Mchezaji Emmanuel Okwi kutoka nchini Uganda ambaye amesaini mkataba mpya na timu ya Simba kwa miaka mitatu zaidi
BAADA ya kuwepo kwa
tetesi za Yanga kutaka kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Emmanuel
Okwi, hatimaye ameongezewa mkataba wa miaka miwili kwa dau la sh milioni 50
pamoja na gari la kifahari.
Hivi karibuni, nyota huyo
ambaye alikuwa nchini Austria
kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Red Bull
Salzburg kabla ya kurejea nchini Jumanne, amekuwa akidaiwa kuwaniwa na Yanga.
Chanzo cha habari kutoka
ndani ya Simba kinaeleza kwamba, zoezi hilo
lilifanyika juzi likiendeshwa na wajumbe wawili wa Kamati ya Usajili, ambao
walitoa kiasi hicho cha fedha ili kumbakiza, Okwi Msimbazi.
Imeelezwa kuwa Simba
wameona wamuongeze mkataba Okwi, ili kumuepusha na mpango uliokuwa ukifanywa na
mahasimu wao nchini, Yanga kutaka kumsajili.
“Tayari tumeshamfunga
Okwi kwa sasa, hivyo mahasimu wetu walie tu, tumempa miaka miwili kwa dau la
mil. 50, pia tumempa gari na mambo mengine madogomadogo tumeyaweka sawa,”
alisema mtoa habari huyo.
Nyota huyo, mkataba wake
umebakiza miezi minne kabla kumalizika ambapo kuna taarifa kwamba aliwataka
viongozi wa Yanga wampe sh milioni 56 ili aweze kumwaga wino Jangwani.
Katika hatua nyingine,
Simba jana ilihitimisha Wiki ya Simba na Jamii kwa kutoa misaada yenye thamani
ya sh milioni 1.5 katika kituo cha kulea watoto yatima cha Maunga, kilichoko
Kinondoni Hananasif, Dar es Salaam, kwa
lengo la kuwafariji.
Katika ziara hiyo, baadhi
ya wachezaji waliohudhuria ni pamoja na Okwi, Juma Nyosso, Uhuru Suleiman na
wengineo sambamba na baadhi ya viongozi chini ya Makamu Mwenyekiti, Geofrey
Nyange ‘Kaburu’, ambaye alisema wameona watembelee kituo hicho, kwani watoto
hao pia wanahitaji faraja na kuwa huo ni mwanzo tu watakuwa wakifanya hivyo
mara kwa mara.
Wakiwa kituoni hapo,
walikabidhi fedha taslimu sh 500,000 pamoja na mahitaji mbalimbali ikiwemo
unga, mchele, sabuni na vinginevyo.
Chanzo:www.dinaismail.blogspot.com
Post a Comment