, Mwenyekiti anapenda kutuma salamu za
pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu
kutokana na msiba huu mkubwa sana si kwao pekee bali kwa taifa zima la
Tanzania.
Sharo Milionea
hakuwa msanii wa kawaida. Yeye ni miongoni mwa kizazi kipya cha vijana wa
Kitanzania walioamua kutafuta maisha kwa kutumia vipaji walivyopewa na Mungu.
Yeye alijitumbukiza zaidi katika uchekeshaji na baadaye akaonyesha uwezo mkubwa
katika fani ya muziki.
Sharo
alikuwa maarufu kiasi kwamba makampuni makubwa yalikuwa yameanza kumtumia
kwenye matangazo yao ya kibiashara. Hii ilionyesha kwamba makampuni yalibaini
faida itakayopatikana kwao kwa kumtumia msanii huyu ambaye bado alikuwa na
heshima kubwa kwenye jamii kutokana na haiba yake na uwezo wake kwenye kazi
alizokuwa akifanya.
Msiba huu
umekuwa pigo kubwa kwa tasnia ya filamu ambayo bado inaomboleza vifo vya
wasanii kama Steven Kanumba, Mlopelo na John Steven Maganga, waliofariki dunia
mwaka huu pia.
"Ifahamike
kwamba Sharo Milionea alikuwa miongoni mwa wasanii wa Kitanzania waliotuma
maombi Simba ya kutaka kushiriki kwenye mchakato wa kutengeneza wimbo rasmi wa
klabu ya Simba. Yeye alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiumizwa na
ukweli kwamba klabu kama Simba inashindwa kufanya biashara ya kuuza nyimbo zake
ilhali wanunuaji wapo," alisema Rage.
Kwa klabu ya
Simba, namna pekee ya kumuenzi marehemu ni kufanyia kazi mambo ambayo alikuwa
akitushauri kwenye eneo la biashara. Ni matumaini yetu kwamba iwapo tutafanya
lile alilokuwa akitushauri, atakuwa mwenye amani huko alikotangulia mbele ya
haki.
Rage
amewaomba wasanii wa tasnia ya filamu na muziki kuwa watulivu na wenye subra
kwenye kipindi hiki kigumu kwao. Kila kitu katika maisha ya wanadamu kinapangwa
na Mwenyezi Mungu na ndiyo maana Waswahili wana msemo kuwa Kazi ya Mungu haina
makosa.
Mola na
ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Hussein Ramadhani Mkeity
(Kamwaga
ni Ofisa Habari wa Simba SC).
Post a Comment