Evarist Chahali
---
“TUMEROGWA na aliyeturoga naye karogwa, kisha kafariki.”
“Hapana, hatujarogwa ila nadhani bongo zetu zimefungwa, na funguo zimetumbukia chooni.”
Hizo ni
baadhi ya kauli zinazoanza kuzoeleka masikioni mwa Watanzania wanapojadili mustakabali wa nchi.
Ukisikia
kauli hizo unaweza kuishia kucheka kwa kuzitafsiri kuwa ni utani tu.
Lakini ukichukua muda kuzitafakari, unaweza kujikuta unaungana kimtizamo
na watu hao.Hivi
katika mazingira ya kawaida unawezaje kuelezea ‘busara’ za Kamati ya
Olimpiki kujaza viongozi wengi zaidi wa wanamichezo kwenye msafara wa
wawakilishi wetu kwenye mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto
yaliyomalizika juzi jijini London, hapa Uingereza?
Wakati
wenzetu Wakenya wakirejea na medali kadhaa huku Waganda wakijivunia
medali ya dhahabu, sisi tumeendelea kupigilia mstari ‘sifa’ yetu ya kuwa
kichwa cha
mwendawazimu.Lakini
ukidhani uhuni huo katika ushiriki wetu kwenye Olimpiki unachefua, basi
sikiliza hii ‘kali kubwa’ kutoka kwa Bunge letu tunaloliita ‘tukufu.’
Wiki iliyopita, Naibu Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai aliwaeleza Watanzania kuwa
baadhi ya wawakilishi wao bungeni (wabunge) wamekuwa wakiingia kwenye
vikao vya chombo hicho cha kutunga sheria wakiwa wamelewa pombe na
sigara zisizo za kawaida.
Kabla
hatujaenda mbali kujadili taarifa hii ya kuogofya ni vema
tukakumbushana kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya hivi karibuni,
waheshimiwa wabunge wanalipwa shilingi milioni 11 kwa mwezi. Ni muhimu
kutaja kiwango hicho ili tunapowajadili watu hawa tuwe na uelewa kuwa
pamoja na umasikini wa nchi yetu tumejikamua na kuwapatia waheshimiwa
hawa maslahi manono kabisa.
Kwa
namna fulani ninampongeza Naibu Spika Ndugai kwa kutufungua macho
kuhusu swali ambalo ninadhani wananchi wengi wamekuwa wakijiuliza,
“kwanini baadhi ya waheshimiwa huonekana wamelala bungeni huku kikao
kinaendelea?”
Mitandaoni
kumejaa picha za ‘wachapa usingizi bungeni’ na kuna waheshimiwa wengi
tu wanaopenda kuligeuza Bunge kuwa sehemu ya kulala.
Baadhi
yetu tulipoona picha za aina hiyo tulijaribu kujipa matumaini kuwa
labda waheshimiwa hao wanazidiwa na usingizi kwa vile ‘wanakesha
wakitafakari jinsi ya kuwatumikia wapigakura wao, na pengine nchi kwa
ujumla, kwa ufanisi mkubwa zaidi.’
Kadhalika,
kauli ya Ndugai imetusaidia pia kutupa mwanga kuhusu michango ya baadhi
ya wabunge ambayo mwananchi hawezi kulaumiwa akihisi mchangiaji
anatafuta nafasi ya ushiriki wa Bongo Star Search kwa
kipaji cha mipasho. Inakera lakini ndio ukweli wenyewe, baadhi ya
waheshimiwa hutumia fursa ya kuchangia hoja kuonyesha umahiri wao wa
kukebehi, kudhihaki na hata kutusi.
Lakini kilichonikera katika maelezo ya Ndugai ni
‘utetezi wa kitoto’ kuwa, (ninamnukuu) “Wabunge
ni watu kama watu wengine, wana tabia kama walivyo wanadamu wengine,
wapo ambao kwa namna ninavyohisi wanaingia bungeni hasa vikao vya
kuanzia mchana wakiwa wamepiga bia.”
