CHAMA cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimefuta wazo la
kuendesha mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mdahalo huo
ulikuwa ufanyike Februari 15, 2013 na tayari chama kilikuwa katika hatua
nzuri ya mazungumzo na wadhamini pamoja na kituo kimoja cha televisheni
kwa ajili ya kurusha 'live' tukio hilo, ambapo kesho ilikuwa tutangaze
utaratibu mzima wa mdahalo huo.
Katika
mazungumzo ya leo na uongozi wa kituo hicho ambao hautaki tukitangaze,
tumekubaliana kufuta wazo la mdahalo kwa sababu nafasi ya urais amebaki
mgombea mmoja, hivyo mdahalo hautakuwa na tija.
Dhamira ya
awali ya kufanya mdahalo ilikuwa kuwapa fursa wapiga kura wasikie vyema
sera za wagombea urais na Makamu wa Rais, ili wananchi wawasikilize
wagombea hao na pia wapiga kura wawatambue vizuri.
Hata hivyo
TASWA itatafuta utaratibu mwingine mzuri ambao utawezesha wagombea
kuzungumza na waandishi wa habari na kuulizwa maswali mbalimbali ambayo
tunaamini kwa kiasi fulani yatasaidia wapiga kura katika uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu. TASWA inawatakia kila la
kheri wagombea wote wa TFF waliobakia.
TASWA imekuwa
ikifanya mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF,
ilifanya hivyo mwaka 2001 na mwaka 2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya
wa live mwaka 2008, ambapo yote ilikuwa ya mafanikio makubwa.
Post a Comment