Na Ally Kondo,
Tehran, Iran
Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikari wa Nchi Zisizofungama na Upande Wowote
(NAM) umeanza jijini Tehran, Jamhuri ya Kiislam ya Iran siku ya
Jumapili, tarehe 26 Agosti 2012. Mkutano huo utakaoisha tarehe 31 Agosti
2012 umeanza na kikao cha wa Wataalam ambacho kitafuatiwa na Mkutano wa
Mawaziri tarehe 28 na 29 Agosti 2012 na kisha ule wa Wakuu wa Nchi na
Serikali tarehe 30 na 31 Agosti 2012.
Katika
Mkutano wa Wataalam, Ujumbe wa Tanzania unajumuisha Balozi Celestine
Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dkt Justin Seruhere, Kaimu
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, New York, pamoja na
maafisa wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa.
Mheshimiwa
Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, atamwakilisha Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwenye Mkutano
wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Wakati
wa ufunguzi wa kikao cha wataalam, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Dkt.
Ali Akbar Salehi alieleza kuwa nchi yake ambayo imechukuwa Uenyekiti wa
NAM kutoka kwa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri katika kipindi cha miaka
mitatu ijayo, itajitahidi kuhakikisha kuwa Umoja huo unaendelea
kuimarika katika kutekeleza malengo yake ya msingi. Waziri huyo
aliendelea kueleza kuwa kufanyika kwa Mkutano huo ni ishara ya wazi kuwa
NAM ina dhamira ya dhati ya kuuenzi umoja huo na kuufanya kuwa chombo
madhubuti cha kutetea na kulinda maslahi ya wanachama wake.
Mhe.
Salehi alifafanua baadhi ya masuala ambayo NAM imekuwa ikiyapa umuhimu
mkubwa tangu kuundwa kwake mwaka 1961 na yanayotakiwa kundelea kupewa
kipaumbele ni pamoja na: kutambua na kuheshimu tofauti za tamaduni
duniani na kupinga jitihada zozote za kupandikiza tamaduni za kigeni
zisizokubalika katika nchi nyingine.
Hivyo,
alibainisha kuwa NAM inafanya juhudi kubwa kufanya majadiliano miongoni
mwa jamii, tamaduni na dini tofauti kwa lengo la kukuza na kuimarisha
ushirikiano, amani na kuondoa ubaguzi.
Waziri
huyo alibainisha kwamba nchi zote duniani zinauona Umoja wa Mataifa
kuwa ni Taasisi kubwa ulimwenguni ambayo iliundwa kutokana na athari za
Vita Kuu vya pili vya dunia. Hivyo, wanachama wa NAM hawaungi mkono masuala yote ambayo yanatokea duniani yenye dhamira ya ukandamizaji kama
vile dhuluma, ubaguzi, matumizi mabaya ya madaraka, ubabe, aina zote za
ukoloni pamoja na mizozo inayohusisha matumizi ya silaha.
Aidha,
Mhe. Salehi katika hotuba yake aligusia masuala ambayo yanajiri hivi
sasa duniani, hususan Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.
Alisisitiza umuhimu wa kusikiliza ujumbe unaotolewa na watu wa maeneo
hayo ambao wanapigania uhuru, haki na utu. Alisema kuwa mafunzo
yanayopatikana kutokana na vitendo hivyo ni kwamba hakuna utawala ambao
unaweza kupuuza matakwa na malengo halali ya watu wake. Hivyo, njia
pekee ya kuepukana na masuala hayo ni tawala za kiimla zikubali kufanya
majadiliano, kuheshimu haki za msingi za binadamu na kutimiza mahitaji
ya msingi ya watu wao.
Post a Comment