Muuza maji (kushoto) akishangaa gari alilopanda Rais Magufuli leo asubuhi wakati akitoka Benki ya CRDB tawi la Holland.
Gari
alilokuwa amepanda Rais John Magufuli lenye namba za usaji T 182 DGQ
likitoka katika benki ya CRDB tawi la Holland lililopo katika makutano
ya barabara ya Samora na Ohio jijini Dar es Salaam.
Rais
John Magufuli akiwa ndani ya gari lenye namba za usajili T182 DFQ huku
akiwapungia mkono watu waliokuwa nje ya Benki ya CRDB tawi la Holland
jijini Dar es Salaam jana, wakati akitoka katika benki hiyo. (Picha na
Francis Dande)
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amezua
taharuki mjini leo baada ya kufika katika Tawi la CRDB (Holland Branch),
akiwa kwenye gari binafsi lenye namba T 182 DFQ huku likiwa halina
nembo ya adamu na hawa wala bendera.
Tukio
hilo lililochukuwa takribani dakika 25, limetokea majira ya saa nne
asubuhi ya leo jijini Dar es Salaam katika tawi la benki hiyo ambalo
liko katika makutano ya Barabara ya Ohio na Samora bila kutarajiwa.
Mara
baada ya Rais Magufuli kufika katika eneo liliko tawi hilo makutano ya
barabara hizo yalifungwa huku ndipo rais aliposhuka kwenye gari na
kuingia ndani ya benki hiyo.
Wakati
akikaribia kuingia ndani ilibidi baadhi ya wateja waliokuwa wakijiandaa
kuingia ndani ya benki hiyo ilibidi wazuiwe kuingia huku huduma
ikiendelea tu kwa wale ambao waliokwisha ingia.
Aidha,
baada ya kuingia ndani baadhi ya wateja wa tawi hilo na wananchi
wengine walibaki wakishangaa huku wengine wakijiuliza imekuwaje Rais
kuingia benki kwa staili ile kwani baadhi ya wananchi kudai kuwa
hawajaona tukio kama lile kwa marais wote waliopita.
James
Charles, ambaye ni dereva wa Texi, alisema baadhi ya wananchi waliokuwa
kwenye eneo hilo baada ya kuona ulinzi unaimalishwa walishtuka huku
wasijue ni nini kinaendelea, hadi pale walipomuona Rais Magufuli
akishuka kwenye gari hali iliyowafanya wafikirie anakwenda kutembelea
ofisi yake ya zamani.
“Lakini
kufumba na kufumbua tukamuona anaelekea kwenye benki ya CRDB
tukajiuliza vipi rais leo kaamua kuwa kama mteja hata hivyo hatujui kama
hiyo ilikuwa inawezekana. Lazima kutakuwa na kitu haiwezekani aende
akachukue fedha kwa utaratibu ule ngoja tusubiri tutasikia amefuata
nini,” alisema Charles.
Joyce
Godwin ambaye ni mwanafunzi wa chuo kimojawapo cha elimu ya juu,
alisema kuja kwake kumewashtua wafanyakazi wa tawi la benki hiyo kwani
walidhani alikwenda pale kwa ajili ya kutumbua majipu.
“Mimi
wakati Rais Magufuli anaingia nilikuwepo ndani kwenye foleni nikisubiri
huduma kwa ujumla kila mmoja wetu alishtuka lakini hatukujua
kilichomleta,”alisema.
Baada ya Rais Magufuli kumaliza kazi yake iliyompeleka alitoka na kuingia kwenye gari huku akiwapungia mkono wananchi.
Post a Comment