Moja ya
mambo yaliyoibadilisha historia ya siasa chafu hapa visiwani Zanzibar
tangu 1964, ni ile hatua ya mkuu wetu Mheshimiwa Amani Karume (Mungu
amsamehe dhambi zake na ampokelee toba zake) kuruhusu Serikali ya umoja
wa kitaifa. Serikali ambayo kwa mara ya kwanza imeruhusu vyama vikuu
viwili vya siasa, CCM na CUF kukaa pamoja, katika kuendesha hatamu ya
nchi.
Hakuna kiumbe katika sisi wanakaumu ya wazanzibari alietegemea kama
hili lingewezakena na kama kuna mtu angetabiri hili kutokea hapo awali,
angeliwa ‘nyam nyam’ na wananchi kwa kusema uongo uliokithiri katika
bahari za uongo. Mtu huyo angeliwa kwa sababu historia ya Zanzibar chini
ya vyama vingi haikuwa njema tena na ilishajenga mazoea na utamaduni wa
chuki na uhasama kama mbolea kuu za kujiiimarisha kisiasa hapa nchini.
Kutokana na kuwepo kwa chuki hizo na uhasama uliokwisha ota mizizi,
suali la CCM na CUF kukaa pamoja lilibaki kama ndoto ya ‘alinacha’.
Kuna mantiki ya kutoamini uwezekano wa kuwepo umoja wa kitaifa ambao
kimsingi ndio suluhisho la siasa za chuki na uhasama hapa visiwani.
Ukivuta kumbukumbu za uonevu wa CCM kwa wanachi hasa hasa wa CUF,
dhuluma katika kura na uchaguzi, maafa na vifo, mateso na manyanyaso
waliyofanyiwa CUF kwa kipindi kifupi tu cha kutoka 1992 hadi 2010 tu,
achilia mbali haya ya Mbwa mwitu hivi sasa, yalitosha kabisa kutoa picha
ya ugumu uliokuwepo wa kuungana na kuwa kitu kimoja. Na ndio maana hata
mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba alisema wakati CUF inajiunga na GNU
kwamba ‘tumesamehe lakini hatutosahau’.
Mheshimiwa Amani Karume, amefuata wasia wa Bwana Mtume (SAW) pale
aliposema ‘mcheni mwenyezi mungu popote mlipo. Na mfuatishe jema kwa
baya ili lifutwe, na mkae na watu kwa tabia njema’. Mheshimiwa Karume
alifanya mabaya mengi tunayoyajua na tusiyoyajua kama waja wengine
tunavyofanya. Hakuna aliemsafi. Lakini Mheshimiwa alifanya jambo kubwa
jema lililofuta mabaya yake mengi kama si yote kwa Wazanzibari. Kuruhusu
kwa nguvu yote kuundwa kwa serikali ya umoja wa Kitaifa Zanzibar. Na
kama hakutaka yeye hili lisingekuwepo kamwe. Hali hii imeifanya CUF
iwemo Serikalini leo pamoja na kuwa mfumo wenyewe wa GNU unapigwa vita
sana na washirika wenza CCM waliopo madarakani hivi sasa. Haya tunayaita
mafanikio kwa sasa.
Lakini pamoja na kuwemo serikalini , chama cha CUF kimo katika
mtihani mkubwa kwani muundo halisi wa GNU ulivyo tangu awali ni kikwazo
kikubwa kwa CUF kuweza kuathiri na kutekeleza maamuzi muhimu ya
Serikali. Kikwazo kikubwa ninachokiona kwa sasa ni mgawanyo wa nafasi
katika GNU tuliyokubaliana. Naamini CUF hawakufikiria vya kutosha au
walitegemea kutumia ile nadharia ya ngamia na bwana wake waliponyeshewa
na mvua. CUF ilitegemea kuingia kichwa Serikalini na baadae iingize
shingo na mwili nzima. Sijui kama itawezekana. Au ilitegemea iwemo tu na
wenza wao watabadilika na kuwa na sura za utu. Na hili gumu pia!
Nionavyo, muundo wa GNU hauisaidii sana CUF. Kwa sababu, CUF haina nafasi kubwa ya maamuzi na kiutawala, ipo zaidi kiheshima (ceremonial). Katika muundo wa GNU ya sasa Rais ana nguvu kubwa na anamiliki Serikali. Makamo wa Pili wa Rais ambae pia ni CCM anamiliki Bunge yaani baraza la wawakilishi na ndie mtendaji mkuu wa Serikali. Hapo jiulize makamo wa kwanza wa Rais ana kazi gani? Tutake tusitake hapa pana mapungufu makubwa na ndio hata kwa aliekuwepo pale kibanda maiti kumsikiliza maalim Seif akimwaga radhi au akifyatuka (kwa maana alipita kipimo cha maadili kusema kuhusu Serikali yake na wakubwa zake na viongozi wenzake hadharani), ni moja ya dalili ya ‘makununu’ ya GNU yanavyomkwaza kwa sasa humo Serikalini.
