Mwanza. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Dk
Charles Kitima amekitabiria kifo Chama Cha Mapinduzi kama kitaendelea na
mtindo wa kuwanyima fursa wazawa katika maendeleo.
Akizungumza katika kongamano la kujadili amani na
maendeleo na mpango wa miaka mitano wa kukuza uchumi na kuondoa umaskini
nchini lililofanyika chuoni hapo jijini Mwanza, Dk Kitima alisema nchi
haiwezi kufikia dira ya maendeleo ikiwa Serikali imeshindwa kutoa
kipaumbele katika utawala mzuri wa rasilimali na wazawa:
“CCM isipojirekebisha itakufa mapema kama isipoipa
kipaumbele sekta binafsi ya wazawa katika kusimamia rasilimali ya
nchi.Tunataka rasilimali za nchi tusimamie wenyewe,” alisema Charles
Kitima.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Nchi katika Ofisi
ya Rais, Uhusiano na Urtatibu, Steven Wassira aliyekuwa mgeni rasmi,
aliongeza kuwa nchi itaendelea kwa kuwapa fursa wananchi wake.
Kwa upande wake Waziri Wassira alikiri kuwa
umaskini wa Tanzania unasababishwa na kutokuwapo kwa uzalendo, kupungua
kwa uadilifu na mfumo mbovu ya ufuatiliaji na utekelezaji wa mipango.
“Uadilifu umekuwa mdogo sana kwa viongozi wetu wa leo. Mawazo
yaliyotawala ni wizi tu na mimi sina mpango wa kuiba”alisema Wassira.
Hata hivyo Wassira alisema kutokuwa na uelewa
tulikotoka nayo ni sababu kubwa kwa wananchi kutokujua maendeleo
yaliyofikiwa kwa miaka 50 ya uhuru.
“Tanzania ni nchi tuliyoirithi ikiwa ni shamba tu
hatukukuta kitu. Hapakuwa na barabara za kutosha, elimu haikupewa
kipaumbele, kutoka wasomi wachache wa mwaka 1961 sasa kuna vyuo 44’’
alisema.
Naye Mhadhiri wa Sheria chuoni hapo, Adelardius
Kilange alisema tatizo la umaskini nchini linatokana na wananchi kukosa
misingi imara ya itikadi ya siasa na uchumi wa jamii na kwamba ipo haja
kwa Serikali kujipanga.
NA MWANANCHI
NA MWANANCHI

Post a Comment