Kwa ufupi
            
Tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani miaka 
saba iliyopita na kupewa kofia ya uenyekiti wa CCM, chama hicho kimekuwa
 kwenye minyukano ya siasa za visasi kiasi kwamba hakijawahi kuwa na 
utulivu wa kisiasa kama ilivyo sasa, miezi michache baada ya kufanyika 
mabadiliko kadhaa ya kiuongozi.
Tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani miaka 
saba iliyopita na kupewa kofia ya uenyekiti wa CCM, chama hicho kimekuwa
 kwenye minyukano ya siasa za visasi kiasi kwamba hakijawahi kuwa na 
utulivu wa kisiasa kama ilivyo sasa, miezi michache baada ya kufanyika 
mabadiliko kadhaa ya kiuongozi.
Uteuzi na baadaye uchaguzi wa wajumbe wa Kamati 
Kuu umeweka kando baadhi ya vigogo wa kisiasa hasa waliokuwa wakitajwa 
katika harakati za kuusaka urais katika uchaguzi wa 2015 na kuziingiza 
sura mpya ambazo huenda baadhi yao wanaweza kuingia katika 
kinyang’anyiro hicho.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa 
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa 
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ni vigogo ambao wamekuwa 
wakitajwa kupiga mbio hizo, lakini waliwekwa kando katika Kamati Kuu ya 
sasa.
Pia majina ya mawaziri na wizara zao kwenye mabano
 Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais – Kazi Maalumu), Dk John Magufuli
 (Ujenzi), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi) pamoja na Naibu Waziri wa 
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Katibu Mkuu wa 
UVCCM, Martin Shigela, pia hayakuwa sehemu ya waliopendekezwa kuingia 
katika CC ambacho ni chombo cha kufanya uamuzi mkubwa ndani ya CCM.
Profesa Mwandosya licha ya kuwa na matatizo ya 
kiafya, amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa watu muhimu katika mustakabali wa
 siasa za sasa za Tanzania wakati Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wamekuwa 
wakipigiwa chapuo na umma kwamba huenda wangefaa kuwania urais kutokana 
na kasi katika utendaji kwenye wizara wanazoziongoza.
Badala yake Kamati Kuu inawajumuisha makada ambao 
siyo wapya, lakini ambao wanaweza kutumika kubadili sura na mwelekeo wa 
siasa ndani ya CCM hasa tunapoelekea 2015, akiwamo Waziri Mkuu wa 
zamani, Dk Salim Ahmed Salim.
Hatua hiyo inaweza kuwa ni hatua ya kujaribu 
kujipanga kwa CCM katika kuzipa sura mpya siasa za ndani ya chama hicho.
 Dk Salim kama ilivyo kwa Profesa Mwandosya, alikuwa mpinzani wa Kikwete
 katika kinyang’anyiro cha urais wa 2005, ambaye bado anatizamwa kuwa 
mtu mwenye uwezo licha ya kwamba umri wake ni mkubwa.
Wengine ambao kuingia kwao katika Kamati Kuu ya 
CCM kunaweza kuwa na maana ya kubadili siasa za urais ni pamoja na 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Afya na
 Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na mwenzake kutoka Tanzania Visiwani
 ambaye alipata kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya 
Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha.
Dk Nchimbi anarejea Kamati Kuu ambako aliingia kwa
 mara ya kwanza akiwa na umri mdogo pale alipochaguliwa kuongoza Umoja 
wa Vijana wa CCM (UVCCM) na kuongoza jumuiya hiyo kwa miaka kumi 
mfululizo. Kwa mujibu wa kanuni za CCM, wenyeviti wa jumuiya za chama 
huwa ni wajumbe wa CC kwa mujibu wa nyadhifa zao. Nchimbi amekuwa mjumbe
 wa CC kwa miaka 10.
Hali kadhalika, Dk Mwinyi ni mmoja wa makada wa 
CCM ambaye amekuwa ndani ya CC kwa muda mrefu, wakati Nahodha alikuwa 
akiingia ndani ya kamati hiyo alipokuwa Waziri Kiongozi wa SMZ (kwa 
wadhifa wake).
Nahodha, Dk Mwinyi na Dk Nchimbi kwa nyakati 
tofauti wote wamepita katika wizara nyeti ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga 
Taifa. Dk Mwinyi wakati alipokuwa waziri, naibu wake alikuwa Dk Nchimbi 
ambaye baadaye alihamishiwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na 
Michezo na sasa Mambo ya Ndani.
Dk Nchimbi alichukua nafasi ya Nahodha ambaye sasa yupo ulinzi.
Mwingine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera na
 Uratibu), Steven Wassira ambaye katika siku za karibuni ametokea kuwa 
moja ya nguzo kuu za CCM katika kujibu hoja mbalimbali ndani na nje ya 
Bunge, kusuluhisha migogoro ya kichama na kupambana na wapinzani wakuu 
wa chama chake, ambacho ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Wassira aliongoza kwa kupata kura nyingi miongoni 
mwa makada wa CCM waliochaguliwa kuwa wajumbe wa NEC kupitia uchaguzi wa
 kitaifa, lakini amekuwa akitajwa kwamba ni mmoja wa wanaokusudia 
kuchukua fomu za urais katika uchaguzi wa 2015.
Katika mazingira ya kawaida hii ni CC mpya ya 
mwisho kuundwa na Rais Kikwete akiwa Mwenyekiti wa CCM kwani ndiyo 
inayotazamiwa kukivusha chama hicho katika kinyang’anyiro cha 2015 
ambacho yeye hatogombea kwani atakuwa amemaliza muda wake.
Umekuwa ni utaratibu wa CCM kwamba ni vigumu 
kumteua mgombea urais ambaye si mjumbe wa Kamati Kuu na kitendo cha 
baadhi ya vigogo wa kisiasa kuwekwa kando kunaweza kutafsiriwa kwamba ni
 kuwaweka kando katika kuwania nafasi hiyo na kuwapa fursa makada 
wengine ambao wanaonekana kuwa ‘watulivu’.
Licha ya kwamba Rais Kikwete ni mwenyekiti, lakini
 uwapo makamu wake, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman 
Kinana, kunakipa nguvu chama hicho kuendeleza utulivu uliopo na kupitia 
kwao, CCM wanaweza kufanya uamuzi mgumu ambao utawashangaza wengi kwa 
kumteua mgombea ambaye hafikiriwi na wengi kupeperusha bendera ya chama 
hicho.
Pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa 
Mataifa, Asha-Rose Migiro ambaye ameteuliwa hivi karibuni katika 
sekretarieti mpya, naye amekuwa akitajwa kwamba huenda akachukua fomu ya
 kugombea urais katika chama hicho.
Kwa upande wa Dk Mohammed Shein naye huenda 
akachukua fomu ya kugombea urais wa Muungano baada ya kuweza kufanya 
kazi na upinzani bila ya mikwaruzo mikubwa huko Zanzibar. Hata hivyo, 
CCM kama itatupa karata yake kwa Dk Shein itabidi kufanya kazi ya ziada 
kumnadi.
NA MWANANCHI
NA MWANANCHI
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Post a Comment