Maalim Seif hana kauli kiivyo ndani ya GNU inavyoonekana. Ndio ukaona
anasema, nilimshauri Rais wangu Dr. Shein, nikazungumza na Mohd Aboud,
Mwinyi haji Makame, lakini hakuna kilichokuwa. Ni kama alichochea moto
machafuko zaidi. Hii ina maana kuwa hakuna aliemsikiliza jambo ambalo
ni kufeli kukubwa kwa mfumo wa GNU iwapo hali iko hivi.
Maalim anasema nia na mpango wa kuanzishwa kwa vurugu hapa visiwani
ulikuwepo mapema na ulipata Baraka iliyofanyika katika kikao huko
Dodoma. Kikao hicho alikuwemo Rais Shein na Balozi Idd ambao waliitwa
huko kikatiba kulingana na vyeo vyao. Maalim analaumu hakuitwa na sababu
aliyopewa ni kuwa hatambuliwi kikatiba jambo ambalo naliafiki kwa sasa.
Maalim Seif ni Makamo wa Rais wa Heshima (Ceremonial) au kama msimamizi
wa mambo ya CUF katika GNU (a watchdog) na si vyenginevyo. Haya yote ni
kweli kikatiba na maalim na CUF walipaswa kuyatambuwa haya mapema mno.
Chukulia ingekuwa CUF ilikubali GNU yenye muundo tafauti kidogo,
yaani ule wa mgawanyo wa madaraka kamili, kwa mfano; CCM ikitoa Rais,
basi Mtendaji mkuu wa Serikali atoke CUF. Nionavyo, haitoshi tu kuwa na
makamo wawili wa Rais, kwa kile tunachokidai kuwa nasi ‘tumo’ ‘tumo’ na
‘hatutoki ng’o’. Hii haisaidii sana, kwani kuwemo tu hakuna maana ya
kuwa mtaleta ufanisi au mabadiliko. Kule Bungeni Dodomo Wabunge wetu
wamo, na wamo tu, yamekuwa yakiongezwa mambo ya Muungano kiholela mpaka
kurasa zimejaa, wao wamo, wamo tu! Kuna lipi walilofanya. Wansema sana
kama CUF wanavyosaula,na kumwaga radhi hadharani hivi sasa, lakini
hawana nguvu kikatiba na kisheria ni bure tu! Kidomo bobo!
GNU haikuonesha hata pahala pamoja mgawanyo wa madaraka baada ya
nafasi za Uwaziri. Kuanzia makatibu na manaibu katibu wakuu,
wakurugenzi, maafisa wadhamini, wakuu wa wilaya na mikoa, na hata wale
mafatani wakubwa masheha, nafasi hizi hazikujadiliwa na GNU. CUF
ilitosheka na Uwaziri na Umakamo kivuli tu. CCM wamebaki na nafasi zao
zote ukitoa vijiwizara viwili vitatu tulivyokubaliana. Sasa leo ukiona
unashauriana na wenzako Serikalini husikilizwi na huna nguvu humo ujue
huna kitu au hutakiwi. Na nani alaumiwe kwa hilo?
Nakichukulia kitendo cha Maalim Seif kumwaga radhi hadharani pale kibanda maiti kama ni silaha yake ya mwisho ya kujitetea kwani si katika maadili halisi ya Uongozi kwa viongozi wakuu wa Serikali kusasambuana hadharani kama vile hata kama ni wapinzani. Tuwaone Nick Clegg na Cameron. Hawakubaliana kwa mengi lakini huzungumza wakafikia pahala bila ya kuita mikutano ya hadhara ya kumwagiana radhi. Hutuba ya maalim Seif inaonesha wazi jinsi wenzake walivyokuwa hawamfanyi kuwa na nafasi katika Serikali licha ya kudai kuwa wanamuheshimu. Lakini yote haya ni makosa ya tangu asili ya muundo wa GNU ambayo CUF kwa njia moja au nyengine haikuyaona au ilitarajia makubwa bila kuyatathimini mapema kwa kina.
Hivyo basi, ili kuleta utulivu na haki ndani ya muundo wa sasa wa GNU
ambao mimi ni muumini mkubwa, basi ipo haja ya kufanya makubaliana
mengine ya mgawanyo wa madaraka kwa vyama vyote kwa usawa au kwa
asilimia Fulani itakayokubalika itumike katika ngazi zote za utawala na
uendeshaji. GNU pia iangalie upya nafasi ya mshirika mwenza wa chama
kilichoshindwa Urais kuwa na mamlaka kamili ya kiundeshaji kama ilivyo
sasa kwa makamo wa pili wa Rais. Kinyume na hivi, CUF imekanyaga msuro!
Wabillahi Taufiq
Wabillahi Taufiq
Chanzo:www.mzalendo.net
Post a Comment