Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
akizungumza na viongozi wa CUF kwa ngazi ya majimbo na Wilaya nne za
Pemba katika ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba.
Mwakilishi wa Jimbo la Ole Mhe. Hamad Massoud Hamad akizungumza na
viongozi wa CUFngazi ya majimbo na Wilaya nne za Pemba kilichofanyika
ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba.
Viongozi wa CUF ngazi ya majimbo na Wilaya nne za Pemba wakimsikiliza
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika
ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
akisalimiana na baadhi ya viongozi wa CUF wakati akijiandaa kuingia
katika kikao cha viongozi wa CUF kwa ngazi ya majimbo na Wilaya nne za
Pemba kilichofanyika ukumbi wa Chuo cha Benjamin Mkapa Wete Pemb.Picha, Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
--
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Maalim Seif Sharif Hamad, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu
katika sensa ya watu na makaazi, ili kuirahishia serikali kupanga
mipango yake ya maendeleo kwa uhakika.
Maalim Seif ametoa wito huo leo katika ukumbi wa chuo cha Benjamin Mkapa
Wete Pemba alipokuwa akizungumza na viongozi wa CUF kwa ngazi za Wilaya
na Majimbo.
Amesema Sensa ya watu na Makaazi ni muhimu kwa wananchi na serikali kwa
ujumla katika kutathmini na kuandaa mipango yake ya maendeleo kwa
wananchi, na kuwataka kuachana na mtazamo kuwa suala hilo linaihusu
serikali pekee.
Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa msimamo huo kufuatia wananchi wengi wa
Kisiwa cha Pemba kuwa na mtazamo wa kutaka kususia suala la sensa kwa
madai kuwa hawakushirikishwa ipasavyo katika suala hilo.
Sababu nyengine iliyowafanya wananchi hao kutaka kususia suala hilo ni
kwa madai kuwa hawawezi kushiriki suala la sensa, huku wakiwa bado
hawajatekelezewa haki zao za kisheria ikiwemo kutopewa vitambulisho vya
uzanzibari ukaazi.
Amewataka wananchi kupima faida na hasara za kushiriki kwenye zoezi
hilo la sensa, na hatimaye waweze kushiriki kikamilifu kwa maslahi ya
maendeleo ya nchi.
Akizungumzia kuhusu mchakato wa ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya
mabadiliko ya katiba, Maalim Seif amewataka wananchi kuwa huru kutoa
maoni yao, na kwamba hakuna atakayeadhibiwa kwa sababu ya kutoa maoni.
“Mimi najua wapo wanaotaka serikali moja, wengine mbili, tatu, nne, na
muungano wa mkataba, lakini wengine wanataka waachiwe wapumuwe.
Yote hayo ni maoni na kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake bila ya
kulazimishwa, kwa hivyo wakati wenu ukifika nendeni mkatiwe maoni hayo
kwa uwazi”, alisisitiza Maalim Seif.
Amesema lengo la serikali ya Tanzania ni kuwa na katiba mpya ifikapo
April mwaka 2014, na kufahamisha kuwa kwa Wazanzibari suala kubwa
linalowagusa kwenye mabadiliko hayo ni suala la Muungano.
“Zanzibar tunayo katiba yetu ambayo imejitosheleza kwa mambo yetu ya
Zanzibar, lakini suala kubwa kwenye mabadiliko hayo kwetu sisi litakuwa
ni la Muungano, na hili haliwezi kuepukwa”, alibainisha.
Amesema Zanzibar kabla ya Muungano ilikuwa nchi huru iliyokuwa na kiti
chake katika Umoja wa Mataifa, na kuelezea haja ya kuwepo kwa Mamlaka
kamili ya Zanzibar ili iweze kurejesha kiti chake kwenye umoja huo.
Amewataka wananchi kuangalia maslahi ya nchi yao kwanza katika mchakato
wa kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba, na kuachana na misimamo ya
vyama katika suala hili linalohusu maslahi ya nchi.
“Katiba ya nchi ni mali ya wananchi sio ya chama chochote, lakini najua
kila chama kina katiba yake na hiyo ndio itabakia kuwa katiba na
muongozo wa chama husika, kwa hivyo ndugu zangu naomba tulifahamu hili
na tuangalie maslahi ya nchi yetu kwanza”, alifahamisha.
Makamu wa Kwanza wa Rais alitumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa
wananchi walioathirika kutokana na ajali mbaya ya boti ya Mv. Skagit
ilisababisha vifo vya watu kadhaa.
Amewataka wananchi kuweka imani zao kuwa suala hilo limetokana na
mipango ya Mwenyezi Mungu, na kwamba hakuna mtu angeweza kulizuia
lisitokee.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amempongeza aliyekuwa Waziri wa
Miundombinu na Mawasilino Mhe. Hamad Massoud Hamad kutokana na kitendo
chake cha kijasiri cha kuamua kujiuzulu nafasi hiyo.
Amesema kitendo hicho cha kuwajibika kisiasa kimemjengea heshima yeye
mwenyewe, chama chake na taifa kwa ujumla, kitendo ambacho linapaswa
kuingwa na viongozi wengine wa nchi iwapo litatokea jambo lolote
linalogusa maslahi ya wananchi.
“Mhe. Hamad amekuwa mwalimu wa viongozi wa Afrika, kwani viongozi wa
Afrika hawana utamauni huo hata likitokea jambo gani, lakini yeye
ameamua kujisafisha licha ya kuwa hakuwa na kosa kwa sababu safari ili
haikuanzia Zanzibar”, alifahamisha Maalim Seif
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Ole Mhe. Hamad Massoud Hamad
ambaye alikuwa akishikilia nafasi hiyo ya uwaziri, amesema aliamua
kuachia nafasi hiyo siku chache baada ya tukio, ili kujijengea heshima
kisiasa.
“Niliamua kujiuzulu nafasi ile kwa nia njema, sikulazimishwa wala
kupokea shinikizo kutoka kwa mtu yoyote”, alisema Hamad Massoud.
Alisema kwa sasa akiwa Mwakilishi wa wananchi na kiongozi wa chama
hicho, ataendelea kushirikiana na viongozi na wanachama katika kukijenga
zaidi chama hicho ili kiweze kufikia malengo yake iliyojiwekea.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais aliwataka wananchi wa kisiwa cha
Pemba kuendeleza utamaduni wa kufutari kwa pamoja ili kuongeza upendo
miongoni mwao.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti baada ya kushiriki
katika futari ya pamoja aliyoiandaa kwa wananchi wa mikoa ya Kusini na
Kaskazini Pemba iliyofanyika Ukumbi wa kiwanda cha makonyo Wawi na
viwanja vya Ikulu ya Wete.
Na
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
Post a Comment