Loading...
Malawi:Hatutapigana
MALAWI imesema imeondoa ndege zake zilizokuwa zikifanya utafiti wa mafuta katika Ziwa Nyasa kwa kuwa haitaki kuingia vitani, badala yake imeamua kupeleka mgogoro huo Mahakama ya Kimataifa.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani na Uhusiano wa Kimataifa kwa Mambo ya Kiusalama wa Malawi, Uladi Mussa alipokuwa akizungumza na gazeti linalochapishwa nchini humo la Nyasa Times.
“Nawahakikishia wananchi mtaendelea kuishi kwa utulivu. Tupo kwenye mazungumzo na Serikali ya Tanzania, bila shaka mambo yataenda vizuri. Kama hali ikishindikana tutalipeleka suala hili kwenye Mahakama ya Haki ya Kimataifa,” alisema Mussa.
Kauli ya Waziri huyo imekuja wakati baadhi ya wananchi wa Malawi wanaoishi katika Vijiji vya Karonga na Chitipa vilivyopo kando ya Ziwa Nyasa upande wa Malawi wakiwa wameanza kuvihama vijiji hivyo kuhofia usalama wa maisha yao.
Baadhi ya wakazi hao wamekaririwa na Nyasa Times wakisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo kunusuru maisha kutokana na kuwapo kwa dalili za kutokea vita kati ya Malawi na Tanzania.
Waziri Mussa amesema suala hilo la mgogoro wa mpaka litaamuliwa kwa njia ya amani na hivyo kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao bila wasiwasi.
Waziri huyo aliwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali ya Malawi ina ushahidi wa kutosha kuwa ziwa lote la Malawi (Nyasa)ni mali ya Malawi na Tanzania haina nguvu ya kuwasimamisha kuendelea na kazi ya kutafuta mafuta.
“Kimsingi hapa hakuna hoja ya kubishania. Wote tunajua ziwa hili ni mali yetu (Malawi),” alisema.
“Kama malalamiko haya yangekuwa yametolewa na Msumbiji, hapa tungekuwa na hoja ya kubishania, lakini si Tanzania.” alisisitiza.
Alisema ushahidi wao wa mipaka ni wa tangu mwaka 1890 wakati ambako wakoloni wa Uingereza na Ujerumani walitiliana saini juu ya suala hilo.
Aliendelea kueleza kuwa umiliki huo wa ziwa umeongezewa nguvu na maazimio ya mwaka 1963 ya Wakuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) kwamba wanachama wanapaswa kuheshimu mipaka waliyorithi kwa wakoloni.
Kauli za wananchi
Wakati Serikali ya Malawi ikitoa msimamo huo watu kadhaa waliohojiwa wameonyesha hofu ya nchi hizo kuingia katika vita.
Heckley Christopher ambaye ni raia wa Malawi anayefanya biashara eneo la Mbambabay mkoani Ruvuma anasema: " Malawi ni nchi ndogo sana kupigana na Tanzania, ni nchi yenye mikoa minne tu, kukiwa na vita itaangamia mara moja."
Raia mwingine wa Malawi ni Vilion Gordon ambaye alisema Tanzania na Malawi ni marafiki wa siku nyingi, hivyo hawana sababu za kugombania ziwa ambalo lilikuwapo tangu enzi hizo.
"Nashauri wakae chini wapatane, kwa nini tugombane sasa wakati ziwa hilo lilikuwapo tangu enzi hizo?"alisema.
Mtanzania mkazi wa Kijiji Lundo kilichoko Mbambabay mkoani Ruvuma, Zakhia Chengula ameitaka Serikali ya Tanzania kuendelea kuimarisha ulinzi na kukubali kuingia katika mazungumzo na Malawi badala ya kufikiri vita.
"Hapa sisi ni kwetu, vita ikiingia sisi tutakufa tu hakuna pa kukimbilia. Tunaiomba Serikali iimarishe ulinzi eneo hilo na ikae na Malawi kuzungumzia mgogoro huo," alisema.
Mkuu wa Wilaya mpya ya Nyasa, Ernest Kahindi alisema hakuna hofu yoyote kwa wakazi wanaoishi kando ya Ziwa Nyasa upande wa Tanzania.
Amewataka wananchi hao kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali kama kawaida kwani suala hilo sasa linashughukiliwa kitaifa.
"Mwanzoni kulikuwa na hofu kubwa, lakini baada ya Serikali ya Tanzania kutoa tamko la kutaka ndege za Malawi ziondoke na zenyewe kutii amri hiyo, hakuna tatizo lolote," alisema na kuendelea;
"Shughuli katika eneo hili zinaendelea kama kawaida. hakuna mwananchi aliyepigwa risasi wala ndege iliyotunguliwa, mambo yako shwari."
Jeshi laimarisha ulinzi
Katika hatua nyingine Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeimarisha ulinzi katika mwambao wa Ziwa Nyasa na kupiga marufuku wananchi kukatisha eneo lao la jeshi.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Kyela waliozungumza na gazeti hili jana walisema kuibuka kwa mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, kumesababisha kuongezeka kwa ulinzi katika eneo hilo.
“Mara ya kwanza tulikuwa tunaingia tu pale kambini kama tumeagizwa vitu kama mayai, vocha na vitu vingine na wanajeshi wa pale tunawapelekea, lakini sasa tangu kuibuka kwa mgogoro huo wa mpaka wa Ziwa Nyasa na hawa wa Malawi tumezuiliwa kabisa kuingia hapa” alisema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina Hamis
Chanzo cha hofu
Jumatatu wiki hii, akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe aliitaka Malawi kuziondoa ndege na kampuni zinazofanya utafiti wa mafuta katika eneo hilo kwa kuwa ni mali ya Tanzania.
“Serikali ya Tanzania inapenda kuyaonya na kuyataka makampuni yote yanayoendelea na shughuli za utafiti eneo hilo zisitishe mara moja kuanzia leo (Jumatatu),” alisisitiza Membe.
Mbali na Waziri Membe viongozi wengine waliozungumzia mgogoro huo na kuitaka Malawi iache uchokozi ni Samuel Sitta na Mwenyeti wa Kamati ya Bunge ya masuala ya ulinzi, Edward Lowassa.
Wakati Sitta akiwataka Watanzania kuendelea nashughuli zao bila hofu kwa kuwa Serikali iko tayari kwa tishio lolote, Lowassa alisisitiza kuwaTanzania imejiandaa kiakili na kivifaa kuingia vitani na Malawi kama italazimika kufanya hivyo.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
Chediel . Powered by Blogger.
Post a Comment