Serikali
ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, imeamua kutumia mfumo wa
‘Cash Budget (kutumia kilichokusanywa), huku baadhi ya wachumi wakisema
utaleta nidhamu ya matumizi ya serikali na kubana watumishi ambao
walizoea kutumia vibaya fedha za umma kwa kuzipangia matumizi yasiyo na
tija.
Wizara ya Fedha na Mipango imeieleza Nipashe jana kuwa, mfumo wa
kupanga na kutumia kinachokusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA), ndiyo
ulioamuliwa kutumiwa na serikali ya awamu ya tano.
Itakumbukwa kuwa, tangu Novemba mwaka jana, mapato ya TRA yalipanda
kutoka wastani wa Sh. bilioni 800 na Sh. bilioni 900 kwa mwezi mpaka
Sh. trilioni 1.3, Desemba, mwaka jana Sh. trilioni 1.4, Januari, mwaka
huu Sh. trilioni 1.06 na malengo ya Februari ni kukusanya Sh. 1.03.
Jana Ofisa Habari wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ingiaheddi Mduma,
alisema utaratibu wa kutumia kilichokusanywa utaendelea kutumika kila
mwezi.
Alisema kila makusanyo yatakayopatikana kwa mwezi husika, yatatumika kulingana na mahitaji husika ya mwezi huo.
“ Mahitaji yakiwa mengi katika mwezi husika, basi hata fedha
itakayokusanywa kwa mwezi huo itatumika kulingana na mahitaji hayo,
tutakuwa tunafanya hivyo kila mwezi,” alisema Mduma.
WASOMI WAZUNGUMZA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Wilhelm Ngasamiaku,
alisema mfumo ambao unatumiwa na serikali ya awamu ya tano unajulikana
zaidi kama ‘Cash Budget,’ ambapo mipango na matumizi ya serikali inabidi
ipangwe kutokana na kile
kinachokusanywa.
“Kutumia kile unachokipata hiyo ndiyo ‘Cash Budget’, siyo mara ya
kwanza mfumo huu kutumiwa hapa nchini hata miezi ya mwisho ya serikali
ya awamu ya nne baada ya wahisani kuacha kutoa misaada, ulitumika.
Huu mfumo faida yake unaleta nidhamu ya matumizi ya serikali kwa
hiyo inaifanya itumie na kupanga kutokana na makusanyo yake ya ndani,
ndiyo sifa pekee ya mfumo huo.
“Hasara yake ni kwamba unaposhindwa kukusanya mapato ya kutosha,
matumizi yako mengi uliyopanga kuyafanya utashindwa kuyagharimia na kwa
sababu unatumia unachokusanya ni lazima nguvu nyingi zielekezwe kwenye
kukusanya,” alisema Dk. Ngasamiaku.
Alisema kwa muda mfupi ambao Rais Magufuli ameanza uongozi wake,
suala la makusanyo limeongezeka kuanzia Novemba, Desemba na Januari,
ingawa fedha za nyuma ambazo hazikukusanywa zimesaidia ongezeko hilo.
Alisema kuongeza zaidi mapato kutawezekana endapo biashara nyingi
za wajasiariamali wadogo na wa kati zitatozwa kodi, jambo ambalo sasa
hivi halifanywi kwa ufasaha.
Kuhusu matumizi kadhaa aliyofayanya ikiwa ni pamoja na kukata fedha
za sherehe za uhuru na za wabunge, alisema hatua hiyo ilichukuliwa kwa
kuwa aliingia madarakani bajeti ya mwaka 2015/16 ikiwa imeshapita.
“Ikumbukwe alipoingia madarakani bajeti ilishasomwa, kwa hiyo hivi
vitu ambavyo siyo lazima kama hizo sherehe za uhuru, za wabunge, semina
elekezi fedha zilikuwa zimeshatengwa kwa shughuli hiyo, akaona ni vyema
kupeleka kwenye masuala muhimu zaidi,” alisema na kuongeza:
“Hiyo ilikuwa ni re-allocation tu ya kawaida na kwa sababu
makusanyo ni makubwa anayatumia kutekeleza baadhi ya ahadi zake ambazo
hazikuwa kwenye bajeti,” alisema.
Mhadhiri wa UDSM na mtaalam wa uchumi, Dk. Haji Semboja, alisema
anachofanya Rais Magufuli sasa kiliwahi kufanywa na marais
waliomtangulia.
Alisema tofauti yake na marais hao ni kuwa, Rais Magufuli anatumia
kutokana na kile alichokikusanya, tofauti na watangulizi wake waliokuwa
wanatumia kutoka katika kile walichokopa.
“Unashona nguo kulingana na ukubwa wa kitambaa chako, mfumo huu ni
mzuri kwa kuwa anatumia kutoka kile alichokusanya na nchi haitakuwa na
deni kubwa miaka ya mbele,” alisema.
Dk. Semboja alisema mfumo wa kutumia fedha katika sekta mbalimbali
ni mzuri kwa sababu, mtu anatakiwa kutumia kulingana na kile
alichonacho na siyo asichonacho.
