*Lowassa, Malinzi wammwagia pongezi
NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
SASA ni wazi kuwa siku zinahesabika kwa mshambuliaji wa Tanzania,
Mbwana Samatta kuendelea kubaki kuichezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wakati zikiwa zimesalia siku 53 dirisha dogo la usajili kufunguliwa
barani Ulaya, juzi Samatta alimulikwa na mawakala wengi kutoka barani
humo na hapa Afrika kwenye mchezo wa fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa
Afrika dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Ukiondoa bao alilofunga kwenye fainali hiyo na kumtengenezea lingine
Roger Assale, Samatta pia alifunga bao katika fainali ya kwanza
waliyoshinda mabao 2-1 ugenini, hivyo TP Mazembe imetwaa ubingwa kwa
ushindi wa jumla wa 4-1.
Mbali na Samatta na Thomas Ulimwengu kuandika rekodi ya kuwa
Watanzania wa kwanza kutwaa ubingwa huo na kufika fainali ya michuano
hiyo, Samatta ameweka rekodi nyingine ya kuwa miongoni mwa wafungaji
bora akilingana mabao na Bakri Al-Madina wa El Merreikh wote wakiwa
wamefunga saba.
Samatta pia yumo kwenye orodha ya wachezaji 10 wanaowania uchezaji
bora Afrika kwa wachezaji wa ligi ya ndani, huku akitajwa kupewa nafasi
kubwa ya kutwaa tuzo hiyo kutokana na mafanikio yake binafsi pamoja na
klabu yake.
Akizungumza na MTANZANIA jana Meneja wa straika huyo, Jamal Kisongo,
alisema kuwa wanatarajia kupokea ofa nyingi kutoka Ulaya kwani mawakala
wengi wanaotafuta wachezaji walikuwa uwanjani kumshuhudia Samatta pamoja
na wachezaji wengine kwenye fainali hiyo.
“Vyombo mbalimbali vya Uingereza vimeripoti habari hiyo na kumwelezea
Samatta hivyo tunatarajia kupokea ofa nyingi wiki hii kabla ya
kuangalia mwelekeo wake ujao barani Ulaya pale mkataba wake
utakapomalizika mwakani.
“Lakini tayari tumekubaliana na mmiliki wa TP Mazembe aondoke usajili
wa dirisha dogo Januari mwakani japo anamaliza mkataba Aprili, hivyo
hawezi kukataa kwani ameshakubaliana na hilo na Samatta ataondoka kama
mchezaji huru lakini itakapotokea hali yoyote ya kuzuiwa Januari,
tutaufidia mkataba wake wa miezi mitatu utakaokuwa umebakia kwa
kuuvunja,” alisema.
Kisongo alizungumzia pia mafanikio aliyopata Samatta na kudai kuwa:
“Hayakuja kama ajali, ni kijana mwenye nidhamu, anajitambua na anajua
anafanya nini, hakutanguliza fedha mbele bali malengo, amekataa fedha
nyingi sana za Zamalek ya Misri iliyokuwa ikimtaka, lakini ndoto yake
ilikuwa ni kutaka kuingia kwenye soko Ulaya na sasa inakaribia kutimia.”
Aliongeza kuwa wanachosubiria kwa sasa ni Samatta kutangazwa kuwa
mchezaji bora wa Afrika kama hakutakuwa na siasa kwenye tuzo hiyo
anayoiwania, huku akidai mshambuliaji huyo anatosha kabisa kupewa
heshima hiyo kutokana na mafanikio aliyopata.
Lowassa, Malinzi, Lyon wasifu
Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
Edward Lowassa, naye amempongeza Samatta kwa kuwa Mtanzania wa kwanza
kuwa miongoni mwa wafungaji bora barani Afrika kwa mabao yake saba sawa
na Bakri Al-Madina.
Lowassa ambaye alifuatilia mchezo huo kwa njia ya runinga, alisema
Samatta amedhihirisha kuwa wanasoka wa Tanzania wakiamua kujituma na
kuwa wavumilivu wanaweza kufika mbali.
