WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki ametangaza
kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA) waliokwamisha mradi wa kuwasaidia wafugaji wa hifadhi
hiyo ulioahidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2008.
kizungumza na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro na viongozi wa NCAA mara
baada ya kuelezwa kuhusu kukwama kwa mradi huo, Balozi Kagasheki alisema
lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya viongozi hao.
“Haiwezekani mradi ulioahidiwa mwaka 2008 leo hii ukwame, waliohusika
kuukwamisha ni lazima wakae pembeni. Ninakwenda Dar es Salaam ila wakae
wakijua kuwa barua zao zinakuja” alisema Kagasheki na kuongeza;
“Kabla sijaondolewa wizarani kutokana na matatizo kama haya, mtaondoka
ninyi kwanza.…, kukwama kwa mradi huu kutawafanya wananchi wamchukie
Rais Kikwete na wanasiasa,” alisema Balozi Kagasheki.
Awali, Kaimu Mhifadhi wa Ngorongoro, Bruno Kawasange alisema mradi huo,
ambao ulifikia hatua nzuri, umesitishwa na PPRA kwa maelezo kuwa
taratibu hazikufuatwa katika kumtafuta mtaalamu mwelekezi.
Kawasange alisema awali, mtaalamu mwelekezi wa mradi huo, alipatikana
nchini Ufaransa na tayari taratibu kadhaa zilianza ikiwa ni pamoja na
kutolewa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji wa kisasa.
Hata hivyo, alisema katika hatua za mwisho, PPRA iliwataka kuanza upya
taratibu za kumpata mtaalamu huyo, kwa maelezo kwamba taratibu za
kisheria hazikufuatwa.
Akizungumza katika mkutano huo, aliyekuwa mmoja wa wasimamizi wa mradi
huo, Justice Muumba alisema licha ya kutakiwa kuanza upya kwa taratibu
za kumpata mtaalamu mwelekezi, mambo mengi ya msingi yalikuwa
yamefikiwa.
Katika mradi huo, NCAA kwa kushirikiana na Baraza la Wafugaji, walikuwa
waanzishe mradi mkubwa wa ufugaji wa kisasa na kiwanda cha kusindika
nyama na maziwa ambacho kingesaidia kumaliza matatizo ya wakazi wa
Ngorongoro hasa ya njaa.
Apokewa kwa mabango
Katika ziara yake hiyo, Waziri Kagasheki alipokewa kwa mabango na wakazi
wa Tarafa ya Ngorongoro, yaliyokuwa yakieleza jinsi wanavyoshindwa
kufanya shughuli za kilimo kutokana na kubanwa na NCAA.
Waziri Kagasheki, ambaye alikuwa ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, Mbunge wa
Ngorongoro, Saning’o ole Telele na maofisa kadhaa wa Serikali, alikutana
na mabango hayo alipofika katika Kijiji cha Mokilali Kata ya
Ngorongoro.
Baadhi ya mabango hayo yalisomeka: “Njaa inatuuwa Ngorongoro,”
“Tunalaani kauli ya Mkuu wa Mkoa Arusha kuwa Ngorongoro hakuna njaa,”
“Tumechoka kuwa watumwa, tunataka uwiano Ngorongoro.”
Katika mkutano huo, wananchi karibu wote, waliopewa nafasi ya kuzungumza
walieleza tatizo kubwa la njaa ambalo linawakabili wakisema
linasababisha watoto kufariki, kuugua magonjwa ya utapiamlo, wanaume
kutelekeza familia zao na vijana kukimbilia mijini kufanya kazi za
ulinzi.
Diwani wa Kata ya Enduleni, James Moringe alisema karibu kila kaya
katika tarafa hiyo, sasa inakabiliwa na njaa kali na wananchi hawana
chakula kutokana na kuzuiwa kwa shughuli za kilimo cha bustani bila
kuwapo kwa utaratibu mwingine wa kuwapatia chakula.
“Kwanza tunakanusha taarifa ya Mkuu wa Mkoa wetu, Magesa Mulongo kuwa
Ngorongoro hakuna njaa, sisi tunamshangaa sana mkuu wa mkoa na tunalaani
kauli yake,” alisema Moringe.
Chanzo: Mwanachi
Post a Comment