Kwanza,
wabunge wetu si sawa na ‘watu wengine.’ Ni ‘watu wengine’ wangapi
wanaitwa ‘waheshimiwa’? Na ni wangapi wanaolipwa posho kwa kutimiza
wajibu wao (licha ya kulipwa mshahara kwa nyadhifa zao)? Na ni ‘watu
wengine’ wangapi wanaolipwa mishahara minono japo kwa kiasi kikubwa
ufanisi wao upo zaidi kwenye mipasho, kukashifiana na porojo nyingine
zisizomsaidia Mtanzania?
Ndugai
hayupo sahihi kudai kuwa wabunge wanaoingia bungeni wamelewa ‘wana
tabia kama walivyo binadamu wengine.’ Mimi
kama mwanafunzi siruhusiwi kuingia darasani nikiwa nimelewa. Hata
kwenye sehemu za vinywaji ‘baamedi’ haruhusiwi kuingia kazini amelewa.
Sasa hao ‘binadamu kama wengine’ anaotueleza Naibu Spika wametoka sayari
gani?
Halafu
cha kuchukiza zaidi ni ukweli kwamba Naibu Spika anafahamu kuwa kuna
wabunge wanaingia kwenye vikao vya Bunge wakiwa wamelewa lakini hachukui
hatua zozote bali anasubiri hadi apate nafasi ya kumwaga jambo hilo
kwenye mahojiano na kituo cha runinga.
Huyu
ni kiongozi dhaifu. Japo tunaweza kumpongeza kwa ‘kutuibia siri ya
yanayojiri bungeni’ lakini dhamana aliyokabidhiwa si kunyooshea watu
vidole (kwa maana ya kubainisha kuna wabunge walevi) bali kuchukua hatua
stahili dhidi ya ‘wahalifu’ hao.
Na
si kama nimetumia neno ‘wahalifu’ kwa bahati mbaya. La hasha. Mtu
anayelipwa shilingi milioni 11 kama mshahara wa kumwakilisha mwananchi,
kisha akaamua kufanya uwakilishi huo akiwa amepata bia kadhaa, au
amevuta sigara isiyo ya kawaida (bangi?) au amelamba vitu fulani
(‘unga’-madawa ya kulevya?), hana tofauti na mhalifu.
Ni
jambazi anayesababisha watu waishi kwa shida ili wamudu maslahi yake
kwa matarajio kuwa maslahi hayo manono yataleta ufanisi katika kazi
lakini yeye anaishia kutekeleza majukumu yake akiwa na ‘faida kichwani’
(kalewa)!
Katika moja ya makala zangu huko
nyuma niliweka wazi msimamo wangu kuwa mishahara mikubwa kupita kiasi ya wabunge wetu ni ujambazi wa mchana kweupe (daylight robbery)
kwa sababu haiendani na hali mbaya ya uchumi watu. Na sasa ujambazi huo
unajidhihirisha bayana kwa uhuni wa baadhi ya waheshimiwa wanaopuuza
kanuni za Bunge na wajibu wao, na kutinga bungeni wamelewa.
Lakini
kuna swali moja la msingi ambalo kila Mtanzania anapaswa kujiuliza,
“IMEKUWAJE TUMEFIKA MAHALA BAADHI YA WABUNGE WANATINGA BUNGENI WAKIWA
WAMELEWA?”
Msomaji mmoja wa jarida hili, Omary Abdallah, Mtanzania anayeishi nchini Ujerumani alinitumia ujumbe kupitia mtandao wa facebook akishauri
kuwa badala ya kuendelea kuwalaumu viongozi wabovu inabidi sisi
Watanzania wenyewe tuangalie mapungufu yetu yanayotufanya kuchagua
viongozi wasiofaa (kwa mfano hao walevi).
