Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

MAKALA YA UCHAMBUZI MCHEZO WA TANZANIA VS IVORY COAST - ILIKUWA LAZIMA IVORY COAST ISHINDE NDANI NA NJE YA UWANJA



  MAKALA HII kwa hisani kubwa ya Shaffih Dauda in Sports.
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefungwa mabao 4-2 dhidi ya Ivory Coast na kuzima harakati zake za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014 huko Brazil.
Watanzania wengi na wadau wa michezo walidhani Taifa Stars ingeweza kusonga mbele katika harakati hizo za kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014, lakini sasa ukweli umejidhihirisha.
Sasa wengi wamekubaliana na uhalisia wa mambo kwamba, inahitaji muda kidogo kuona Taifa Stars ikisonga mbele katika kuelekea kufuzu Kombe la Dunia na siyo rahisi kama ilivyodhaniwa hapo kabla.
Ni mambo mengi yaliyotokea katika mchezo dhidi ya Ivory Coast ambayo yaliigharimu Taifa Stars licha ya uwanja kujaa idadi kubwa ya mashabiki waliokuwa wakiishangilia timu yao bila kuchoka.
Jambo la msingi ni kwamba, Taifa Stars ikiwa katika harakati za kuhakikisha inafuzu Kombe la Dunia wengi tulisahau kwamba, kwa ‘reality’ ilikuwa ngumu kwa Taifa Stars kufuzu fainali hizo japokuwa kwa mapenzi tulidhani timu hii ingeweza kufuzu kwa kuanza na vipigo kwa timu za Morocco na Ivory Coast.
Tukitazama mchezo kati ya Taifa Stars na Ivory Coast kuna baadhi ya mambo yalionekana kwamba bado tuna safari ndefu ya kufuzu Kombe la Dunia kama kweli tuna nia ya kufanya hivyo.
Mambo mengi mno yalijitokeza katika mchezo kati ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast na haya ni machache kati ya mengi yake;

TAIFA STARS ILICHEZA KUFURAHISHA MASHABIKI SIYO KUIFUNGA IVORY COAST
Kiungo wa Manchester City, Yaya Toure alicheza kama mshambuliaji na alitimiza majukumu yake kama straika hasa kwa kutokubali kukaa na mpira kwa muda mrefu licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Wakati Toure mwenye uwezo wa kumiliki mpira atakavyo na kufanya jambo lolote hakutoa nafasi hiyo zaidi ya kutafuta ushindi kwa timu yake, viungo na wachezaji wengi wa Taifa Stars walikuwa wakitumia muda mwingi kukaa na mpira bila ya sababu ya msingi.
Kiungo Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ mara nyingi alikuwa kitumia muda mwingi kukaa na mpira na kutaka kupambana na wachezaji wa Ivory Coast licha ya kuonekana wazi kwamba mara zote alizidiwa nguvu.
Tazama hata Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Frank Domayo walikuwa wakitumia muda mwingi ‘ku-hold’ mipira huku wakitoa pasi zisizo na macho na kujikuta wakipoteza mipira mingi kutokana tu na vitendo vyao vya kuchelewesha mipira.
Pamoja na vitendo hivyo kuwa hatari kwa timu, lakini mashabiki walikuwa wakiwashangilia kwa nguvu viungo wa Taifa Stars bila ya kujua madhara ya kufanya hivyo. Hao walijali zaidi kushangiliwa kuliko umuhimu wa mchezo husika.
Taifa Stars ilihitaji zaidi kucheza kwa kutokubali kukaa na mpira kwa muda mrefu kwa wachezaji wake ili kuitengeneza nafasi za haraka za kupata bao ili iweze kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Kuanzia Sure Boy, Kiemba, Kazimoto na Domayo, wote walionekana kufurahishwa na kelele za mashabiki waliokuwa wakiwashangilia kutokana na chenga na madoido mengine waliyokuwa wakiyafanya uwanjani.

