*Adai ni vibaraka wa mabeberu kuvuruga nchi
*Awafananisha na nguruwe mwenye tabia la kula watoto akiwa na njaa.
*Ataka watanzania kuwapuuza
*Amuumbua Tundu Lissu
*Atetea mchakato wa katiba nchini
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeibuka na kusema kuwa madai yaliyotolewa
bungeni dhidi ya chama chao hayana ukweli huku akimtupia kombora mbunge
wa Singida Mashariki Tundu Lissu (CHADEMA), kwa kinachombusmbua yeye na
baadhi ya viongozi wenzake ni ugonjwa wa kifafa cha siasa.
Kauli hiyo ya CCM imekuja siku chache baada ya msemaji wa kambi ya
upinzani bungeni Tundu Lissu, kudai kuwa CCM ilimeteka nyara mchakato wa
Katiba katika hotuba yake aliyoitoa bungeni Mei 3, mwaka huu ikiwemo
kuandika barua kwa viongozi wake wa ngazi za mikoa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema
hatua ya Lissu haina mashiko mbele ya Watanzania kwani wajibu wa CCM
ni kuhakikisha nchi inapata katiba iliyokubalidika na wananchi bila
kupata shinikizo kutoka mawakala wa mabeberu na kwamba CCM Kama ilivyo
taasisi yoyote makini na yenye uzalendo kwa nchi yao, katika mchakato
wa uundwaji wa katiba mpya ina jukumu la kuwahamasisha wanachama na
wasio wanachama wake kushiriki mchakato wa katiba nchini kutokana na
kutambua umuhimu wake.
Alisema tofauti kati ya CCM na CHADEMA katika hilo ni wakati CCM
wanahamasisha watu washiriki kwenye mchakato wa katiba nchini, wao
wanahamasisha watu wavuruge au wasishiriki kabisa mchakato wa kupatikana
Katiba mpya ya nchi.
IFUATAYO NI TAARIFA KAMA ILIVYOTOLEWA NA NAPE
IFUATAYO NI TAARIFA KAMA ILIVYOTOLEWA NA NAPE
Ijumaa iliyopita Mei 3, 2013 Msemaji wa kambi ya Upinzani Bungeni
Masuala ya katiba na Sheria Ndg. Tundu Lissu katika hotuba yake pamoja
na kuzishutumu taasisi zingine, lakini pia alitoa tuhuma kadhaa dhidi ya
CCM.
Tuhuma hizo zilielekezwa kwenye maeneo kadhaa hasa yahusuyo suala la
mchakato wa uundwaji wa katiba mpya unaoendelea nchini na ushiriki wa
makundi tofauti katika mchakato huo.
Katika kuipa uzito hoja hiyo, Lissu alitoa malalamiko mengi dhidi ya CCM
kwa madai kuwa tumeteka mchakato huo kwa kujaza Makada wa CCM katika
Mabaraza ya Katiba yaliyoundwa kwenye ngazi ya kata hivi karibuni.
CCM Kama ilivyo taasisi yoyote makini na wenye uzalendo kwa nchi yao,
katika mchakato wa uundwaji wa katiba mpya ina jukumu la kuwahamasisha
wanachama na wasio wanachama wake kushiriki mchakato wa katiba nchini
kutokana na kutambua umuhimu wake.
Tofauti ya CCM na Chadema katika hili ni, wakati CCM tunahamasisha watu
washiriki kwenye mchakato wa katiba nchini, Chadema wao wanahamasisha
watu wavuruge au wasishiriki kabisa mchakato huu.
Mfano mzuri ni jitihada zao za kuziria mchakato huu kwa visingizio vya
kitoto kabisa. Juhudi zao za kumtaka Prof. Baregu, Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Chadema, ambaye wao Chadema walimpendekeza kwenye tume, ajitoe kwenye
tume zinafahamika na wala sio SIRI.
CCM inampongeza kwa dhati Prof. Baregu kwa uzalendo na ukomavu wa
kisiasa aliouonyesha kwa kuwakatalia kujitoa kwenye tume na kuweka mbele
masilahi ya taifa lake. Kukataa kwa Prof. Baregu kujitoa kwenye tume
kwa hoja za kitoto kabisa za Chadema ilipaswa kuwa fundisho kwa vibaraka
hawa.
Ilivyo fanya CCM, kuhamasisha wanachama na watanzania kwa ujumla
kushiriki mchakato huo, ndivyo taasisi nyingine pia zilivyofanya.
