Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

HALIMA MDEE ATIMULIWA


Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee
.....................
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, ametimuliwa kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa madai kwamba ana maslahi ya upande mmoja katika mgogoro uliotokea bungeni juzi wakati Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Taarifa za uhakika zilizopatikana bungeni jana zilieleza kwamba Mdee ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, alizuiwa kuhudhuria kikao kilichojadili sakata hilo kwa kuwa alikuwa akishabikia vurugu bungeni.

Taarifa zaidi zimedai kwamba kumeibuka mvutano kuhusu kanuni iliyotumika kumruhusu Waziri Maghembe kutumia nusu saa kujibu hoja ya Mnyika wakati alipaswa kutumia dakika 15 kama wachangiaji wengine.

Jana Mdee alithibitishia NIPASHE kuwa alizuiwa kuhudhuria kikao cha kamati hiyo kwa maelezo kuwa ana maslahi na upande wa kambi ya upinzani juu ya suala la mgogoro wa hoja ya Mnyika ambayo ilipokwa na serikali juzi na kuiua.

Mdee alielezwa kuwa alikuwa bungeni siku hiyo na alishiriki katika kadhia iliyosababisha Bunge kuahirishwa kabla ya muda wake baada ya wabunge wote wa Chadema na NCCR-Mageuzi kusimama kwa muda mrefu na kuzuia shughuli za Bunge kuelendelea wakipinga kitendo cha kuvunjwa kwa kanuni za Bunge kwa kuipa nafasi serikali uondoa hoja binafsi ya Mnyika juu ya upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika jiji la Dar es Salaam.

Kamati ya Maadili imepewa jukumu la kuchunguza chanzo cha vurugu hizo kwa kuwahoji wabunge waliohusika na kadhia ya Jumatatu jioni ili kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa dhidi yao.

WAJUMBE WA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE

Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi (Mwenyekiti); Christopher Ole Sendeka; Rashid Ali Abdallah, Dk. Maua Daftari; John Chiligati; Dk. Christina Ishengoma; Riziki Omar Juma; David Kafulila; Vita Kawawa; Philemon Ndesamburo; Augustino Masele, Said Arfi; Augustine Mrema; Cynthia Ngoye; Halima Mdee na Gosbert Blandes.

Hata hivyo, Chadema imewaelekeza wabunge wake wote kutoitikia wito wa kamati hiyo hadi hapo Spika wa Bunge, Anne Makinda, atakapotoa uamuzi wa rufaa 10 ambazo wabunge hao wamekata kwake, lakini amezikalia tangu mwaka 2011.

Pia Chadema kimetishia kuwasilisha hoja ya kumng'oa madarakani Spika Makinda na Naibu Spika, Job Ndugai, kwa madai ya kukiuka kanuni za Bunge kwa kutotenda haki kwa pande zote, hasa kambi ya upinzani, kwa maana hiyo wamepoteza sifa za kuongoza muhimili huo.

WABUNGE HAWAJAHOJIWA
Wakati huo huo, Kamati hiyo bado haijawahoji wabunge wanaodaiwa kufanya fujo ndani ya Bunge.

Taarifa zilizoifikia NIPASHE, zilieleza kwamba hakuna hata mbunge mmoja ambaye amepewa samansi ya kuitwa kwenye kamati hiyo.

Katika hatua nyingine, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, amesema kitendo cha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumtuhumu kuwa ni mropokaji namba moja bungeni ni kwa sababu ya chuki na upendeleo dhidi ya wabunge wa upinzani.

Akizungumza na NIPASHE jana Lissu alisema siyo kweli kwamba amekuwa ni mropokaji bungeni kama Spika Makinda alivyomtuhumu na kwamba amekuwa akifuata kanuni zinazotakiwa kwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia na kuishauri serikali.

Alisema yeye ni miongoni mwa wabunge wachache ambao wanazifahamu kanuni za Bunge, Katiba ya nchi na sheria mbalimbali.

“Kuniita mropokaji ni kunifananisha na baadhi ya wabunge wa CCM ambao hawajui sheria wala wajibu wa Bunge…wanadhani kazi ya mbunge ni kuikingia kifua serikali na kuitetea, wamesahau kwamba wajibu wao ni kuishauri na kusimamia, " alisema.

Lissu alisema kamwe hawezi kuogopa kuisimamia serikali kama Katiba inavyomtaka na hawezi kuitetea pale inaposhindwa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

KAMATI KUCHUNGUZA MTAALA

Katika hatua nyingine, Bunge limeunda kamati ya wabunge sita kuchunguza mitaala ya shule ya awali, msingi na sekondari iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ili kubaini kama ina upungufu au la.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, wiki iliyopita, kuitaka serikali kuonyesha mitaala hiyo.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni jana kuwa amekabidhiwa mitaala hiyo na ameunda kamati hiyo ili ikajiridhishe juu ya jambo hilo.

Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni Mbunge wa Kibiti (CCM) Abdul Jabiri Marombwa; Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahya Kassim Issa na Mbunge wa Karatu (Chadema), Israel Natse.

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Benardetha Mushashu; Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Margaret Sitta na Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa.

Ndugai alisema wengine watakaoingia kwenye kamati hiyo kuwa ni Mbatia, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Kamishina wa Elimu, Mwanasheria wa Wizara na wataalamu wengine wa elimu.

Hata hivyo, Ndugai aliitaka kamati hiyo kufanya kazi yake jana na ifikapo leo iwe imekuja na majibu juu ya suala hilo. Wiki iliyopita, Mbatia aliwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu udhaifu katika sekta ya elimu na kutaka mfumo unaosimamia elimu nchini ufumuliwe.

Alitaja udhaifu uliopo katika sekta ya elimu kuwa ni pamoja na kutokuwapo sera ya pamoja kuhusu elimu, matatizo ya mitaala na utungaji wa vitabu vya kufundishia shuleni.
Hoja ya Mbatia ilizua mjadala mrefu bungeni kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mitaala, sera na mihutasari ya elimu.

Baadhi ya wabunge walitaka kamati ya Bunge na wengine walitaka iundwe tume huru ya kufuatilia suala hilo.

Mjadala huo uliendelea kwa Dk. Kawambwa kutetea mfumo wa elimu uliopo na mtaala, kabla ya wabunge kuchangia na Mbatia kuhitimisha hoja yake.

Akiwasilisha hoja yake, Mbatia aling’ang’ania kupatiwa mitaala hiyo, jambo ambalo Dk. Kawambwa alijibu kuwa ilikuwapo ingawa hakuwa nayo bungeni.
Baada ya majibu ya Dk. Kawambwa, Mbatia aliomba hoja yake iahirishwe hadi mitaala itakapowasilishwa bungeni.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama bungeni na kuhoji: “Katika kikao kilichopita, hata katika hansard, tulisema mtaala utawasilishwa katika kikao hiki, sasa wasiwasi wa mbunge (Mbatia) ni nini? Hata siku ya mwisho ya Bunge tutaleta.”

Baada ya kauli hiyo, Ndugai alipiga kura kwa kuuliza wanaotaka hoja imalizike na baada ya majibu, aliruhusu Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamisi Kigwangalla, kuwasilisha hoja binafsi kuhusu ajira kwa vijana na kilimo.

Hata hivyo, baada ya kumruhusu Dk. Kigwangalla, wabunge wa upinzani walitoka nje ya Bunge na kufanya mkutano wa dharura uliochukua dakika 38 katika ukumbi wa Pius Msekwa.

HAKIELIMU YAIBANA SERIKALI

Katika hatua nyingine, serikali imetakiwa kuacha ubabe wa kupangua hoja zinazotolewa na watalaamu wa masuala ya elimu, ambao wanafanya utafiti na kuainisha upungufu uliopo katika sekta hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na wanaharakati wa masuala ya elimu, ambao wameunga mkono hoja iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Mbatia, aliyetaka Bunge lichunguze udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu linalojishughulisha na masuala ya elimu, Elizabeth Misokia, aliwaaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote na kwamba, kitendo cha serikali kukosoa tafiti za watalaamu na kuzitupa, hakilengi kuijenga nchi na kuinua kiwango cha elimu nchini.

“Serikali isitumie nguvu nyingi kukosoa tafiti mbalimbali zinazofanywa na watalaamu kuhusu elimu, badala yake izifanyie kazi ili kuziboresha,” alisema Misokia.

Alisema sera ya elimu ya mwaka 1995 haieleweki inasema nini kuhusu elimu na kwamba, hata mitaala ya kufundishia nayo haileweki kwa walimu wanaoitumia kufundishia.

Misokia alisema sekta ya elimu nchini inakabiliwa na matatizo mengi, ukiwamo uhaba wa walimu, walimu kukata tamaa kutokana na serikali kuwapuuza, kushindwa kuwalipa madai yao ya siku nyingi pamoja na kufanya kazi katika mazingira magumu.

Matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu, ni pamoja na wakaguzi kushindwa kufika katika shule mbalimbali kwa ajili ya kuzikagua.
Alisema kati ya mwaka 2000 hadi 2002 elimu ya shule ya msingi ilipanuliwa, lakini hakuna juhudi zozote za kuwapo sera moja ya elimu itakayoisimamia kikamilifu.

Aliomba serikali kutengeneza kwanza sera yenye nguvu kuhusu elimu kabla ya kuanza kuandaa mitaala inayofanana nchini kote ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu inayofanana na iliyo bora.
 
CHANZO: NIPASHE
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top