Kwa ufupi
Lissu ambaye ni kada wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema jana kwamba atakuwapo
mahakamani leo na wakili mwenzake, Method Kimomogolo wakishirikiana
kumtetea mteja wao.
,,,,,,,,,,,,,,
,,,,,,,,,,,,,,
Pamoja na mambo mengine, rufani hiyo
itakayosikilizwa Dar es Salaam, itawakutanisha wanasheria wawili ndugu;
Tundu Lissu na Alute Mghway wa upande wa mashtaka na utetezi.
Lissu ambaye ni kada wa Chadema na Mnadhimu Mkuu
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema jana kwamba atakuwapo
mahakamani leo na wakili mwenzake, Method Kimomogolo wakishirikiana
kumtetea mteja wao.
Wakati Lissu akimtetea Lema, Mghway ni wakili
anayewatetea warufani wa (wajiburufaa) ambao ni makada wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.
Makada hao walimfungulia Lema kesi katika Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha, wakipinga matokeo yaliyompa ushindi katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Hukumu ya kesi hiyo ndiyo iliyomvua ubunge
Aprili 5, 2012 mwaka huu.
Baadaye Lema alikata rufaa kupinga hukumu
iliyomvua ubunge, lakini ilitupiliwa mbali baada ya Mahakama kuridhika
kuwa kulikuwa na dosari za kisheria, kutokana na pingamizi lililowekwa
na warufaniwa.
Hata hivyo, tofauti na hoja za wakili wa
warufaniwa, Mghway kuwa kutokana na dosari hiyo, mrufani hana nafasi ya
kufanya marekebisho, mahakama ilimpa Lema nafasi nyingine ya kufungua
upya rufaa hiyo baada ya kusema dosari hizo zinarekebishika.
Mahakama hiyo ilimpa Lema siku 14 kufanya marekebisho na kufungua tena rufaa hiyo, kazi ambayo aliitekeleza.
Awali, rufaa hiyo ilikuwa ikisikilizwa na jopo
lililoongozwa na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman akisaidiana na Jaji
Salum Massati na Jaji Nathalia Kimaro, lakini sasa Jaji Mkuu, Othman
hayuko katika jopo hilo na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Luanda.
Katika rufaa yake ya awali, Lema alitoa hoja 18 za
kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha iliyomvua ubunge,
lakini tarehe ambayo rufaa hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa, wakili
wa wajiburufaa, Mughwai aliweka pingamizi la awali.
Wajiburufaa katika pingamizi lao walitoa hoja tatu
za pingamizi wakidai kuwa kuna mkanganyiko katika vifungu vya sheria
kati ya vile vilivyotumika kwenye hukumu na vile vilivyokuwapo kwenye
muhtasari wa hukumu.
Hoja nyingine walidai kuwa muhtasari wa hukumu
haukuwa na mhuri wa Jaji aliyeitoa wala tarehe na hoja ya tatu ilikuwa
ni utaratibu wa kuandika muhtasari huo, kwa kutokuandika maneno;
“Imetolewa kwa mkono wangu na mhuri wa Mahakama.”
Kutokana na hoja hizo, Wakili Mghwai aliiomba Mahakama hiyo
iitupilie mbali rufaa hiyo, akidai kuwa kwa dosari hizo, mrufani hana
nafasi tena ya kuzifanyia marekebisho.
Upande wa wajibu pingamizi, Wakili wa Lema,
Kimomogoro na Wakili wa Serikali, Timoth Vitalis kwa niaba ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali walidai kuwa kasoro zote zilizotajwa hazina
athari na zinaweza kurekebishika.
Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali hoja mbili
za rufaa kuwa hazina msingi na ikakubaliana na hoja moja ya pingamizi
kwamba kulikuwa na tofauti au kuchanganywa kwa vifungu hivyo vya sheria.
Katika uamuzi wake wa Novemba 8, 2012, Mahakama
ilisema kuwa kisheria, hati ya muhtasari wa hukumu ni lazima ikubaliane
na hukumu lakini katika shauri hilo muhtasari wa hukumu ulikuwa
haukubaliani na hukumu.
“Hukumu inarejea Kifungu cha 114 (1)-(7), (Sheria ya Uchaguzi), lakini hati ya decree inarejea Kifungu cha 113 (1)- (7),” ilisema Mahakama hiyo na kuongeza:
“Decree lazima ikidhi masharti ya Amri ya XX,
Kanuni ya 6 na 7, za Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Sura ya 33. Katika
shauri hili na kukiuka amri ya XX Kanuni ya 6 na 7, dosari hiyo
inaifanya hati hii isiwe halali.
Hata hivyo, mahakama ilisema kuwa inakubaliana na
mawakili wa wajibu pingamizi hilo kuwa kosa hilo linawezekana limetokana
na kuteleza kwa kalamu au kutokana na kosa la uchapaji.
“Kwa sababu hii linaweza kurekebishwa chini ya
Kanuni ya 111ya Kanuni za Mahakama,” ilisema Mahakama na kumpa Lema
siku 14 kufanya marekebisho ya dosari hizo na kufungua tena rufaa hiyo
Chanzo:Mwananchi
Post a Comment