Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) |
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Mpwapwa, mkoani
Dodoma, kinapanga kwenda mahakamani kupinga matokeo ya ubunge na udiwani
kwa baadhi ya kata katika majimbo ya Mpwapwa na Kibakwe, kwa madai
kuwa uchaguzi uligubikwa na rushwa na ukiukwaji wa taratibu na sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa Chadema
wilayani humo, Fabian Moke, alisema kutokana na hali hiyo chama hicho
kinajiandaa.
kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo. Alisema kufuatia kasoro hizo,
wagombea wote wa chama hicho katika maeneo hayo waligoma kusaini
matokeo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi. “Tumeitisha
kikao cha dharura cha viongozi ngazi ya wilaya na jimbo ili kueleza
hali hiyo ya sintofahamu kwa wanachama wetu,” alisema Moke.
Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi wilayani humo, Mohamed Maje, alisema
sheria ya uchaguzi haikatazi kutangaza matokeo hata kama mgombea kagoma
kusaini, bali anachotakiwa kufanya mgombea huyo ni kufuata taratibu za
kisheria kutafuta haki yake.
Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, George Lubeleje
(CCM) aliibuka mshindi wa nafasi ya ubunge Jimbo la Mpwapwa kwa kupata
kura 32,208 sawa na asilimia 74.46, huku nafasi ya udiwani CCM ikishinda
kata zote 15.
Kwa upande wa Jimbo la Kibakwe, George Simbachawene (CCM) ambaye pia ni
Waziri wa Nishati na Madini, alitangazwa mshindi wa nafasi hiyo kwa
kupata kura 37,327 sawa na asilimia 81, huku kwenye udiwani CCM
kikishinda viti vyote 18.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment