Na Veronica Kazimoto- MAELEZO
Dar es Salaam
20/09/2012.
Uchaguzi mdogo wa Madiwani katika kata ishirini na tisa na halimashauri ishirini na saba Tanzania bara utafanyika tarehe 28 Oktoba, mwaka huu.
Uchaguzi mdogo wa Madiwani katika kata ishirini na tisa na halimashauri ishirini na saba Tanzania bara utafanyika tarehe 28 Oktoba, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na viongozi wa
siasa ngazi ya Taifa leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi
Julius Mallaba amesema maandalizi ya uchaguzi huo yameanza rasmi ili
kuhakikisha kwamba kila raia mwenye sifa anapata fursa ya kushiriki na
kuchagua kiongozi anayemtaka.
Amezitaja Kata na Harimashauri hizo kuwa ni pamoja na Bangata
(Halmashauri ya Wilaya ya Arusha), Darajambili (Halmashauri ya Manispaa
ya Arusha), Msalato (Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma), Mpwapwa
(Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa), Magomeni (Halmashauri ya Wilaya ya
Bagamoyo), Lwezera (Halmashauri ya Wilaya ya Geita) na Bugarama
(Halmashauri ya Wilaya ya Kahama).
Nyingine ni Mwawaza ambayo iko Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga,
Vugiri (Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe), Tamota (Halmashauri ya Wilaya
ya Lushoto), Makata (Halmashauri ya Wilaya ya Liwale), Mnero Miembeni
(Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea), Mlangali (Halmashauri ya Wilaya
ya Ludewa), Luwumbu (Halmashauri ya Wilaya ya Makete), na Mpepai
(Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga).
Zimetajwa pia Kata za Mletele (Halmashauri ya Wilaya ya Songea), Ipole
na Kiloleli (Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge), Miyenze (Halmashauri ya
Wilaya ya Tabora), Karitu (Halmashauri ya Wilaya ya Nzega), Mpapa na
Myovizi (Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi), Lubili (Halmashauri ya Wilaya
ya Misungwi), Kilema Kusini (Halmashauri ya Wilaya ya Moshi), Nanjara/
Reha (Halmashauri ya Wilaya ya Rombo), Mtibwa (Halmashauri ya Wilaya ya
Mvomero), Mahenge (Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga), Likokona
(Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu) na Kitangari (Halmashauri ya Wilaya
ya Newala).
Katika mkutano huo Mallaba ametangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa
madiwani kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 2 oktoba, 2012,
kampeni za uchaguzi zitaanza oktoba 3 hadi oktoba 27, 2012 na fomu za
uteuzi kwa wagombea na wasimamizi wa uchaguzi zimeanza kutolewa.
Aidha Mallaba amefafanua kuwa tayari tume imeshateua watendaji
watakaosimamia chaguzi hizo na inaendelea na maandalizi mengine ambayo
ni pamoja na mafunzo kwa watendaji, uchapishaji na ununuzi wa vifaa vya
uchaguzi, uchapishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, utoaji wa
elimu ya mpiga kura na uudaji wa kamati za maadili.
Amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itahakikisha kwamba chaguzi hizi
zinafanyika kwa uwazi, uhuru na haki kwa kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu zilizowekwa ili kujenga demokrasia na kuimarisha utawala bora.
Julius Mallaba ameviomba vyama vyote vya siasa vitavyoshiriki katika
uchaguzi huo kuzingatia sheria na maadili ili kuepusha malumbano
yanayoweza kujitokeza.
Post a Comment