Mwenyekiti Freeman Mbowe akisalimiana na viongozi mbalimbali wa CHADEMA mkoa wa Mwanza waliofika kumlaki uwanja wa ndege
.....................
Na Fredrick Katulanda, Mwanza
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, amevunja ukimya na kusema atawasilisha jina makini la mrithi wa
nafasi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, baada ya kumalizika kikao
cha kwanza cha Kamati Kuu, Mbowe alisema sifa za kiongozi anayepaswa
kushika wadhifa huo zinafahamika.
Alisema wajumbe na wanachama wa Chadema watarajie kumpokea mtu makini
ambaye jina lake atalipendekeza kisha kupigiwa kura na wajumbe wa
Baraza Kuu kesho.
“Sifa za Katibu Mkuu zinajulikana, nawaomba wanachama na wajumbe
kutulia, jina watakutana nalo ukumbuni muda ukifika… nina imani litakuwa
jina la mtu makini,” alisema.
Mbowe alisema chama hicho kinakutana kwa mara ya kwanza tangu
kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais mwaka jana, hivyo wana mambo mengi
ya kujadili, ikiwa ni pamoja na kupanga mikakati mipya ya kuwafikia
wafuasi wao.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema kitamtambulisha Katibu
Mkuu mpya rasmi Jumapili wakati wa mkutano wa hadhara utakaofanyika
viwanja wa Furahisha jijini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa chama hicho,
Tumaini Makene, alisema majina mawili yatawasilishwa katika Baraza Kuu
litakalokaa usiku wa Jumamosi kwa ajili ya kupitisha jina moja.
Alisema majina yatakayowasilishwa hayatakuwa na uhusiano au urafiki wowote na Mwenyekiti Mbowe.
“Tayari viongozi wa kitaifa wamewasili Mwanza, Sekretarieti imekutana
kwa ajili ya kuandaa ajenda ambazo zitajadiliwa na Kamati Kuu yenye
wajumbe 36.
“Siku inayofuata Baraza Kuu litakaa usiku kwa ajili kumpata Katibu
Mkuu, hii ni nafasi nyeti sana ndiyo maana hata wenzetu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wanafuatilia kwa ukaribu kujua nani atapewa mikoba ya
Dk. Willibrod Slaa.
CHANZO:MTANZANIA
Post a Comment