waziri Mkuu akisalimia ofisi za Tamisemi |
WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka
wakurugenzi wa vitengo na wakuu wa taasisi katika Ofisi ya Waziri Mkuu
(TAMISEMI) wapate nakala ya hansard ya hotuba ya Rais Dkt. John Pombe
Magufuli ya kuzindua Bunge la 11, waisome na kufanyia kazi maeneo yote
aliyoyaainisha.
“Katibu Mkuu hakikisha umepata hansard ya
hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge na uhakikishe kila mkurugenzi
ana nakala na kila mmoja wenu lazima ahakikishe anafanyia maeneo ambayo
Mheshimiwa Rais ameyaainisha. Ni lazima tuelewane ni nini tunapaswa tufanye,”
alisema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Novemba 24,
2015) wakati akizungumza na wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi
ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) kwenye mkutano uliofanyika ofisi ndogo ya TAMISEMI,
barabara ya Kivukoni, jijini Dar es Salaam.
“Ninatamani kuona mabadiliko ya utendaji kazi
Serikalini katika kipindi kifupi. Natamani kila mmoja asiridhike na uzembe
unaofanywa huku chini. Ni nyote ni wataalamu, kwa hiyo mnapaswa kudhirisha
elimu yenu na ujuzi mlionao,” aliwasisitizia Wakurugenzi hao.
Alisema kila mkurugenzi na mkuu wa taasisi
anapaswa kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa kazi kwenye sekta yake kwani hilo
litasaidia kukidhi matarajio ya Watanzania ya kuona mabadiliko ya utendaji kazi
kwenye Serikali ya Awamu ya Tano. “Ninyi wakurugenzi siyo desk officers
bali ni field officers. Nataka muweke utaratibu wa kwenda vijijini
mkasimamie watu wenu, pia mhimize uadilifu, uaminifu na weledi wa kazi,”
alisisitiza.
“Mambo ninayotaka mhimize watendaji waliopo chini
yenu ni pamoja na haya yafuatayo: muda wa kuripoti kazini uzingatiwe, muda wa
kukaa kazini uzingatiwe, utokaji kazini kwenda kwenye chai na chakula cha
mchana udhibitiwe, na mipango na malengo ya kazi kwa siku ni lazima yafikiwe,”
alisema.
“Tunataka kujua mtumishi amefanya nini tangu
alipoingia ofisini. Suala siyo kukaa tu ofisini, kwani kuna mtu anakaa ofisini,
hajaenda hata kunywa chai lakini ukiuliza amefanya nini hupati jibu la
kueleweka. Sisi kama vongozi wao ni lazima tujue wanafanya kazi gani wanapokuwa
maofisini,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa
ameitisha kikao ofisini kwake kesho saa 4 asubuhi akitaka kupatiwa taarifa ni
kwa nini mradi wa mabasi yaendayo kasi (DART) haujaanza kazi hadi sasa. “Kesho
saa 4 asubuhi Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu DART na watendaji wako mje ofisini.
Nataka kupata maelezo ni kwa nini mabasi hayajaanza kazi hadi leo, je ni lini
yataanza kazi, je ni nani anakwamisha. Na hata kama ni sheria, ni kwa nini
tusiziharmonise ili kuondoa hivyo vikwazo,?” alihoji Waziri Mkuu.
“Ninataka kupata haya maelezo kwa sababu
Watanzania na hasa wana-Dar es salaam, wamesubiri kwa muda kuona mradi ukianza
kazi ili uondoe kero ya usafiri. Wao wanajua anayehusika ni TAMISEMI,”
aliongeza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na
watumishi na viongozi wa TAMISEMI, Katibu Mkuu wa OWM-TAMISEMI, Bw. Jumanne
Sagini alimweleza baadhi ya mafanikio na changamoto ambazo wizara hiyo
imekabiliana nazo katika utendaji wake wa kazi.
Kuhusu ujenzi wa vyumba vya maabara kwa ajili ya
kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi, Bw. Sagini alisema vyumba hivyo
vimeongezeka kutoka 247 mwaka 2005/2006 na kufikia 6,161 mwaka 2014/2015. Pia alisema vyumba 4,228 viko kwenye hatua za
kukamilika ujenzi wake.
Kuhusu utengaji wa madirisha ya kuhudumia makundi
yenye msamaha kama wazee na watu wenye ulemavu hospitalini na kwenye vituo vya
afya, Katibu Mkuu alisema nayo yameongezeka kutoka madirisha 5,074 mwaka 2010
na kufikia 7,903 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 55.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, NOVEMBA 24, 2015.
Post a Comment