Release No. 184
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 20, 2012
NYAMLANI
ATEULIWA KAMATI YA AFCON 2013
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman
Nyamlani ameteuliwa kuwemo kwenye ujumbe rasmi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) utakaosimamia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON)
zitakazofanyika Januari mwakani nchini Afrika Kusini.
Uteuzi
huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou na Kamati yake ya Utendaji. Ujumbe huo
wa CAF kwa ajili ya fainali hizo zitakazoanza Januari 19 na kumalizika Februari
10 mwaka huu una jumla ya watu 148.
Nyamlani
ni mmoja wa wajumbe watatu watakaoshughulikia masuala ya rufani. Wajumbe
wengine ni Prosper Abega kutoka Cameroon na Pierre-Alain Monguengui wa Gabon.
Nyamlani ni mjumbe wa Bodi ya Rufani ya CAF yenye watu 12.
MECHI YA
SERENGETI BOYS YAINGIZA MIL 23/-
Mechi
ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya
Tanzania (Serengeti Boys) na Congo Brazzaville iliyochezwa juzi (Novemba 18
mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 23,021,000.
Mapato
hayo yametokana na washabiki 18,022 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo
kwa viingilio vya sh. 10,000, sh. 5,000, sh. 2,000 na sh. 1,000. Washabiki 15,850
walikata tiketi za sh. 1,000.
Asilimia
18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 3,511,677.97 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa tiketi (sh. 5,956,635),
usafi na ulinzi (sh. 2,350,000), maandalizi ya uwanja- pitch preparation (sh.
400,000), Wachina- Beijing Construction (sh. 2,000,000), umeme (sh. 300,000) na
ulinzi wa mechi (sh. 3,500,000).
Kwa
upande wa mgawo asilimia 20 ya gharama za mechi ni sh. 1,000,537, asilimia 10
ya uwanja sh. 500,269, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)
sh. 250,134, asilimia 45 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
2,251,209, asilimia 20 ya TFF (sh. 1,000,537) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 50,027.
UCHAGUZI WA
CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU MKOA WA KATAVI (KAREFA)
Mchakato
wa uchaguzi wa KAREFA umefutwa kutokana na wagombea watano kati ya nane vyeti
vyao vya elimu ya sekondari kuwa na utata. Mchakato wa uchaguzi huo utaanza
upya Novemba 21 mwaka huu.
UCHAGUZI WA
TASMA
Mchakato
wa uchaguzi wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) utaanza
upya Novemba 26 mwaka huu baada ya mchakto wa sasa kupata wagombea kwenye
nafasi mbili tu za Kamati ya Utendaji ya chama hicho.
UCHAGUZI WA
CHAMA CHA MPIRA WA MIGUU MKOA WA RUKWA (RUREFA)
Mchakato
wa uchaguzi wa RUREFA utaanza Novemba 26 mwaka huu na Kamati ya Uchaguzi ya
RUREFA itapewa maelekezo ya usimamiaji wa uchaguzi huo baada ya mchakato wa
awali kuwa umefutwa kutokana na kufanyika bila kuzingatia kanuni za uchaguzi.
MKUTANO NA
WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari
utakaofanyika keshokutwa (Novemba 22 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 6
kamili mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Post a Comment