SAFU YA ULINZI ILIPAPARIKA
Ilikuwa kama kila mchezaji ameahidiwa kiasi kikubwa cha fedha, kwani mara nyingi wachezaji wa Taifa Stars hawakucheza katika nafasi zao na hilo liligharimu timu na kujikuta wakilala mabao 4-2.
Erasto Nyoni ndiye beki anayeweza kuondoka na lawama nyingi lakini halikuwa kosa lake wakati mwingine kwani alilazimika kwenda katikati kusahihisha makosa ya mabeki wa kati na kuisahau nafasi yake.
Ilionekana wazi kwamba yalikuwepo mawasiliano hafifu juu ya kutengeneza mtego wa kuotea yaani ‘offside trick’ na matokeo yake Ivory Coast walitumia vyema mwanya huo na kujipatia mabao manne.
Baada ya kuonekana ‘njia’ tangu dakika za mwanzo, beki Erasto Nyoni inaonekana hakupata ushauri wa kutosha kuhusu kutulia na kucheza soka kwani hata makelele ya mashabiki yalimfanya aonekane mtu asiyefaa kikosini. Lakini alikuwepo benchi anayeweza kumudu nafasi yake moja kwa moja?

NGUVU HAFIFU
Wachezaji wengi wa Taifa Stars walionekana kutokuwa na nguvu ya kupambana na wenzao wa Ivory Coast kutokana na hali halisi ya miili yao.
Sure Boy mfupi na mwenye mwili mdogo alionekana kama mchezaji wa kawaida mbele ya Yaya Toure mwenye mwili mkubwa na nguvu, na mara nyingi Toure aliiwahi mipira ambayo ingeweza kuwahiwa na Sure Boy.
Domayo naye hakuweza kufua dafu mbele ya Traore Lucina na Jean Jacques ambao wote ni watu wa miraba minne. 
   
WAO WALIMKATAA KALOU, SISI TUKAFUATA SAMBUSA
Kabla hata ya mapumziko, waandishi kadhaa wa Ivory Coast walionekana kutopendezwa na uchezaji wa Salomon Kalou ambaye muda mwingi kila alipopewa mpira alikuwa akitaka kukaa nao kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa kina Sure Boy na wengine wa Taifa Stars.
Waandishi hao walionekana wazi kuchukizwa na hali hiyo na mara kwa mara walionyesha wazi kutoridhika na uchezaji wa Kalou.
Ulipofika wakati wa mapumziko, waandishi hao walishuka chini katika vyumba vya kubadilishia na kuzungumza na baadhi ya maafisa wa timu yao ili kutazama uwezekano wa kumpumzisha Kalou kwa maslahi ya nchi.
Wakati hayo yakitokea kwa Ivory Coast, waandishi wa Tanzania walikuwa wamekaribishwa ukumbi wa VIP kupata vitafunwa kama sambusa, mishikaki na vinywaji baridi, hao hawakuwaza kupeleka mawazo yao kwa benchi la ufundi na hata wangefanya hivyo wasingesikilizwa kutokana na utaratibu ulivyo.
Mbaya zaidi siyo waandishi tu, hata viongozi kadhaa wa Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars nao walionekana wakiwa VIP wakijichana kana kwamba Taifa Stars ipo katika nafai nzuri. Kumbuka hadi muda huo timu ilikuwa ipo nyuma kwa mabao 3-2.
HONGERA ULIMWENGU
 
Kama kuna mchezaji wa Ivory Coast aliyeomba mpira uishe haraka kuliko wengine basi ni Bamba Souleman ambaye alikuwa akicheza kama beki wa kati anayemkaba mshambuliaji wa Taifa Stars, Thomas Ulimwengu.
Ulimwengu alimmudu vizuri Bamba kiasi cha kumkimbiza na kuufanya mpira atakavyo hadi kufunga bao moja. Mara nyingi Bamba alizidiwa nguvu na kasi na Ulimwengu kiasi cha kulalamikiwa na wenzake.
Kama wachezaji wanne tu wa Taifa Stars wangeweza kucheza kama Ulimwengu, ni wazi timu hiyo ingepata matokeo mazuri na ya kuridhisha.  

BY ELIUS KAMBILI
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top