Ndugu zangu,
Mwanafalsafa Jean- Paul Sartre
anasema; “ Hell is the other people” – Kwamba jehanam ni wale wengine,
anataka pia tukubaliane, kuwa pepo yaweza kuwa ni wale wengine.
Na hakika, tofauti ya mwanadamu na
mnyama iko kwenye kufiri. Mnyama anaongozwa na hisia, lakini mwanadamu
anapaswa aongozwe na kufikiri. Ndio maana ng’ombe anaweza kumpanda mama
yake. Ni hisia tu zitakazoongoza tendo lake.
Hivyo, mwanadamu kwenye mambo ya msingi hapaswi kabisa kuongozwa na hisia ikiwamo ushabiki. Anapaswa kfikiri.
Vinginevyo, ni ukweli, kuwa kijamii,
mwanadamu anaweza kuwa kiumbe anayeishi kwenye mahusiano ya kirafiki na
kiadui na wenzake. Na katika hilo la uadui, wanadamu, kama ilivyo kwa
wanyama, wanaweza kushindania na hata kugombania vingi; iwe fedha,
mashamba, wanawake na hata kivuli cha mti.
Ndio, unaweza kabisa kuwakuta wanadamu
wawili wanagombania kivuli cha mti, kwamba nani mwenye haki ya kukaa
kivulini. Na wanaweza kugombana mpaka akatokea mwendawazimu atakayekuja
kuukata na huo mti wenyewe. Na wanadamu hao watabaki wakitazama juani.
Hoja yangu hapa, kuwa lililo la msingi
ni kuwa wanadamu tunategemeana. Kwamba panapo kushindania jambo,
mwanadamu, tofauti na mnyama, anapaswa kufikiri sana. Atangulize kwanza
hekima na busara.
Na kwenye mgogoro wowote ule,
mwanadamu ayape mazungumzo nafasi ya pekee katika kufikia muafaka, na si
vurugu au mapigano. Kwenye mgogoro, na kwenye kuitafuta amani,
panakosekana mazungumzo ina maana ya uwepo wa mazingira ya kuvunjika
kwa amani. Hapa Serikali inapaswa iandae haraka mazingira ya
mazungumzo katika kuitafuta suluhu.
Ndugu zangu,
Nikiwa shuleni miaka ile ya 80 pale
aliyekuwa Waziri Mkuu, Dr. Salim Ahmed Salim alipotembelea Mtwara na
kukutana na umasikini uliomstusha sana. Kule Mtwara Dr. Salim alikutana
na Watanzania waliovaa magunia na miguuni hawana hata kandambili. Na
kwenye jua kali walijipanga kando ya barabara kumpokea. Kwenye jua kali
walikusanyika kumsikiliza Waziri Mkuu wao.
Ni kule Mtwara inasemekana Dr. Salim,
kwa mara ya kwanza, alipofikia maamuzi ya kutoa ruhusa ya mitumba
kuingizwa nchini. Maana, kulikuwa na Watanzania wengine wengi nje ya
Mtwara waliokuwa kwenye hali ya umasikini wa kufikia kuvaa nguo za
viraka na kushindwa hata kuvaa viatu vya matairi ya magari. Tunajifunza nini?
Kwamba ni kweli Mtwara na sehemu
nyingine za nchi zimekuwa nyuma sana kimaendeleo. Na leo tunaposikia
Mtwara kuna gesi, nakubaliana na Rais Jakaya Kikwete, kuwa gesi hiyo
haiwezi kuwa ni ya WanaMtwara tu. Ni gesi ya Watanzania wote.
Ni vema na ni busara, na kwa
kuwashirikisha wazee wa Mtwara, kuwa WanaMtwara wakasikilizwa. Kuna ya
msingi ambayo WanaMtwara na Serikali wanaweza kukubaliana kwenye meza ya
mazungumzo.
Hata kama tunakubaliana, kuwa
rasilimali za nchi ziwasaidie pia watu wa eneo inakotoka rasilimali
hiyo, lakini kamwe, tusikubaliane na hoja kuwa gesi iliyo Mtwara ni ya
WanaMtwara. Kwamba dhahabu ya Geita ni ya watu wa Geita, twiga wa Ruaha
ni wa Wahehe na kadhalika. Haya si mawazo mazuri kuyapandikiza katika
nchi.
Ni mawazo ya hatari yanayoweza
kupandikiza chuki, sit u miongoni mwa wananchi na Serikali, bali hata
miongoni mwa wananchi wenyewe wa maeneo tofauti. Ni mawazo yenye
kupandikiza pia fikra za kibaguzi.
Na tufikiri hili, je, kama gesi ile
iliyopatikana kule Mtwara, Tanzania na Msumbiji nayo ingesema ni ya
kwake, WanaMtwara wangesemaje kama watu wa mikoa mingine ya nchi hii
nao wangesema wapelekwe wanajeshi wa Kimakonde, Kiyao na Kimakua tu
wakambapane na majeshi ya Msumbiji kutetea ‘ Gesi ya Mtwara!’?
Naam, ya kule Mtwara isije ikawa yale yale ya kugombania kivuli.
Maggid Mjengwa,
Iringa,
0754 678 252
1 comments:
cha kufanya ni serikari kukaa na wanaMtwara kuangalia watanufaika vipi na hiyo gesi wawekana sawa mambo yatakuwa mazuri.
ReplyPost a Comment