Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam
--
Kamati
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi iliyokutana juzi Mjini Dodoma imeipongeza
serikali kwa hatua inayoendelea kuchukua katika kuchunguza chanzo cha
tukio la mlipuko wa Bomu uliotokea Kanisani Jijini Arusha.
Bomu
hilo lilirushwa Mei Tano mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Kanisa la
Romani Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olisiti na
kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi kadhaa.
Akizungumza jana Jijini Dar es salaam Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi
NAPE NNAUYE ameeleza kuwa taarifa hiyo ya serikali iliwasilishwa jana
katika kikao hicho na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dokta EMMANUEL
NCHIMBI .
Kufuatia tukio hilo, Kamati Kuu imelaani na imeitaka serikali
kuharakisha uchunguzi pamoja na kuongeza kasi ya uchunguzi wa suala hilo
sanjari na kutafuta mzizi wa matukio hayo pamoja na kutoa taarifa mara
kwa mara kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa tukio hilo.
Hata hivyo Kamati Kuu imewapongeza viongozi wa Madhehebu ya Dini
nchini kwa kuweza kuwaelekeza waumini wao kuhusu mlipuko huo na kuweza
kusimamia amani na utulivu tangu kutokea kwa tukio hilo.
Pia Kamati Kuu imewataka viongozi wa kisiasa nchini kuliachia Jeshi la Polisi liendelee na kazi ya upelelezi wa tukio hilo.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi-CCM, Rais JAKAYA
KIKWETE wiki ijayo anatarajia kukutana na Wabunge wote wa CCM Mjini
Dodoma katika kikao cha kazi. Kikao hicho kitakuwa ni cha siku Mbili
kuanzia Mei 18 na 19 mwaka huu. Katika kikao hicho, Wabunge watatumia
fursa hiyo kutoa maoni yao kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2010/2015 katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika Majimbo
yao ya Uchaguzi.
NAPE amefafanua kuwa Chama Cha Mapinduzi kimekuwa na utaratibu wa
kukutana na Wabunge wa Chama hicho ili kujadili masuala yanayohusu nchi
likiwemo suala la utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ambalo ndio Dira ya
maendeleo ya wananchi.
Pia amesisitiza kuwa kuitishwa kwa kikao hicho hakuna uhusiano na suala
la aina yoyote ya kuwawajibisha Wabunge wa CCM kinidhamu bali ni mkutano
wa kawaida na wa kazi.
Mara baada ya kikao hicho cha Wabunge wa CCM, Kamati Kuu ya CCM
itakutana kwa siku Mbili Mjini Dodoma kuanzia Mei 20 hadi 21 mwaka huu.
Post a Comment