Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif
Sharrif Hamad amesema ataomba tena kugombea urais kupitia Chama cha
Wananchi (CUF) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45
kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV, Maalim Seif alisema kuwa
anachoomba tu Mwenyezi Mungu ampe afya njema.
“Ni uamuzi wa wananchi na wanachama wenyewe wa CUF
lakini kama Mwenyezi Mungu akinipa afya na uzima bado nia ipo,” alisema
Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Alisema hivi sasa chama hicho kimekuwa
kikijiimarisha visiwani huko kwa kufanya mikutano Pemba na Unguja ili
kuhakikisha kinaendelea kukubalika kwa wananchi.
Kauli hiyo ya Maalim Seif ambaye amekuwa akiwania
nafasi hiyo tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi, ilipokewa kwa hisia
tofauti ambapo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bashiru Ali
alisema vyama vya siasa ni lazima viwe vinatayarisha viongozi wa baadaye
ambao watafahamu kwamba uongozi ni dhamana wanayopewa na wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema
Maalim Seif kama mwanachama wa chama hicho anaruhusiwa kwa mujibu wa
Katiba kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa dola
NA MWANANCHI
Post a Comment