*Akuta makontena 2,431 yametoka bila kulipiwa
ushuru
*Ataka majina yaletwe ofisini leo saa 11 jioni
*Atoa wiki wiki moja kwa mfumo wa malipo
kubadilishwa
*Akagua mabehewa, awaweka kiporo TRL
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara
nyingine ya kushtukiza bandarini na kukagua mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo
na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431
yametolewa bila kulipiwa ushuru.
Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya
ukaguzi wa bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita
bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM
na AZAM.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni watumishi 10 tu
ambao wamesimamishwa kazi kutokana na makosa hayo. “Mmeamua kuwasimamisha kazi
watu wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea
kuikosesha Serikali mapato namna hii,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Bw.
Hebel Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji
kodi huo ifikapo leo saa 11 jioni. Pia amempa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha
kuwa mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye billing
system na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment).
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 3, 2015),
wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi wa
mizigo unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa kwenye chumba cha scanner
mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa diapers
lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya
kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari upande wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Ben Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha scanner,
inapobainika taarifa kama hiyo inapaswa itumwe kwa wenye ICDs ili wafanye
ukaguzi kwa kulifungua kontena ili kuhakikisha mali zilizomo ndizo
zilizoandikishwa kwenye manifest.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amefanya
ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Shirika la Reli (TRL) na kukagua mabehewa
yaliyokuwepo kisha akazungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye
stesheni hiyo ambako alibaini madudu kwenye malipo ya mishahara na makato ya
michango ya wafanyakazi.
Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Mhandisi Elias
Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji
wao kazi lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha sh.
bilioni 13.5/- ili waendeleze miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo.
“Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha
kibiashara lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema.
“Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa sh.
bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika lakini badala ya
kufanya miradi, fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui
mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila
kupata majibu.
Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani hapo
TRL, Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato
yao kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na
malimbikizo ya kuanzia Julai – Novemba 2014.
Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka
Mhandisi Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la Dar
es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi waweze kuwa na
uhuru wa kuchagua aina ya usafiri wautakao.
“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili
watu wenye magari wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja
mjini kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es
Salaam,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
ALHAMISI, DESEMBA 3, 2015.
Post a Comment