Release No. 135
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MICHUANO YA KOMBE LA TAIFA 2012
Michuano
ya Kombe la Taifa (Taifa Cup) inayoshirikisha kombaini za mikoa ya
Tanzania Bara haitakuwepo mwaka huu kutokana na kukosekana kwa udhamini.
Licha
ya kukosekana kwa udhamini, awali tulifikiria kuendesha mashindano hayo
kwa michango ya wanachama wetu (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa) na
Serikali za mikoa kugharamia timu zao.
Lakini
baadhi ya wanachama wetu na Serikali za mikoa walitushauri kuwa ni
ngumu kuendesha mashindano hayo kwa sasa kutokana na shughuli za kitaifa
zinazoendelea hivi sasa ikiwemo maandalizi ya sensa ya watu na makazi.
Kwa mujibu wa Kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), mashindano ya Kombe la Taifa yalitakiwa kufanyika
kuanzia Julai 23 hadi Agosti 6 mwaka huu.
Michuano
ya Kombe la Taifa msimu uliopita ilidhaminiwa na Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambapo Mbeya
iliibuka mabingwa katika fainali iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
WACHEZAJI 11 KUTOKA NJE WAPATA ITC
Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea Hati ya
Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wachezaji 11 wa nje kati ya 14
walioombea usajili na klabu mbalimbali za Ligi Kuu.
Wachezaji
walioombewa usajili Yanga na tayari ITC zao zimepatikana ni Nizar
Khalfan kutoka Vancouver Whitecaps ya Canada, Didier Kavumbagu (Atletico
Olympic- Burundi) na Mbuyu Twite kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Kwa
upande wa Simba ni Musa Mude (Sofapaka, Kenya) na Daniel Akuffor
(Stella Abidjan, Ivory Coast) wakati Mtibwa Sugar ni Shabani Kisiga timu
ya El Itihad ya Oman.
Waliopata
ITC kwa upande wa Kagera Sugar ni Wilfred Ojodale Ame na Benjamin Efe
Ofuyah wote kutoka FC Abuja ya Nigeria. Wengine ni Deangelis Silva
kutoka New Road ya Nepal kwenda Coastal Union, George Odhiambo kutoka
Randers FC ya Denmark kwenda Mtibwa Sugar na Jerry Santo kutoka Tusker,
Kenya kwenda Coastal Union.
Wachezaji
ambao wameombewa usajili na ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje
na Pascal Ochieng wa AFC Leopards, Kenya kwenda Simba na Ayoub Hassan
Isiko kutoka Bull FC, Uganda kwenda Mtibwa Sugar. Bado klabu ambazo
hazijakamilisha usajili na kupata ITC zina fursa ya kufanya hivyo hadi
Septemba 4 mwaka huu ambapo dirisha litafungwa.
Pia
TFF imetoa ITC kwa wachezaji wanane walioombewa kwenda kucheza mpira wa
miguu katika nchi za Kenya na Msumbiji kutoka katika klabu mbalimbali
za hapa nchini. Wachezaji hao na klabu wanazokwenda katika mabano ni
Abdallah Ally Abdallah (CD Madchegde, Msumbiji), Almasi Khatib Mkinda
(Ferroviario da Beira, Msumbiji), David Naftali (Bandari, Kenya) na
Hassan Hassan Mustafa (CD Madchegde, Msumbiji).
Wengine
ni Meshack Abel (Bandari, Mombasa), Mohamed Banka (Bandari, Kenya),
Thobias Davis Silas (CD Madchegde, Msumbiji) na Thomas Maurice (Bandari,
Kenya).
VIPIMO VYA TIBA KWA WACHEZAJI
Klabu
zote zilizowasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) maombi
ya usajili kwa wachezaji wao zinatakiwa pia kuwasilisha nakala za hati
zao za vipimo vya afya (medical certificate) kwa mujibu wa kanuni za
usajili.
Boniface Wambura Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Post a Comment