....................................
Janatarehe 26/06/2012, ni siku ya maadhimisho ya mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya duniani. Tamko la kimataifa kuhusiana na matumizi ya dawa za kulevya ni kwamba bado dawa za kulevya zinaendelea kuathiri afya za binadamu na ndio maana juhudi za mapambano hayo zikaendelezwa.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari huko ofisini kwake Migombani Mjini Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Fereji amesema vita dhidi ya dawa za kulevya ni ngumu sana, lakini inawezekana iwapo jamii itashirikiana dhidi ya mapambano hayo.
“Hii ni kutokana na ukweli kuwa wanaojishughulisha na biashara hii ni watu wenye fedha nyingi na ujanja kupita kiasi, inafika wakati watu hawa wanashusha mzigo baharini na kwenda kuuzamia kwa wakati wao na kuupeleka wanakokujua wao. Na kama wakiamua kuhonga hawahongi laki moja au mbili, hesabu hiyo inakuwa kwa dola, sasa fikiria”, aliweka wazi Mhe. Fatma Fereji.
Hata hivyo amesema serikali inajitahidi kuongeza nguvu za kupambana na uingizaji na matumizi ya dawa hizo, sambamba na kusaidia kupata hifadhi na mafunzo ya amali kwa vijana walioamua kuachana na dawa hizo.
Amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali hadi sasa ni pamoja na kutenga shilingi milioni mia moja kwa ajili ya matayarisho ya ujenzi wa nyumba za kuwaendeleza vijana walioamua kuachana ya dawa za kulevya (sober houses) huko Tunguu ambazo zikimalizika zitatoa huduma zote bure kwa vijana hao. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “Tujenge jamii yenye afya bila ya dawa za kulevya”.
Post a Comment