![]() |
| jengo lilibomolewa |
SIKU chache baada ya jengo
la ghorofa 16 kuporomoka na kuua watu 36 Dar es Salaam, Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu Dodoma (CDA), imevunja nyumba ambayo ilikuwa ikiongezwa ghorofa
kinyemela.
Kwa hatua hiyo, imesema pia
itaendelea kuwa makini na kutoruhusu ujenzi holela hasa wa maghorofa.
Hayo yalisemwa juzi na
Kaimu Mkurugenzi wa CDA, Pascas Muragili katika mkutano wake na waandishi wa
habari.
Jengo lililovunjwa lipo
katika barabara ya 11 mjini hapa, ambapo mhusika ametambuliwa kwa jina moja la
Massawe.
Alibainisha kuwa mmiliki wa
jengo hilo amekimbilia mahakamani kufungua kesi kupinga kuvunjwa kwa jengo
lake, akidai kuonewa.
Alisema hakukuwa na kibali
cha ujenzi huo, kwani nyumba hiyo ilikuwa ya kawaida na mmiliki aliamua
kuongeza ghorofa juu.
Akizungumzia suala la
wapangaji wa nyumba za CDA zilizopo Kikuyu kugoma kuondoka kupisha ukarabati, alisema kwa kuwa
suala hilo liko mahakamani watasuburi mahakama iamue.
Alisema mwaka 2008, CDA
ilipandisha kodi katika nyumba hizo ambapo walikuwa wakilipa Sh 22,000 kwa
vyumba vitatu, Sh 18,000 vyumba viwili na nafasi kubwa na Sh 15,000 kwa vyumba
viwili na nafasi ndogo.
Alisema walipendekeza
kupandisha kodi iwe Sh 55,000 kwa vyumba vitatu ndipo wapangaji wakasema walikuwa
wakionewa kodi kubwa hawalipi na ilikuwa imekwenda kinyume na makubaliano ya
siku za nyuma.
Aliongeza kuwa wapangaji
hao walikwenda Baraza la Ardhi la Wilaya ambalo liliamua walipe kodi mpya ya Sh
55,000 lakini hawakukubaliana na uamuzi huo na badala yake kukata rufaa
Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Baraza.
Katika uamuzi Mahakama Kuu
iliridhika kwani kulikuwa na makubaliano kati ya wapangaji na CDA na mahakama
ilisema mamlaka hiyo hairuhusiwi kupandisha kodi hadi itakapofanyika ukarabati
nyumba zake.
Pia baada ya matengenezo,
kodi mpya ya CDA lazima iendane na soko na kutokana na makubaliano hayo ya
mahakama, wakatafuta mkandarasi ili kufanyia matengenezo makubwa katika nyumba
hizo ikiwemo kurekebisha mfumo wa vyoo, lakini wapangaji hao walikataa na kukimbilia
tena mahakamani.
Alisema kuwa kuna jumla ya
familia 174 katika nyumba hizo na mafundi hawawezi kufanya lolote mpaka
wapangaji hao wahame kutokana pia na sababu za kiafya.
Aliongeza kwamba kwa kuwa
wapangaji hao wamekimbilia mahakamani na Mahakama Kuu kuamuru wasiondolewe
mpaka kesi ya msingi itakaposikilizwa,
wanasubiri uamuzi huo ili waone nini cha kufanya.
Pia alibainisha kuwa
wafanyakazi wanne kati ya 14 ambao ni wapangaji katika nyumba hizo tayari
wameondoka na waliobaki wako mbioni kuhama.
Source Sifa Lubasi,Habarileo

Post a Comment