Serikali iache kutafuta mchawi, iende Mtwara
Katika
kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamamo, malumbano na vurugu
kuhusu mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam. Mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa kilometa
542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi kuliko miradi
mingine yote ya miundombinu iliyopata kutokea hapa nchini. Mradi huu
utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani 1.2 bilioni kutoka Benki ya
Exim ya China.
Wananchi
wa Mtwara kupitia maandamano ya tarehe 27 Desemba 2012 wametaka kujua
hatma ya maendeleo ya mikoa wa kusini kutokana na mradi huu wa bomba la
gesi. Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita wahaini, watu hatari
na wasio elewa. Imefika mahali inapotosha madai yao kwamba hawataki gesi
itoke Mtwara.
Kimsingi
Serikali haijajibu hoja yeyote ya msingi ya wananchi wa Mtwara kuhusu
mradi wa kusafirisha gesi. Badala yake imekuwa ikijaribu kupotosha madai
ya watu wa Mtwara kupitia mikutano na vyombo vya habari.
Tangu
maandamano haya yatokee, na baadaye mikutano ya hadhara na hatimaye
matukio ya kusikitisha ya kuharibu mali za watu, mauaji ya watu na
majeruhi mbalimbli, Serikali na hasa Wizara yenye dhamana ya mradi huu,
imekuwa ikitoa matamko kwenye vyombo vya habari badala ya kwenda Mtwara
kuzungumza na wananchi, kusikiliza madai yao na kuona namna ya
kutekeleza madai hayo. Kutokana na Serikali kutofanya hivyo, kusikiliza
na kuzungumza na wananchi wa Mtwara, vurugu mbaya sana zimeendelea
mkoani humo.
Mwezi
uliopita, Desemba 2012, tatizo lilionekana kuwa ndogo na lenye
kuhusiana zaidi na ukosefu wa kushirikishwa kwa wananchi. Badala ya
kushughulikia tatizo likiwa bado ndogo, Serikali imeona njia pekee ya
kushughulikia suala hili ni kutafuta mchawi na kwa wiki zote hizi
imekuwa ikisemakuwa wanasiasa na makampuni ya uwekezaji ya nje
yanachochea mgogoro
huu.
Leo
hali iliyopo mkoani Mtwara inasikitisha sana, maana mali za wananchi
zinaharibiwa, nyumba zinachomwa moto na watu wanapoteza maisha.
Tunalaani matukio haya kwa nguvu zetu zote, maana kinachotokea Mtwara si
Utanzania. Tusipowasikiliza wananchi na kutatua mgogoro huu kwa
kuwashirikisha, hali itazidi kuzorota wakati tukitupiana lawama.
Hivi
sasa serikali imeona njia pekee ya kushughulikia suala hili ni kutafuta
mchawi na kwa wiki zote hizi imekuwa ikisema kuwa wanasiasa na
makampuni ya uwekezaji ya nje yanachochea mgogoro huu.
Kwanza,
Serikali imekuwa ikiaminisha umma kwanza suala hili limechukuliwa
kisiasa. Pili, Serikali imekuwa ikirudia kusema kuwa baadhi ya makampuni
ya uwekezaji nchini na mataifa ya Magharibi yamekuwa yakichochea
wananchi wa Mtwara.
Katika
mwendelezo wa mtindo wa Serikali wa ‘management by press conferences’
jana Jumamosi Naibu Waziri wa Nishati na Madini ndugu George
Simbachawene aliwaambia wahariri kwamba mimi Zitto Kabwe ninachochea
wananchi wa Mtwara, ninatumiwa, na si mzalendo. Vile vile alitoa
vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi ni
gharama sawasawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo.
Katika
kipindi chote cha mgogoro wa Gesi Mtwara, sijafika Mtwara. Sijafanya
mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu, kama
Mtanzania kuhusu suala hili.
Nimeandika makala nne na zimechapishwa katika magazeti kadhaa hapa nchini na kwenye blogu yangu (zittokabwe.com).
Niliandika:
Utajiri wa Gesi Asilia: Tuwasikilize Watanzania wa Mtwara na Lindi.
Nikaandika tena: Tusipuuze mandamano dhidi ya Bomba la Gesi: Kilio cha
Uwajibikaji; Nikaandika tena: Mtwara : Serikali inavunja nchi kwa
kutosikiliza Wananchi; ni baadhi ya makala nilizoandika kuhusiana na
suala la Mtwara.
Sitaki
kubishana na Naibu Waziri ama Kiongozi yeyote ya Serikali kwa sasa.
Hatuwezi kuendelea kulumbana, kuzozana, kuzodoana na kurushiana maneno
wakati nchi yetu inaungua. Huu sio wakati wa kutafuta mchawi bali
kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yetu.
