Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye akikabidhi Ipad
tano kwa mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw.Jackson Msome kwa ajili ya matumizi ya
maafisa habari wa mkoa wa Kagera. Bwana Msome alikuwa akimwakilisha Mkuu wa
mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Mustafa kijuu.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Sekta
ya habari ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya wananchi na serikali
yao. Ndiyo maana wanazuoni hupenda kusema kuwa habari ni muhimili wa nne
wa dola. Kwa kuzingatia umuhimu huo, katika kuchekecha huku na huko,
Mhe. Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli akamteua mtu mahiri kuongoza sekta hii, Mhe. Nape Moses
Nnauye.
Kwa
uteuzi huu ninadiriki kusema hatimaye Wizara imepata mtu sahihi na
mchapakazi anayeweza kwenda na kasi ya Mheshimiwa Rais Magufuli na ni
dhahiri kabisa kuwa kumpa Mhe. Nape ni kuthibitisha usemi wa wahenga
usemao upele umepata mkunaji.
Kwa
jinsi hii tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa
Mbingu na Nchi kwa kutujalia kupata kiongozi wa nchi ambaye ni
mchapakazi na aliyejaliwa kipawa cha kuona mbali kwa kuwaweka viongozi
wa chini yake katika nafasi za uongozi wanazostahili.
Sekta
ya habari ni sekta nyeti na muhimu sana katika dunia hii kwa kua bila
kupashana habari na kujua kinachoendelea daima hakutakua na maendeleo
kwa hiyo, ni sekta inayohitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu ili
kuhakikisha kwamba inachukuliwa uzito na inapewa kipaumbele kwa kupewa
vifaa na elimu ya kutosha ili kuepusha upotoshaji na kukosekana kwa
habari muhimu hasa za Serikali zinazotakiwa kuwafikia wananchi kwa muda
husika.
Tukiangalia
katika sekta ya habari, Mhe.Rais hakukosea kabisa kumuweka Waziri Mhe.
Nape kwa kuwa ameanza kuitumikia Wizara kwa kasi nzuri na ameonyesha nia
ya kuiboresha Wizara hasa kwa tasnia ya habari kwa kuanzia kwenye
wizara yake hadi katika ofisi za umma zilizoko mikoani ili kuhakikisha
wanahabari wote nchini wanatambua thamani ya kazi yao.
Kwa
maneno yake aliyoyatoa Jijini Mbeya alipokua akigawa vitendea kazi vya
kisasa kwa ajili ya mawasiliano yaani ipad kwa maafisa mawasiliano wa
mkoa huo alikaririwa akisema,"Nataka Wizara ihamie mikoani" hii
haimaanishi kuwa Wizara ihamie mikoani kama alivyosema bali alimaanisha
kiutendaji zaidi kuwa yale yote anayoyafanya katika Wizara yake
atahakikisha na maafisa wa mikoani pia wanafanyiwa hivyo ikiwemo
kugawiwa vitendea kazi pamoja na mambo mengine.
Katika
kuhakikisha hilo, kwa upande wa sekta ya habari, Waziri Nape ameanza
kwa kugawa ipad kwa maafisa mawasiliano walioko mikoa ya pembezoni
ambao wana upungufu mkubwa wa vitendea kazi na kwa muda mrefu
wameshindwa kuifanya kazi yao kwa ufanisi kwa sababu ya uhaba wa vifaa
vya kufanyia kazi hiyo.
Ipad
hizo zilizotolewa kama msaada kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo na kampuni ya Startimes ambayo imeahidi kuwa bega kwa bega na
Wizara hii katika kuisaidia ili kuongeza ufanisi hasa katika sekta hii
nyeti ya habari maana kwa maneno mengine tunaweza kusema sekta ya habari
ndio daraja linalounganisha serikali na wananchi.
Siku
aliyokabidhiwa ipad hizo Mhe. Nape alikaririwa akisema "Nawashukuru sana
Startimes kwa kutujali,ipad hizi tutaanza kuzigawa kwa maafisa habari
wa mikoa ya pembezoni kwa kuwa ndiko kuna uhaba mkubwa sana wa vifaa kwa
maafisa hao"alisema Mhe Nape.
Maneno
haya ya Mhe.Nape yanaungana na usemi wake wa kuifanya Wizara kuhamia
mikoani kwa maana ya kuwapa kipaumbele katika kuwapatia vitendea kazi
ili nao wasijione kuwa wametengwa au kutokuthaminiwa kama maafisa
mawasiliano wengine hasa walioko Dar es salaam na mikoa mingine
iiliyoendelea. Maana anaamini kuwa mikoani ndiko kuna wadau na ndiko
ziliko shughuli nyingi kwa kuwa watu wengi wenye uwezo wa kuzikuza
tasnia anazozifuatilia wapo mikoani.
