Marehemu Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Meles Zenawi,
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
asubuhi ya jana, Jumanne, Agosti 21, 2012, amepokea kwa mshtuko mkubwa,
masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Waziri Mkuu wa Ethiopia,
Mheshimiwa Meles Zenawi, kilichotokea jana usiku nje ya nchi ambako
alikuwa anatibiwa.
Kufuatia
taarifa hizo, Mheshimiwa Rais Kikwete, kwa niaba ya wananchi wa
Tanzania, Serikali yake na kwa niaba yake mwenyewe amemtumia salamu za
rambirambi Rais wa Ethiopia, Mheshimiwa Girma Wolde-Giorgis.
Katika rambirambi zake kwa Mheshimiwa Wolde-Georgis, Rais Kikwete amesema: “Tanzania
imepokea kwa mshtuko mkubwa, masikitiko na huzuni nyingi taarifa za
kifo cha Mheshimiwa Meles Zenawi kilichotokea jana usiku.”
Amesema Rais Kikwete: “Kwa
niaba ya wananchi wa Tanzania, Serikali yangu na mimi mwenyewe, natuma
salamu zangu za dhati za rambirambi kwako, kwa wananchi wa Ethiopia na
kupitia kwako kwa Mheshimiwa Azeb Mesfin, mjane wa marehemu na familia
nzima ya Mheshimiwa Meles Zenawi. Tupo nanyi katika msiba huu mkubwa.”
“Kwa hakika, Ethiopia imempoteza kiongozi hodari, mwana mapinduzi na mpenda maendeleo. Kwa hakika, Afrika
imempoteza kiongozi wa kutumainiwa na msemaji hodari sana wa Bara letu.
Daima tutamkumbuka Waziri Mkuu Zenawi kwa msimamo wake thabiti wa
kutetea maslahi ya Afrika na ustawi wa watu wake. Mimi na Tanzania
tumempoteza rafiki wa kweli” amesema Rais Kikwete na kusisitiza, “hakika tutaukosa mchango wake uliojaa busara, hoja zake za kusisimua na zenye mantiki sana.”
Rais Kikwete amemaliza kwa kuwaeleza wananchi wa Ethiopia: “Tunaungana
nanyi katika wakati huu mgumu wa majonzi na tunamwomba Mwenyeji Mungu
awape nguvu, moyo, subira na baraka zake ili muweze kuvuka kipindi hiki.
Aidha, tunaungana nanyi na familia ya Marehemu Zenawi kumwomba Mola
ampe mapumziko mema Marehemu Meles Zenawi.”
Waziri
Mkuu Zenawi ambaye ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 57 amekuwa
Waziri Mkuu wa Ethiopia tokea 1995 na kabla ya hapo alikuwa Rais wa nchi
hiyo kati ya 1991 na 1995.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Agosti, 2012
Post a Comment