ARUSHA, TANZANIA
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha kimesema, kimefanikiwa
kukamilisha uchaguzi wake wa Chama na Jumuiya katika ngazi za
mashina,matawi na kata kwa asilimia 90 kwa mkoa mzima.
Katibu wa siasa na uenezi wa mkoa huo, Loota Sanare alisema hayo leo
alipokua akizungumza na vyombo vya habari ili kuelezea mafanikio
yaliyopatikana katika uchaguzi huo ambao umeonyesha kuungwa mkono na
vijana walio wengi.
Alisema asilimia 10 za matawi,mashina na kata ambazo hazijafanya
uchaguzi wake zimetokana na malalamiko mbalimbali ya wanachama
waliogombea kwa madai tofauti yakiwemo ya kuchezewa rafu kwa majina yao
kukatwa.
Alisema hata hivyo chama kimeshaagiza nafasi hizo kujazwa mara moja kwa
kufanyiwa marekebisho ya makosa mbalimbali yaliyojitokeza katika
uchaguzi huo ili kuwezesha kupatikana kwa viongozi halali kupitia
chaguzi hizo.
Sanare alisema katika chaguzi za ngazi za wilaya na mikoa nafasi
zinazowaniwa ni uenyekiti,wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya,mjumbe wa
halmashauri kuu ya taifa,mwenezi na mchumi wa wilaya,wajumbe wa mkutano
mkuu taifa na wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa.
Alisema zoezi la uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi hizo limeanza leo
Agosti 22 na litakamilika Agosti 29 ambapo aliwataka wanachama wote wa
CCM wenye sifa za kuwania nafasi hizo kujitokeza kwa wingi kuwania
nafasi hizo.
Aidha Sanare alizungumzia kinyang’anyiro cha chaguzi ndogo mbili za
udiwani katika kata ya Daraja mbili jijini Arusha na Bang’ata wilayani
Arumeru ambapo tayari zoezi la kupatikana kwa wagombea ndani ya chama
limeshaanza.
Akizungumzia kata ya Daraja mbili Sanare alisema mgombea ameshapatikana
Philipo Mushi kupitia vikao mbalimbali vya chama ambapo wagombea
walijitokeza watatu kuchukua fomu lakini ni mmoja tu ndiye aliyerejesha
hali ambayo inampa nafasi ya moja kwa moja kuwa mgombea kwakua wenzake
wote wanamuunga mkono.
Kuhusu kata ya Bang’ata alisema mchakato uko ndani ya vikao kwaajili ya
kujadiliwa kwa majina matatu yaliyopo ili kupatikana jina moja kupitia
kamati ya siasa ya wilaya inayokutana kesho ili kupitisha jina hilo.
Alitaja majina matatu yanayojadiliwa kuwa ni Ezekiel Mollel,David Mollel
na Olais Mfele ambapo mgombea atajulikana kupitia kikao hicho cha
kamati ya siasa ya wilaya inayokutana kesho.
Loading...
Chediel . Powered by Blogger.
Post a Comment