Kwa
kifupi, msomaji huyo anahitimisha kuwa Taifa limegubikwa na utapeli na
uvivu. Rejea kwenye kampeni za ubunge. Utaona mgombea ‘anatoka jasho
mwilini na mapovu mdomoni’ kuwahadaa wapigakura jinsi anavyowajali. Na
kwa uvivu wetu wa kufikiri, wala hatuhoji iwapo ‘uchungu’ wa mgombea
huyo ni kwa ajili ya maslahi yetu au ya tumbo lake (na pengine ‘nyumba
ndogo’ zake). Matokeo ndio hao tunaoambiwa wanatuwakilisha wakiwa
wamekunywa, kuvuta au kulamba kilevi.
Lakini
pia, katika skandali hii ya ulevi wa baadhi ya wabunge, ninaona kipato
cha waheshimiwa hao kuwa miongoni mwa vichocheo vya kuwasahaulisha
wajibu wao.
Katika
mazingira ya kawaida tu, mtu anayepewa fedha nyiiingi zaidi ya mahitaji
yake anaweza kuishia kufanya mambo ya ajabu kabisa. Kwa huku Ughaibuni
tunashuhudia baadhi ya wanasoka, kwa mfano, ambao wanalipwa mamilioni ya
fedha, na kuna aina ya mwafaka wa kimtizamo kuwa ‘madudu’ yanayofanywa
na baadhi yao yanachangiwa na wingi wa fedha usiowiana na mahitaji yao
ya kawaida.
Suala
la nyongeza ya mishahara ya wabunge linaonekana kama limeridhiwa na
umma. Wakati madaktari na walimu wakiambiwa serikali haina fedha za
kuboresha stahili na mazingira ya kazi zao,
hatujapewa sababu za msingi za kuongeza mishahara ya wabunge ambao
tayari walikuwa na mishahara mikubwa kabisa.
Utendaji
kazi wa wengi wao hauendani na hata ‘kidogo’ walichokuwa wanapewa kabla
ya mishahara mipya. Ikumbukwe kuwa mamilioni hayo kwa wabunge wetu ni
fedha za walipakodi ambao wengi wao ni masikini wa kupindukia. Kuna kila
sababu ya si tu kulaani ‘unyonyaji’ huu bali pia kuupinga kwa nguvu
zote.
Sasa,
kwa vile tumeruhusu ubunge uwe njia ya mkato ya kukwaa utajiri basi
tutarajie kuona chaguzi zetu huko mbele zikiandamana na kila aina ya
vituko na vioja miongoni mwa wanaotaka kuwa sehemu ya ‘mradi huu wa
utajiri wa chap chap’ (get-rich-quick scheme).
Katika
hali ya kawaida tu, nani asiyetaka kulipwa japo shilingi elfu kadhaa tu
kwa kazi ya kulala huku una bia mbili tatu kichwani? Ni kama kwenda baa
kisha unalipwa kwa kulewa.
Naomba
ieleweke kuwa si kila mbunge hatimizi wajibu wake. Kuna wazalendo
wachache wanaotambua majukumu yao. Baadhi yao, wameishia ‘kuumbuliwa’ na
Kiti cha Spika kwa ‘kukiuka kanuni za Bunge (isomeke: kutetea maslahi
ya wapigakura katika namna isiyokubalika kwa watawala).
Mashujaa
hawa wachache wana ujasiri wa ziada kwani wakati wao wanatolewa nje kwa
kutimiza wajibu wao, wanashuhudia baadhi ya wanaoachwa waendelee na
vikao wakiwa wamelala kutokana na kinywaji, sigara zisizo za kawaida au
kulamba vitu flani.
Nimalizie
kwa kurejea maswali niliyoyanukuu mwanzoni mwa makala hii. Tumerogwa na
aliyeturoga nae karogwa kisha kafariki, au akili zetu zimefungwa kisha
ufunguo umepotea? Naomba usinijibu bali jibu lako liwe kwenye sanduku la
kura katika uchaguzi ujao.
Penye nia pana njia
Post a Comment