| Mbunge wa Arusha Mjini Godbles Lema |
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Dodoma kimeandaa
mapokezi makubwa ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbles Lema,
kesho akiwa anarejea mjini humu kuhudhuria vikao vya Bunge kwa mara ya
kwanza baada ya kushinda rufaa yake ya kupinga kuvuliwa ubunge.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Chadema Mkoa wa Dodoma, Stephen
Massawe, iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, Lema anatarajiwa
kupokewa katika eneo la Ihumwa, nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma.
Massawe alisema baada ya mapokezi hayo, Lema atakwenda moja kwa moja hadi viwanja vya Shule ya Sekondari ya Central mjini hapa.
Massawe alisema mapokezi hayo yameandaliwa kwa lengo la kumpongeza Lema kwa kushinda rufani yake.
Pia yanalenga kumpongeza Lema kwa kazi alizofanya za kuimarisha chama
katika kipindi ambacho ubunge wake ulitenguliwa na Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Arusha.
Alisema ukomavu wa kisiasa wa Lema na ushirikiano na wenzake, vimeleta
chachu kubwa kwa ujenzi wa Chadema na kukifanya chama hicho kusonga
mbele zaidi.
Massawe alisema baada ya mapokezi hayo, Lema atawahutubia wakazi wa
Manispaa ya Dodoma katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika
viwanja wa Shule ya Sekondari ya Central. Alisema Lema atafuatana na
wabunge kadhaa pamoja na viongozi wa kitaifa wa chama hicho, ambao nao
watapata nafasi ya kutoa salamu kwa wananchi.
“Lema tumemwandalia mapokezi ya kifalme katika mkoa wetu. Tumetambua kwa
muda wa miezi tisa aliyokaa nje ya Bunge, amefanya kazi kubwa ya
kujenga chama. Lema ameonyesha ujasiri mkubwa katika kutenda kazi yake
kipindi akiwa bungeni na pale alipokuwa nje ya Bunge,” ilieleza sehemu
ya taarifa hiyo na kuongeza:
“Cha kumshukuru Mungu zaidi ni kurudi kwake bungeni. Ataendelea kuibua
madudu, ambayo yanafanywa na serikali inayoongozwa na Chama Cha
Mapinduzi.”
Lema alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 5, mwaka
jana, baada ya mahakama hiyo kukubaliana na hoja mbili za ushahidi
uliotolewa na wadai.
Kati ya madai manne yaliyowasilishwa mahakamani hapo, Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila, aliyekuwa
akisikiliza shauri hilo baada ya kujitoa kwa Jaji Aloyce Mujulizi,
Februari 6, mwaka jana, alikubaliana na madai mawili hivyo kutengua
ubunge wa Lema.
Jaji Rwakibarila alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa
kwamba, Lema katika mikutano yake ya kampeni za uchaguzi iliyofanyika
kuanzia 20 Agosti hadi Oktoba 30, 2010 alitumia lugha za kashfa dhidi ya
aliyekuwa mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, Dk. Batilda
Buriani.
Alinukuu baadhi ya maneno aliyotamka Lema kwenye mikutano hiyo na
kutolewa ushahidi na wadai ni kama, “Dk. Batilda siyo mwaminifu, amezaa
na Mzee wa Monduli na alipo hapo ana mimba nyingine ya Lowassa
(Edward),” kuwa ni baadhi ya matamshi ya kashfa, ambayo hayakubaliki
kwenye kampeni za uchaguzi.
Pia alisema mahakama imeridhika na ushahidi kuwa Lema katika mikutano
yake ya kampeni alitumia hoja ya ubaguzi wa kijinsia dhidi ya Dk.
Batilda kwa lengo la kushinda.
Alisema ushahidi uliotolewa umethibitisha Lema alitamka kwenye mikutano
yake kwamba, “Tangu lini mwanamke akawa kiongozi wa malaigwanan,"
akisisitiza kuwa hayo ni maneno ya ubaguzi wa kijinsia.
Jaji Rwakibarila alisema madai na ushahidi uliotolewa umeiridhisha
mahakama hiyo kuwa Lema alikiuka kifungu 108 cha Sheria ya
Uchaguzi,1985, kinachozuia kufanya kampeni kwa misingi ya ubaguzi wa
kikabila, kijinsia, kidini au rangi.
Kwa msingi wa ushahidi uliotolewa hapa, mahakama imeridhika kwamba Lema
alikiuka Sheria ya Uchaguzi katika kampeni zake na kwa hivyo, matokeo ya
uchaguzi wa ubunge wake yanatenguliwa kama ilivyoombwa na wadai. Kesi
hiyo namba 13/2010 ilifunguliwa na wapigakura watatu wa CCM; Musa
Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel, kupitia kwa wakili wao, Alute
Mughwai, akisaidiana na Modest Akida.
Waliiomba mahakama kutengua matokeo ya ubunge wa Lema kwa kukiuka
kanuni, taratibu na sheria za uchaguzi. Walidai wakati wa kampeni Lema
alimdhalilisha kijinsia Dk. Batilda kwa kutoa lugha za matusi kuwa yeye
ni Mzanzibari na siyo mwaminifu katika ndoa yake.
Makada hao wa CCM walidai Lema alifanya udhalilishaji huo katika vituo
22 vilivyokuwa vinatumika kufanya kampeni za uchaguzi, ambako alitoa
lugha za kashfa na ubaguzi wa kidini na kijinsia na kwamba lugha hizo
ziliathiri matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali malalamiko mawili ya wadai kwamba, Lema alitumia hoja za udini na ukazi.
Jaji Rwakibarila alisema mashahidi waliopelekwa mahakamani hapo wameshindwa kuthibitisha madai hayo.
Alisema suala la Dk. Batilda kukaa Zanzibar na kugombea ubunge Arusha Mjini hilo peke siyo haramu.
Kuhusu madai ya udini, Jaji Rwakibarila alisema mahakama haijaridhika na
ushahidi uliotolewa kwa sababu mashahidi hawajathibitisha kwamba
wanaovaa vilemba kichwani ni al Qaeda.
Alisema kuvaa kilemba kichwani ni heshima na hivyo, wapo wanawake wengi
wanaovaa vilemba. Lema, ambaye alikuwa mlalamikiwa wa kwanza alikuwa
akitetewa na Wakili Method Kimomogoro, wakati aliyekuwa mlalamikiwa wa
pili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) alikuwa akitetewa na mawakili
waandamizi wa serikali; Timon Vitalis na Juma Masanja.
Hata hivyo, Desemba 21, mwaka jana, Mahakama ya Rufani ilimrejesha
bungeni Lema ikiwa ni takribani miezi tisa tangu alipovuliwa wadhifa huo
na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Mahakama hiyo ilimrejesha Lema bungeni, baada ya kushinda rufaa yake ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Hukumu hiyo iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth
Mkwizu, ilimtambua Lema kuwa mbunge halali wa Arusha Mjini na kuwaamuru
wajibu rufaa kumlipa gharama za rufaa hiyo.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Bernard Luanda kwa niaba ya
wenzake wawili Natalia Kimaro na Salum Massati waliokuwa wakisikiliza
rufaa hiyo, Mahakama ya Rufani ilisema wajibu rufani hawakuwa na haki ya
kisheria kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo ya uchaguzi
yaliyompa ushindi.
“Rufaa imefanikiwa na tunatengua hukumu, tuzo na amri ya Mahakama Kuu.
Tunamtangaza mrufani kuwa Mbunge wa Arusha Mjini,” ilisema Mahakama ya
Rufani katika hukumu yake hiyo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment