“Waziri hana mamlaka ya kumwondoa mkurugenzi wa halmashauri, taasisi,
shirika na katibu wa wizara yake kutokana na kubanwa na mfumo.”
Makamba.
,,,,,,,,,,,,
Mwanza. Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba amesema ipo haja ya kubadili mfumo wa
watendaji serikalini ili wanapoboronga nao wajibishwe na mawaziri.
Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika
mwishoni mwa wiki mjini hapa, Makamba alisema mfumo uliopo sasa, hauwapi
nguvu mawaziri ili kuwawajibisha watendaji pale wanapokosea na badala
yake unawabana wenyewe hivyo kuendelea kuwa kitanzi kwao.
“Mimi ni waziri, akikosea katibu nawajibishwa huyu
anabaki, mimi siwezi kumwajibisha hivyo wanafanya lolote na sisi
tunalazimishwa kuwajibishwa kisiasa kwa makosa ya watendaji,” alisema.
“Baada ya Kamati ya Maliasili Ardhi na Mazingira
iliyo chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli kuomba kwa Spika kutumia
ushahidi kwa kuweka kanda za video ili kuonyesha kilichotokea kwenye
Operesheni Tokomeza Ujangili, hali ilichafuka ndani ya kikao cha Bunge
na kila mmoja akawa na hisia na wengine kuanza kububujikwa na machozi na
wabunge kuchangia hoja za kutaka mawaziri kuachia ngazi, hawakuangalia
kiini cha tatizo, waliwabana mawaziri tu,” alisema.
Alisema Serikali kupitia mamlaka za juu, inapaswa
kuangalia mfumo uliopo kwa lengo la kuubadilisha na kuingiza mapendekezo
na mfumo mpya kwenye Katiba Mpya kuhusu uwajibikaji wa mawaziri na
watendaji wakuu kwenye wizara, taasisi, idara, halmashauri na mashirika
ya umma ambao ni wataalamu mbalimbali kuwajibishwa na mawaziri husika
endapo kutaonekana utendaji wao haukidhi ama kwenda kinyume na maadili
na sheria zilizopo.
NA MWANANCHI
NA MWANANCHI