Dar es Salaam. Ofisi ya Bunge jana ilitangaza majina ya wenyeviti na
makamu wapya wa Kamati za Kudumu za Bunge huku Mbunge wa Jimbo la
Monduli, Edward Lowassa akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Kuchaguliwa kwa Lowassa kuongoza kamati hiyo kunaibua upya vita kati
yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, kutokana na wote kutajwa kutaka kugombea urais katika uchaguzi
mkuu ujao mwaka 2015.
Awali, Lowassa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na
Usalama, ambayo iligawanywa hivi karibuni na kuzaliwa kamati mbili; ya
Ulinzi na Usalama na Kamati ya Mambo ya Nje.
Kushinda kwa Lowassa kunakuja siku moja, baada ya wabunge wote wa CCM
kukutana katika kikao cha ndani kilichofanyika Ukumbi wa Karimjee na
kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kuwachagua
wenyeviti na makamu wa kamati hizo.
Habari za ndani kutoka katika kikao hicho zilieleza kuwa moja ya ajenda
zilizozungumzwa ni kuwataka wabunge kuwachagua wenyeviti kwa kufuata
taratibu na utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo, Naibu Spika Job Ndugai aliliambia Mwananchi Jumamosi kwamba
kikao hicho ni cha kawaida na walikuwa wakijadiliana matatizo yaliyopo
katika majimbo yao na jinsi ya kuyawasilisha serikalini.
Katika uchaguzi huo, Musa Azzan Zungu ambaye alikuwa makamu wa Lowassa
kabla ya kugawanya kwa kamati hiyo, amechaguliwa tena kushika nafasi
hiyo.
Uchaguzi wa wenyeviti na makamu wao ulifanyika jana katika Ofisi Ndogo
za Bunge jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada ya ofisi ya
Bunge kutaja majina ya kamati mpya 16 pamoja na wajumbe wake.
Uchaguzi huo umefanyika ukiwa umepita mwezi mmoja tangu kumalizika kwa
mkutano wa 10 wa Bunge ambapo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza
mabadiliko ya kamati hizo, huku akiifuta Kamati ya Hesabu za Mashirika
ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe.
Kutokana na mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitafanywa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kamati nyingine iliyofutwa ni ile ya Sheria Ndogo wakati zimeundwa
kamati mpya za Bajeti, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ya Ulinzi
na Usalama.
Taarifa za ndani kutoka katika chaguzi hizo zinaeleza kuwa Zitto ambaye
alikuwa akichuana na John Cheyo, alipata kura 13 kati ya 17 zilizopigwa
na wajumbe wa kamati yake, hivyo Zitto sasa ndiye Mwenyekiti wa Kamati
ya Hesabu za Serikali (PAC).
Chanzo: Mwananchi
Post a Comment