Yanayotokea
Mtwara ni fundisho kwetu kwa Taifa namna ya kukabili changamoto za
utajiri wa rasilimali, ili kuweka mkakati, mambo haya yanayotokea Mtwara
yasitokee tena Tanzania. Tutaweza kuzuia maafa haya iwapo tutaweka
uwazi katika mikataba, tutashirikisha wananchi kwenye unyonyaji wa
maliasili za nchi, na iwapo tutaweka uwajibikaji.
Rais Kikwete Kikwete ana majibu; ayatoe sasa kwa wana Mtwara
Kwa
mujibu wa Mpango Kabambe wa Umeme nchini (Power System Master Plan),
kulikuwa na mradi wa kufua umeme MnaziBay, ambao Rais Jakaya Kikwete
aliagiza utekelezwe mara moja. Serikali ieleze umma kuhusu mradi huo wa
kujenga kituo cha kufua umeme 300MW MnaziBay Mtwara na kujenga msongo wa
umeme wa 300KV mpaka Singida. Umeishia wapi? Ikumbukwe kuwa mnamo
tarehe 12 Oktoba 2012, Rais Jakaya Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa
mradi huu kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment
Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani,
ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme
kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga
njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.
Mradi huu ungegarimu dola za kimarekani milioni 684 na Rais aliagiza
utekelezwe haraka sana. Huu mradi uliishia wapi? Kwa nini Serikali ipo
kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara?
Taarifa ya Ikulu kuhusu mradi huu imeambatanishwa hapa.
Tufanyeje?
Hapa
tulipofikia ni lazima kwanza kabisa kusikia kilio cha wananchi wa
Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao. Swali kubwa kubwa la watu wa Mtwara na
Kusini kwa ujumla ni ‘tunanufaikaje’? Jibu la swali hili si ahadi za
miradi bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa kushughulikia
suala hili, kutoelewa madai ya wananchi na kuyapotosha.Viongozi wa
kisiasa wenye ushawishi kutoka pande zote, chama tawala na vyama vya
upinzani, waende Mtwara kuzungumza na wananchi, lakini wawasikilize
kwanza.
Lazima
viongozi tujenge utamaduni wa kusikiliza wananchi na si kuwahutubia tu.
Wananchi wa Mtwara wana madai ambayo lazima viongozi tukae kitako
kuwasikiliza kisha kufanya nao majadiliano ambayo yatatoa mwafaka. Rais
mstaafu, Ndugu Benjamin Mkapa ameshatoa kauli kuhusu suala hili. Ni
wakati mwafaka sasa kwa viogozi wengine kumuunga mkono kwa kwenda Mtwara
na kukaa na wananchi wa Wilaya zote za Mtwara, kusikiliza hoja zao na
kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hili. Wakati hatua hii
inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha vurugu za aina yeyote
ile, na Serikali isimamishe mradi mpaka hapo suluhu na wananchi
itakapopatikana.
Wakati
juhudi hizo zinaendelea Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba,
kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na
uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote kwa
umma Serikali imekuwa ikisema kwamba mradi utagharimu jumla ya dola za
kimarekani 1.2 bilioni, lakini katika taarifa ambayo Wizara ya Nishati
na Madini imesambaza jana kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini
imesema mradi utagharimu dola za kimarekani milioni 875. Usiri katika
mkataba huu unaashiria kwamba Serikali inaficha kitu. Hivyo njia pekee
ni kutaka mkataba uwe wazi kwa wananchi.
Wakati
tunawataka wananchi wa Mtwara kuruhusu utulivu, ni vema Serikali
ijiandae kutoa majawabu ya madai ya wananchi hao. Majawabu ya Serikali
yajikite kueleza wananchi wa Mtwara wanafaidikaje na rasilimali ya gesi
asilia kwa maendeleo yao. Wananchi wa Mtwara wanataka uwajibikaji wa
Serikali kwenye utajiri wa nchi, na wamechoka na porojo za orodha ya
miradi isiyotekelezwa.
Viongozi
twendeni Mtwara kusikiliza wananchi wetu. Nchi inaungua na hatuwezi
kuendelea kuzozana badala ya kuzima moto huu hatari kama vita vya
MajiMaji. Mimi nakwenda Mtwara haraka na mara baada ya viongozi wangu wa
chama kutoa ridhaa.
ZITTO KABWE
Mbunge, Kigoma Kaskazini (Chadema)
Waziri Kivuli wa Fedha
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni
This post was written by: Author Name
Your description comes here!
Get Free Email Updates to your Inbox!
Filed Under:
Michezo
on Sunday, January 27, 2013
Post a Comment