Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limelitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanza upya mchakato wa uchaguzi baada ya kubaini kasoro iliyotokana na ukosefu wa kutokuwepo vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.
FIFA ambayo ilituma ujumbe wake katikati ya mwezi uliopita kufanya utafiti kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa TFF ambao ulisimamishwa baada ya baadhi ya wagombea kulalamika, imetaka uchaguzi ufanyike kabla ya tarehe 30 Oktoba 2013, lakini ukitanguliwa na mabadiliko ya katiba ambayo yatahusisha uundwaji wa vyombo vya kushughulikia ukiukwaji wa maadili.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia
waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa shirikisho hilo kuwa
suala la Tanzania lilijadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Dharura ya
FIFA kilichofanyika tarehe 28 Aprili 2013 na maamuzi yake kutumwa juzi
kwa barua iliyosainiwa na KatibuMkuuwa FIFA, Jerome Valcke.
Baada ya kupokea barua hiyo, Rais wa
TFF alifunga safari kwenda Dodoma jana kukutana na Mheshimiwa Waziri na
Naibu wake pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
“Matarajio yetu sote yalikuwa kupokea
majina ya waliopitishwa ili tufanye uchaguzi. Kinyume chake tumepokea
maagizo hayo. Hata hivyo tumeona kuwa hili ni jambo la kheri kwa vile
siyo tu haki itatendeka bali pia itaonekana imetendeka.” alisema Tenga,
ambaye alishatangaza kuwa hatagombea tena urais baada ya kuliongoza
Shirikisho kwa vipindi viwili vya miaka minne kila kimoja.
“Lengo letu ni kuhakikisha maagizo
hayo yanatekelezwa na uchaguzi kufanyika mapema iwezekanvyo kabla ya
tarehe iliyotolewa. Yale mambo nayoweza kufanyika kwa pamoja yatafanyika
ili tuharakishe utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na FIFA.”
Uchaguzi wa TFF ulipangwa kufanyik
tarehe 23 na 24 Februari 2013 na ulikuwa ukielekea ukingoni, lakini
baadhi ya wagombea walienguliwa katika hatua ya mwisho na Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi ya TFF na ndipo walipo andika barua FIFA kuomba
iingilie kati.
Rais Tenga alisema kuwa ujumbe wa FIFA
ulikutana na pande zote zilizoathiriwa na mchakato wa uchaguzi na
kwamba baada ya kukusanya taarifa hizo, maagizohayo ya FIFA sasa
yatakuwa ni suluhisho la matatizo ya muda mrefu katika uendeshaji wa
mpira wa miguu nchini.
Katika barua hiyo, FIFA imeiagizaTFF:
- Kuunda vyombo sahihi (Kamati ya Maadili itakayokuwa na vyombo viwili ambavyo ni cha kutoa maamuzi ya awali na cha rufaa) ambavyo mamlaka yake yatakuwa ni kushughulikia masuala ya ukiukwaji wa maadili;
- Kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuzingatia uundwaji wa vyombo hivyo;
- Kuanza upya kwa mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji kwa kufungua milango kwa wagombea ambao walishachukua fomu na wagombea wapya:
- Shughuli hiyo ikamilike ifikapo tarehe 30 Oktoba 2013.
Katika kutekeleza hayo, TFF inatakiwa
iitishe Mkutano Mkuu wa Dharura kwa ajili ya kufanya mabadiliko ya
Katiba kwa ajili ya kuunda kamati hizo za maadili na Kanuni za Uchaguzi
kabla ya kuendelea na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Kamati Mpya ya
Utendaji.
Katika maoni yake FIFA imeeleza kuwa
katika mchakato, Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua au kupitisha
baadhi ya wagombea kwa kubaini kuwa walikiuka Ibara ya 9 (7) ya Kanuni
za Uchaguzi na pia Ibaray a 29 (7) ya Katiba ya TFF ambavyo vinahusisha
suala la kufungua kesi mahakamani, kufuja fedha za shirikisho na ukosefu
wa uwajibikaji wa pamoja.
Hata hivyo, FIFA ilisema kuwa watu hao
walitakiwa waadhibiwe kwanza na kamati husika (kamati za maadili) kabla
ya kuenguliwa na kamati za uchaguzi za TFF.
“Kutokana na ukosefu wa kamati za
maadili matokeo yake, mmoja wa wagombea amekuwa akienguliwa kwenye
uchaguzi kila anapombea bila ya kujua adhabu yake ni ya muda gani,”
inasema barua hiyo ya FIFA.
Rais Tenga ameagiza kuitishwa kwa
kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya TFF kupokea maagizo ya FIFA
na kupanga ratiba ya utekelezaji wake kwa lengo la kuhakikisha kuwa
mchakato huu unatekelezwa mapema iwezekanavyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Post a Comment