Naye Mkuu wa Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk. Jehovaness Aikaeli, alisema ni utaratibu mzuri ulionzishwa
kwa kuwa unasaidia kuziba mashimo yaliyokuwapo tangu awali.
Alisema haina haja kwa serikali kuweka akiba wakati wananchi bado
wanahitaji kupata mahitaji muhimu kama vile dawa hospitalini na madawati
katika shule.
“Haina haja ya kuweka akiba, kama vile alivyofanya fedha za
sherehe za uhuru zielekezwe katika ujenzi wa barabara ni sahihi,
utaratibu huu uendelee na usiishie njiani,” alisema.
Dk. Aikaeli alisema katika nchi yoyote duniani kanuni kubwa ni
kutegemea kodi katika kuendeshea nchi, hivyo Rais Magufuli anatakiwa
kuendelea kuziba mianya ya upotevu wa kodi.
Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) cha Dar es Salaam,
Dk. Bill Kiwia, alisema ni mfumo mzuri aliouanzisha Rais John Magufuli
katika kuinua uchumi wa nchi.
Hata hivyo, alisema serikali inapaswa kutotegemea makusanyo ya kodi
pekee katika bajeti yake, bali iangalie vyanzo vingine vya mapato,
kwani kwa kutokufanya hivyo kutaua sekta binafsi.
Alisema serikali pia inapaswa kuangalia makusanyo katika vitalu vya madini na gesi, ushuru na tozo.
Alisema pia serikali inaweza kutumia njia ya kukopa fedha kutoka mataifa ya nje na kuzielekeza katika sekta za maendeleo.
“Serikali isitegemee sana makusanyo ya kodi katika kutekelezea
bajeti yake, inaweza kuangalia vyanzo vingine vya mapato, lakini ni
mfumo mzuri aliouanzisha Rais, utasaidia kukuza uchumi wa nchi,” alisema
Dk. Kiwia.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya Julai, 2015, uwiano wa wigo wa kodi ni asilimia 12.
Alisema Tanzania inahitaji kukusanya kodi zaidi ili iweze kulipia
gharama mbalimbali za uendeshaji serikali na kwamba kupungua kwa misaada
na vikwazo katika mikopo ndio kunapelekea umuhimu wa kukusanya kodi
zaidi.
Alisemal akini ni muhimu ukusanyaji huo wa kodi usidhoofishe sekta binafsi.
Akizungumzia operesheni ya kukusanya kodi inayoendeshwa na TRA,
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma wa mamlaka hiyo, Richard Kayombo,
alisema lengo lake ni kusajili wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa na
kukagua ambao wanapaswa kutumia mashine za EFDs lakini hawazitumii.
Alisema operesheni hiyo ni ya kawaida na inafanyika nchi nzima na
kuwa wale ambao watakutwa wanafanyabiashara bila kusajiliwa watawashauri
kufanya hivyo ili kukidhi matakwa ya sheria.
MAKUSANYO YA SERIKALI
Desemba mwaka jana, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya Sh.
trilioni 1.3 Novemba na Desemba makusanyo hayo yalipanda na kufikia Sh.
trilioni 1.4, huku sehemu ya fedha za miezi hiyo pamoja na mambo
mengine zikitumika kuanzisha mpango wa elimu bure.
Januari kiasi hicho kilishuka mpaka Sh. trilioni 1.06 na malngo ya Februari ni Sh. 1.03.
MATUMIZI YA FEBRUARI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, alieleza
kuwa kwa Februari, mwaka huu, serikali imeweza kutumia zaidi ya Sh.
trilioni moja katika miradi na sekta mbalimbali.
Baadhi ya sehemu ya fedha hizo, Sh. bilioni 18.7 zimepekwa
kutekeleza mpango wa elimu bure, Sh.bilioni 1.65 mafunzo kwa vitendo
katika vyuo 35, Sh. milioni 29.1 kununulia vifaa, Sh. milioni 1.49
zilitumika kulipa posho, Sh. milioni 402.1 zilitumika kulipia posho kwa
wanafunzi.
Pia Sh. bilioni 573.2 zilitumika kulipa mishahara kwa watumishi wa
umma, Sh. bilioni 842.1 zililipa deni la taifa, Sh. bilioni 81.23 kulipa
deni la mifuko ya hifadhi ya jamii, Sh. bilioni 166.1 zilitumika katika
miradi ya maendeleo, Sh. bilioni 2.078 zilipelekwa Mamlaka ya Elimu
Tanzania (TEA).
Sh. bilioni 7.115 katika sekta ya maji na Sh. bilioni 58.168 sekta
ya barabara, Sh. bilioni 40.73 sekta ya ujenzi na Sh. bilioni 16.46
zilipelekwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sh. bilioni
20.1 sekta ya umeme, Sh. bilioni 2.034 sekta ya reli na Sh. bilioni
12.3 sekta ya mahakama.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment