Rais wa TFF, Leodegar Tenga
.............
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa msimamo wake juu ya
uamuzi wa serikali wa kuibatilisha katiba mpya ya shirikisho hilo ya
mwaka 2012 na kuitambua ya mwaka 2006, kwa kusema kuwa agizo hilo
haliwezekani na halitekelezeki.
Februari 25, Waziri wa Habari, Vijana na Michezo, Fenella Mukangara
aliibatilisha katiba hiyo mpya kwa hoja kuwa ilipitishwa kinyume na
sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa vile marekebisho yake
yalifanywa kwa njia ya waraka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kikao cha Kamati
ya Utendaji ya shirikisho hilo, Leodegar Tenga - sentahafu wa zamani wa
Yanga, Pan African na Taifa Stars, alisema Waziri Mukangara anapaswa
kutafakari upya uamuzi wake.
“Ipo haja kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk.
Fenella Mukangara, kufikiria upya uamuzi wake wa kutengua usajili wa
Katiba ya TFF ya mwaka 2012 na kutaka itumike ya mwaka 2006, kwani
hautekelezeki,” alisema Tenga aliyeliongoza shirikisho hilo tangu 2004.
Alisema ni muhimu jambo hilo likaangaliwa upya kwa sababu athari zake
ni mbaya na pengine Waziri Mukangara hakushauriwa vizuri kabla ya
kufanya uamuzi huo.
“Kamati ya Utendaji ya TFF haitaki kubishana na mheshimiwa waziri
hata kidogo, ila tunaamini wakati anatamka haya hakufahamu madhara
yake, athari zake na ugumu wa utekelezaji wake. Kwa waliomshauri hili,
wamemshauri vibaya,” alisema.
Alisema rai ya TFF kwa waziri ni kuwaita ili wamweleze ni kitu gani
wafanye kunusuru soka ya Tanzania kwani wanaamini jambo hili litakwisha
baada ya kumwelimisha hasa kutokana na ukweli kuwa kabla ya kufanya
uamuzi huo hakuwasikiliza.
Katika mkutano huo, Tenga alianza kwa kusema kuwa TFF inaiheshimu
sana serikali, hivyo inaheshimu maagizo yaliyotolewa na waziri, lakini
akaongeza kuwa TFF ina wajibu wa kutoa ufafanuzi juu ya maagizo hayo.
Tenga alisema lengo la kuelezea historia ya TFF ilikotoka ni kubaini
migongano ya maagizo hayo na taratibu za shirikisho hilo ambazo kwa
bahati mbaya zinasigana na maagizo hayo.
Alisema TFF ni chombo cha wanachama, ambapo wanachama wake ni vyama
vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu na ina taratibu za
kufanya uamuzi kwa mujibu wa katiba yake na za wanachama wake ambazo
zimeidhinishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tenga alisema si TFF pekee, bali vyama vya nchi zote ambavyo
vimeunganishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), vinaheshimu
na kufuata maagizo na miongozo ya chombo hicho cha juu zaidi katika
mchezo wa soka duniani.
Alisema TFF haitakiwi kuingiliwa katika uongozi na uendeshaji wake,
kwani jambo hilo likitokea rungu la FIFA litaiangukia, na madhara yake
ni makubwa. Miongozo ya FIFA inasisitiza uhuru wa wanachama wake katika
uendeshaji shughuli za mpira wa miguu, na iko kwenye Katiba ya TFF.
“Sheria za nchi ndizo zilizozaa Katiba ya TFF. TFF ni chama kamili,
kinatakiwa kufanya uamuzi wake ili mradi uzingatie madhumuni ya
kuanzishwa kwake. Leo TFF ikiacha mpira wa miguu na kuanza
kujishughulisha na gofu, hapo msajili ana haki ya kuingilia,” alisema.
Kuhusu maagizo ya waziri, Tenga amesema kifungu cha 11 cha Sheria ya
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kinazungumzia usajili wa chama, na si
marekebisho ya katiba, ingawa kanuni zinahusu marekebisho ambapo
ameongeza kuwa uamuzi wa marekebisho ni wa mkutano mkuu na si msajili.
“Ukienda kuomba viza, fomu unapewa na yule anayekupa viza. TFF
tulipowasilisha marekebisho ya katiba hatukupewa fomu. Msajili akasema
sawa. Jambo la kujaza fomu si la TFF, ndiyo maana tunasema ipo haja ya
jambo hili kufikiriwa upya.
“Usajili tayari umepita, kwamba msajili hakutoa fomu, mwathirika
anakuwaje TFF? Tunaona ni muhimu jambo hili likaangaliwa upya,” alisema
Tenga na kuongeza kuwa utaratibu wa kusajili katiba ya 2006 ambayo
ndiyo waziri ameagiza itumike, ulikuwa huo huo uliosajili katiba ya
2012.
Akizungumzia historia ya TFF kutoka mikononi mwa BMT, Rais Tenga
amesema ni zao la Katiba ya 2004 ambayo ilifanyiwa marekebisho ukumbini
na kugongwa mhuri na msajili hapo hapo na kuingia kwenye uchaguzi.
Katiba hiyo ndiyo iliyoiondoa BMT kuisimamia TFF.
“Huko ndiko tulikotoka, si kwa kulazimishwa, bali kwa kupewa katiba
ya 2004. Katiba ina utaratibu mzima wa kufanya uamuzi. Maelekezo ya
waziri yamesahau huko tulikotoka siku nyingi. Uhalali wa marekebisho
unatokana na ridhaa ya mkutano mkuu. Hiyo ni kwa mujibu wa katiba
yenyewe, hakuna nafasi ya BMT,” alisema.
Alisema katika maagizo ya waziri, ameitaka TFF kufuata katiba ya 2006
na kanuni za BMT, lakini katiba hiyo hiyo ya 2006 haina nafasi ya BMT,
na hata kama TFF ingetaka kutekeleza hilo haliwezekani.
“Kwa maagizo haya inaonekana waziri kashauriwa vibaya. Tunajua
hakuwepo katika nafasi hiyo (2004) wakati wa makubaliano kati ya
serikali na FIFA kuacha mpira wa miguu ujiendeshe wenyewe,” alisema
Tenga.
Pia amezungumzia umuhimu wa katiba toleo la 2012, kwani kuna
marekebisho mengi yalifanyika mwaka 2007, 2008, 2009 na 2011 ambapo
ukiyafuta maana yake unakiweka pembeni Chama cha Mpira wa Miguu
Zanzibar (ZFA), Bodi ya Wadhamini, wanachama wapya (mikoa), Bodi ya
Ligi, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi, Leseni za Klabu na Kanuni za Fedha.
“Kwa uamuzi huu yote yaliyofanyika hayana maana. Waziri sidhani kama
alikuwa anafahamu athari za maagizo yake. Kama angelijua asingefanya
uamuzi huo. Si rahisi kurudi katika Katiba ya 2006.
“Hao wajumbe wa Katiba ya 2006 unawapata wapi? Maana yake hata vyama
wanachama ni batili kwa vile vimerekebisha katiba zao 2009 na 2010,”
alisema.
Alisema kwa serikali kuifuta, maana yake ni kutengua uamuzi wa TFF
ambapo madhara yake ni nchi kufungiwa, ambapo timu za taifa hazitacheza
mpira, klabu hazitashiriki michuano ya kimataifa na wadhamini nao
watakaa pembeni kwa vile hawawezi kudhamini timu ambazo hazishindani
kimataifa.
“Dhana kwamba tukae tu tusicheze nje, ni dhana ya watu walio nje ya
soka. Dhamira yetu ni kuhakikisha hatufungiwi. Waziri ametuagiza
tupeleke barua FIFA kuwa ametengua marekebisho ya katiba. Hatupeleki
hivyo, kwani hiyo ni Government interference, watatufungia.
“Nia yetu bado ni waziri kutupa nafasi ya kutusikiliza,” alisema
Tenga na kuongeza kuwa kuhusu uchaguzi kwa vile FIFA wanakuja, ombi la
TFF kwa waziri ni kuacha kwanza mchakato uendelee hadi ufike mwisho.
“FIFA wanakuja, tuwasubiri. Nilidhani utaratibu huo utaheshimika.
Kama mtu wa mpira haitaki FIFA anataka nini? Ahadi yetu ni kuhakikisha
watu wanapewa haki. Hiyo ndiyo ahadi yetu na tumeisimamia, na ndiyo
maana FIFA wanakuja,” alisema.
Akijibu swali kuhusu waraka, Rais Tenga amesema marekebisho ya katiba
hayakufanywa kwa siri, ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya
marekebisho hayo kwa njia ya waraka ilipatikana ambapo 70 waliunga
mkono na 33 walikataa.
Post a Comment