Zikiwemo taasisi za dini ambazo zimekuwa zikihamasisha zoezi hili
kupitia mikusanyiko ya Ibada, Taasisi zisizo za Kiserikali yaani NGOs
kwa kufanya makongamano na makundi mengine kwa kuendesha midahalo,
dhambi kwa CCM inatoka wapi?.
Ifahamike kuwa mawasiliano na mjadala juu ya zoezi la mchakato wa
uundwaji wa katiba mpya nchini hayakuanza jana ndani ya CCM, bali
yalianza siku nyingi kwa Chama kuunda kamati iliyopitia na kuja na
maoni ya CCM juu ya nini kiwemo kwenye katiba mpya.
Taarifa hiyo haikufanywa Siri. Iliwasilishwa mbele ya vikao kadhaa vya
Chama na kisha kutangazwa kwa umma. Hivyo hoja kwamba mawasiliano ndani
ya Chama juu ya mchakato huo wa Katiba nchini umelenga kuhujumu mchakato
huo hayana maana yoyote, badala yake hoja hiyo imebeba mtazamo finyu wa
wanasiasa wenye tabia za nguruwe za kula watoto wake mwenyewe pindi
apatapo njaa.
Chadema ni kama nguruwe ambaye huweza kuzaa watoto wake kisha akishikwa
njaa huanza kuwala watoto wake mwenyewe. Mchakato wa katiba nchini ni
matunda ya viongozi wa CCM akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa
CCM Taifa, kutangaza kuanza kwa mchakato huu. Hatuwezi kuuzaa wenyewe
mchakato halafu tukauhujumu wenyewe mchakato huo.
Itakumbukwa umezuka utamaduni mbaya kwa baadhi ya Wabunge wa CHADEMA
kutumia Bunge kama jukwaa la kuwashambulia isivyo sawa watu ambao hawana
fursa ya kuingia Bungeni kujibu mashambulizi hayo. Utamaduni huu ni wa
hovyo unakiuka haki za msingi ambazo zinataka mtu
anayetuhumiwa/kushutumiwa apewe fursa ya kusikilizwa. Watanzania lazima
tuukatae utamaduni huu.
Hivi karibuni baadhi ya Wabunge wa CHADEMA wamefanya vitendo vya aibu
vilivyowakera sana Watanzania. Hili bado limo kwenye akili na midomo ya
watu na sasa Chadema wanatafuta namna ya kuficha aibu yao(nitoke vipi)
kwa kurukia hoja ya Mabaraza, kuzusha na kushutumu watu kwa uongo
uliokubuhu.
Vituko vyote hivi vya Chadema vimeongezeka baada ya katibu mkuu wa CCM
hivi karibuni mjini Morogoro kutoa maelezo yaliyoenda shule na hoja
nzito dhidi ya ukibaraka wa Chadema kwenye swala zima la mchakato wa
Katiba.
Nchi nyingi hasa za Afrika zilizokumbwa na machafuko moja ya ajenda
kubwa ilikuwa ni swala la katiba mpya. Sasa hapa nchini Chadema wanaona
watanzania wanaendelea na mchakato bila machafuko wanakosa majibu kwa
mabeberu wanaowafadhili kuchafua nchi yetu, ndio maana kila kukicha
wanakuja na visa na vituko kusumbua mchakato wa katiba.
Walianza kwa kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ikiwemo
kutomtambua rais. Wakatangaza hadharani nchi haitatawalika kisa
wamenyimwa ridhaa na watanzania. Mchakato ulipoanza wa katiba mpya
wabunge wao wakazira na kutoka nje ya bunge, baada ya muda wakarudi.
Juzi bungeni wametishia kujitoa kwenye mchakato wa katiba ifikapo tarehe
30/04/2013, leo ni tarehe 05/05/2013!! Wamezoea kutishia nyau,
tumechoka na vitisho vya vibaraka hawa. Tunapongeza msimamo wa Tume ya
mabadiliko ya Katiba kwa kupuuza hoja ya kufuta mabaraza ya katiba.
Chadema wakisusa na wasuse tu.
Tunawasihi watanzania wote wapuuze utoto na ukibaraka huu wa Chadema
kwani ugonjwa wao tumesha ufahamu WANAUMWA KIFAFA CHA SIASA. Kila
ugonjwa huu ukipanda wanatupa mateke sana. Tuwaombee ipo siku huenda
mwenyezi Mungu atawarehemu watapona.
Post a Comment