“Yule kijana na yule mwenzake (Thomas Ulimwengu) ni wavumilivu na
wanajua nini wanatafuta hivyo watafika mbali sana, hii ni fahari kwa
taifa letu, tunao uwezo wa kuwa na kina Samatta wengi zaidi kama
tukiwekeza zaidi kwenye soka,” alisema.
Waziri Mkuu mstaafu huyo alisema ni muhimu sana kwa Serikali kuwekeza katika vyuo vya michezo.
“Moja ya sera za Chadema na Ukawa ni kuondoa ushuru katika vifaa
vyote vya michezo pamoja na kuanzisha shule maalumu za soka (Youth
Academy), ambazo zitasaidia kukuza vipaji na kuwatoa kina Samatta,”
amesisitiza na kuongeza: “Serikali ya CCM isione aibu kuchukua sera hizo
kwa manufaa ya michezo nchini.”
Wakati huo huo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi, amewapongeza Samatta na Ulimwengu kutokana na klabu ya TP
Mazembe kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga USM Alger
ya Algeria katika mchezo wa fainali juzi.
Amewataka washambuliaji hao waongeze juhudi ili waweze kufanya vizuri
na kuisaidia timu yao katika michuano ya Kombe la Dunia la Mabara
itakayofanyika mwezi ujao nchini Japan.
Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya Watanzania wanaopenda soka, Malinzi
aliwataka pia wajitume zaidi kwenye kikosi cha timu ya soka Tanzania
‘Taifa Stars’ katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la
Dunia 2018 nchini Urusi dhidi ya Algeria utakaochezwa Jumamosi hii
katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Naye mmiliki wa timu ya African Lyon zamani Mbagala Market, Rahim
Zamunda, ambako Samatta alianzia soka lake alisema: “Ni jambo la
kujivunia kila Mtanzania kwa mafanikio waliyopata (Samatta na
Ulimwengu), Samatta alikuwa ni mchezaji wetu na ameitangaza vilivyo
klabu yetu kwa uwezo alionao na mafanikio waliyopata yatawasaidia vijana
wengine kujifunza kutoka kwao,” alisema.
Zamunda alisema ili Tanzania ipate wachezaji wengine aina ya Samatta
na Ulimwengu ni lazima uwekezaji mkubwa ufanyike kupata viongozi bora,
uwekezaji wa soka la vijana na ligi bora.
“Lazima tupate viongozi bora watakaoongoza soka, vile vile lazima
tuboreshe ligi yetu iwe bora katika mfumo utakaoendeshwa kibiashara na
yote hayo yatapatikana kwa kuleta wataalamu na si mfumo tunaotumia kwa
sasa,” alisema.
Samatta alianza kulipwa laki moja
Kabla ya Samatta kutua African Lyon zamani Mbagala Market 2008,
alianzia kucheza soka la mchangani katika timu ya mtaani kwake ya
Kimbangulile, iliyopo Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Usajili wake wa kwanza ulikuwa ni pale alipojiunga na timu ya African
Lyon (zamani Mbagala Market) akiichezea katika Ligi Daraja la Kwanza
kabla ya kupanda Ligi Kuu ambapo inaelezwa alikuwa akilipwa mshahara wa
Sh 100,000.
Lakini hivi sasa tangu ajiunge na TP Mazembe mwaka 2011 akitokea
Simba, Samatta analipwa zaidi ya Dola za Marekani 10,000 (zaidi ya Sh
milioni 22 za Kitanzania kwa mwezi).
Kwa mujibu wa mtandao transfermarkt.co.uk, umechambua thamani
aliyonayo Samatta hivi sasa, ambayo inafikia euro 350,000 (zaidi ya
milioni 900 za Kitanzania), lakini hivi karibuni aliwahi kutakiwa na
timu ya Zamalek kwa dau linalofikia euro milioni moja (zaidi ya bilioni
2.3 za Kitanzania).
SOURCE:Mtanzania
Post a Comment