NINAANDIKA haya kwa sababu nimebaini wasomaji wengi wameshiba taarifa za
uongo na propaganda nyepesi kuhusu kilichotokea hata kusababisha
anayeitwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim
Jecha, kutokwa na akili za kawaida, na kuamua kuchukua hatua ya “peke
yake” inayoendelea kuichumia nchi mgogoro wa kisiasa.
Ni hatua yake ya kufuta uchaguzi mzima wa Zanzibar – Wazanzibari
walimchagua Rais, Wawakilishi na Madiwani wa wadi za Zanzibar Oktoba 25.
Tena niseme wazi ninarudia kudurusu yaliyotokea baada ya kujiridhisha
kuwa nisipofanya hivi, sitakuwa nimetenda haki kwa ukamilifu wake. Kwa
kutotenda hivyo, nawapa ushindi wanasiasa wachache wachovu wanaotaka
kupindisha ukweli kwa maslahi binafsi ya kisiasa.
Nimewahi kuapa kwa jina la mola muumba wa vyote ardhini na angani, ndani
ya uhai wangu, sitavumilia ukweli kupotoshwa, kwa yale ninayoyajua kwa
uhakika wake.
Lakini pia, ninapenda kusema, nimeguswa mno na majadiliano ya Wahariri
katika mjumuiko wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu kilichotokea
hata Jecha akachukua hatua ile ya peke yake.
(Ni “peke yake” kwa sababu mpaka sasa hakuna ushahidi wowote uliotolewa
na yeyote ndani ya Tume kwamba alitumwa na Tume ambayo maana yake ni
yeye mwenyekiti, makamu wake na makamishna kufanya alichokifanya; wala
Tume haikupata kujadili suala lolote tangu wananchi walipomaliza
kupigakura, hata iwe walifikia kuamua kufuta uchaguzi wote nchini.
Kitendo cha Wahariri kujadiliana kupitia gurupu lao mahsusi la WhatsApp,
ni chema. Tatizo ni kuona baadhi yao wanaeneza ninachoona ni upotoshaji
na propaganda ambazo ndizo zinatumiwa na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Zanzibar kujenga kesi dhaifu.
Angalia, Mhariri kwa kutetea ujinga, anahusisha hatua ya Jecha kufuta
uchaguzi uliogharimu karibu Sh. 9 bilioni, na hatua ya Maalim Seif
Shariff Hamad, anayepigania haki yake ya kuongoza Zanzibar, kutangaza
mwelekeo wa kura zake za ushindi.
Huu ni upotoshaji wa kwanza uso maana. Tuseme Maalim Seif amekosea
kufanya alichokifanya Oktoba 26 asubuhi, hilo litakuwa kosa lake binafsi
linalopaswa kuchukuliwa kijinai.
Ni juu ya wachunguzi wa serikali, Jeshi la Polisi, kumshughulikia.
Wangemhoji, wakamrekodi maelezo, wakafungua jalada la tuhuma na
kuliwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wa Zanzibar, ambaye
akiona tuhuma zina msingi na ushahidi, atafungua mashitaka dhidi yake.
Hivi adhabu inayomstahilia (kama ni sahihi) Maalim Seif aliyegombea
urais na “kuchaguliwa” na wananchi kwa mujibu wa matokeo
yaliyokwishatangazwa na wasimamizi wa vituo majimboni, inajuzu vipi
kuangushiwa wapigakura?
Iko wapi hapo haki ya wapigakura wa Zanzibar kama wanaadhibiwa wao
waliopewa haki na Katiba ya Zanzibar ya 1984, kwa kosa lisilowahusu?
Kwani wao ndio waliofanya hicho anacholaumiwa mgombea kufanya?
Walifanyia wapi wananchi waliopigakura? Wanasingiziwa ubaya usiowahusu.
Kwa hakika watu wasio na hatia yoyote zaidi ya kutumia haki yao ya
kikatiba, wanadhalilishwa isivyostahiki.
Maneno niliyoyawekea wino mzito nataka yaeleweke vizuri. Wale wanaojenga
hoja ya kumlaumu Maalim Seif na kumtia makosani eti amejitangaza
mshindi, wajue kwamba kila kituo cha uchaguzi kilichokuwa na wapigakura
wasiozidi 350, kilihesabu kura za urais, pamoja na zile za uwakilishi na
udiwani.
Na wakahesabu za Rais wa Jamhuri na Wabunge.
Msimamizi alijaza fomu za kura hizo, akawasainisha mawakala wote
waliokuwa kituoni, naye akasaini. Akabandika fomu ukutani nje kwa ajili
ya umma kujua. Waangalizi, kama tulivyoshuhudia waandishi wa habari,
nasi tuliangalia kuthibitisha kile tulichoshuhudia wakati kura
zinahesabiwa na kujumlishwa majimboni.
Katika hali kama hiyo, ni nani katangaza matokeo? Ni nani alitangulia
kuyatangaza matokeo ya kura za urais? Asemaye ni Maalim Seif, huyo ana
lake dhidi ya mwanasiasa huyu kipenzi cha umma.
Maalim Seif, mgombea urais, alipata fomu za majimbo yote 54 (majimbo 18
Pemba na 36 Unguja). Asipate vipi wakati sheria ya uchaguzi inaruhusu na
safari hii timu yake ilisimamia kijasusi zipatikane kupitia mawakala
wake vituoni? Akajumlisha kura za majimboni, akaona anatimiza idadi ya
kura za kumshinda Dk. Ali Mohamed Shein. Tunaelewana?
Labda hamjui nyie, viongozi wa CCM wanatafutana uchawi, ni nani
aliruhusu Maalim Seif azipate fomu za majimbo yote? Hamjui baadhi ya
mawakala wa CUF walikimbizwa kiroho mbaya na mazombi (askari wasio
nidhamu wa serikali) wazisalimishe fomu zisimfikie mgombea.
Walichofanikiwa siku zote CCM, kimewashinda safari hii; wanalizana mjue!
Mhariri mzima anashauri kwa njia ya swali, “Maalim Seif akamatwe?” Nani amezuia hili kutendwa?
Kwanini asikamatwe kama amekosa; hata mara moja hajajiweka juu ya
sheria. Anakamatika na kushitakika. Mbona ameshashitakiwa sana.
Maalim Seif amekaa gerezani pasina kuhukumiwa na mahkama. Huyu ni
mpigania haki za Wazanzibari na nchi yao, hahofii mahkama wala gereza.
Amepata kuyasema haya hadharani. Hajabadili kauli.
Juma Duni Haji, mwanasiasa mahiri kwa lugha ya kujengesha hisia
wananchi, na kuzidodosa takwimu na tawala dhalimu Tanzania, ameshasema
haya mara kadhaa. Nimeyasikia kwenye kampeni za uchaguzi uliofanyia
mwezi uliopita.
Hawa wawili wamesema sana hawaogopi yote mawili – mahkama na gereza.
Duni alikaa gerezani miaka mitatu mfululizo wakati huo alishatuhumiwa
kuua askari mjini Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, katika siku ambayo kwa
hakika alikuwa mjini Unguja.
Maalim Seif alishakaa gerezani sana tu. Alisingiziwa kumshika askari
shababi (kijana barubaru) na kumnyang’anya bunduki akiwa na wafuasi wake
kadhaa eneo la Jang’ombe. Wenyewe wanasema wameshauawa bado kuzikwa.
Juwa usiyejua kwamba Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya Zanzibar ya 1984,
Kifungu 88, inamtaka msimamizi wa uchaguzi jimboni “(a) haraka
atamtangaza mgombea aliyepata wingi wa kura halali zilizopigwa kuwa
amechaguliwa; na (b) atapeleka taarifa ya maandishi kwa mgombea
aliyeshinda; na (c) atatoa taarifa ya matokeo kwa Tume, nayo itayapeleka
matokeo, pamoja na idadi ya kura alizopata kila mgombea katika jimbo
kutangazwa katika Gazeti Rasmi.”
Ni hawa wasimamizi walikuwa na matokeo ya kura za urais wakawasilisha
Tume wakiwa wameshabandika fomu kwenye kuta za vituo majimboni. Walikuwa
wameshathibitisha matokeo ya uchaguzi kwenye maeneo yao.
Hatua hiyo imefanywa pasina malalamiko ya mgombea yeyote akiwemo wa CCM.
Ila wakubwa watatu wa CCM walifika Tume Oktoba 27, na barua ya
malalamiko. Walisikilizwa, waangalizi wakiwepo, lakini wakatoka kapa,
hakuna walichokipata.
Hapo, wakaandaa hila – eti makamishna walipigana ngumi, kura zilizidi
wapigaji, nyingine ziliokotwa mitaani, eti Maalim Seif alitoka Afrika
Kusini na kura bandia.
Kote hawana hoja ya kisheria. Kote wamejidhalilisha na kuumbuka. Hata
mpango wao wa kuchakachua matokeo kisiwani Pemba ulishindwa baada ya
kukosa wakala wa kuwasaidia kutengeneza matokeo ya kumpiku Maalim Seif.
Kilichobaki baada ya njia hizo kushindwa, ni kimoja tu – yale ya
kutokabidhi serikali kwa vikaratasi. Walisema na kurudia, si kada mmoja
wala wawili, wengi wao. Wakamtweza nguvu Jecha akafanya ujecha wake, leo
amebakia peke yake ndani kwake, nje hakutokeki, kuchungu. Wao wasema
wamsubiri atangaze siku ya uchaguzi mpya. Haweshi ubabe, na ndiyo
demokrasia yao. Hawa kwa siasa chafu hawawezekani.
Chanzo: MwanaHalisi
Post a Comment