Ni
mengi sana Mhe.Nape ameyaongea hasa kwenye ziara zake alizozifanya
kwenye baadhi ya mikoa kama Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Geita,
Simiyu,Dodoma, Kagera pamoja na Mwanza ambako alipita kugawa ipad na
kuangalia jinsi maafisa habari wanavyofanya kazi katika vituo vyao vya
kazi. Ziara hiyo pia inalenga katika kujua changamoto wanazokumbana
nazo ili kuweza kufanya kila kinachowezekana kuzitatua ili kufanya sekta
hii kufanya kazi ya kupeleka taarifa kwa wananchi kama inavyopaswa
kufanyika ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa
na Jemedari Mkuu Mhe. Rais John Pombe Magufuli.
Kiongozi
huyu ameongelea kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari
ambao ulishirikisha wadau mbali mbali hasa wahariri pamoja na wamiliki
wa vyombo vya habari kutoa maoni yao ambayo kwa asilimia 99 maoni hayo
yamewekwa katika muswada huo.
"Muswada
huo umeshakamilika, uko tayari kufikishwa bungeni, pia nataka
niwathibitishie kuwa muswada huo utalinda maslahi ya waandishi wa habari
kuanzia mishahara yao, mikataba ya kazi zao pamoja na bima ya matatizo
wanayoyapata kwenye kazi zao lakini muswada huo utakua na sheria
zitakazobana ufundishwaji wa masomo ya habari ili tupate waandishi ambao
wamebobea katika fani hiyo" alisema Mhe. Nape.
Ndoto
ya changamoto zinazoikabili tasnia ya habari mikoani zinakaribia kuwa
historia kwa kuwa Waziri Nape amepanga kuleta teknolojia mpya na kuzitoa
zile zilizopitwa na wakati ili kuharakisha ufanisi wa utoaji wa
taarifa, kuweka busta kwa baadhi ya maeneo ili televisheni ya taifa
(TBC) iwe bora zaidi na kuongeza urefu wa minara ili matangazo yafike
mbali zaidi.
Waziri
Nape ameamua kuboresha urefu wa minara ili matangazo yafike mbali kwani
mikoa mingi ya pembezoni imepakana na nchi ambazo teknolojia zao za
mawasiliano ni kubwa kiasi kwamba wananchi wengi wa mipakani
wanasikiliza redio za nchi jirani na kuacha kusikiliza redio za hapa
nyumbani Tanzania.
Katika
harakati za kuboresha tasnia ya habari, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe.
Amos Makalla ameelezea changamoto na jinsi alivyopanga mikakati ya
kusaidia na kuiboresha tasnia hii mkoani kwake ambapo alikaririwa
akisema "Mkoa wangu unaomba kibali cha kuajiri maafisa habari ili kila
Halmashauri iwe na afisa habari wake pia naahidi kuendelea kutenga
bajeti kwa ajili ya kununua vitendea kazi vya maafisa hao".
Wakati
huo huo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa wito kwa
wananchi kuanzisha vituo vya utangazaji 19 katika Wilaya na Halmashauri
mbalimbali na wamewaomba wadau kutuma maombi kabla ya Aprili 29 mwaka
huu.
Akiongea
katika mkutano wa Mhe.Nape na wadau wake, Meneja wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Lilian Mwangoka
alisema, "Mamlaka ya Mawasiliano ipo tayari kushirikiana na wananchi
kuongeza vituo vya utangazaji ili kuongeza idadi ya vituo na kuongeza
fursa katika ukusanyaji wa kodi".
Aidha,
Waziri Nape amesisitiza suala la maafisa habari kupewa ruhusa ya
kushiriki katika vikao vya maamuzi ili wajue mambo yanayoendelea katika
ofisi zao kwani kufanya hivi kutasaidia maafisa habari kuacha kuwakimbia
waandishi wa habari na badala yake kuwapa taarifa kamili ili
wakawajulishe wananchi taarifa sahihi kuhusu Serikali yao.
Akiongea
kwa kujiamini Waziri Nape amehakikisha kuwa yote yatawezekana maana
fedha za kutatua kero hizo zitapatikana kwa kuwa Mhe.Rais tayari
alifanya maamuzi ya kuziamuru taasisi zote za Serikali zilizopewa huduma
ya kutoa matangazo yao kupitia Televisheni ya Taifa bila kulipa waanze
kulipa madeni yao mara moja kwa hiyo fedha hizo ndizo hasa zitatumika
katika kuboresha tasnia hii.
Sasa
ni wakati wa maafisa habari pamoja na waandishi wa habari wote nchini
kuunga mkono jitihada za waziri wetu kwa kufanya kazi za kukusanya na
kutawanya taarifa kwa ufanisi na usahihi wa hali ya juu ili kuifanya
jamii ielewe umuhimu wetu pamoja na kukuza uchumi wa nchi kupitia
taarifa tunazozitoa kwenye vyombo vya habari.
Wahenga
wanasema Taifa lisilo na taarifa haliwezi kukua kiuchumi, litadumaa.
Hivyo tumuunge mkono Mzalendo huyu ili kukuza na kuinua Tasnia ya Habari
na ionekane kweli kuwa muhimili wanne wa dola ambao unachangia kwa
kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo.
Post a Comment