THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za
rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis
Mwamunyange kuomboleza vifo vya askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (TPDF) waliokuwa wanalinda amani katika eneo la Darfur, Sudan,
vilivyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika salamu zake hizo, Mheshimiwa Rais Kikwete amemwambia Jenerali Mwamunyange: “Nimepokea
kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za vifo vya vijana wetu watatu wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) ambao walikuwa wanalinda amani
katika Darfur, Sudan ambavyo nimejulishwa kuwa vilitokea Jumapili
iliyopita.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Vifo
vya vijana wetu hawa vinasikitisha zaidi kwa kuzingatia kuwa wamepoteza
maisha yao katika utumishi muhimu sana wa nchi yetu na katika kulinda
amani ya Bara letu la Afrika. Tutaendelea kuwakumbuka kwa utumishi
uliotukuka na mchango wao kwa nchi yetu na kwa Bara letu la Afrika.”
Amesema Mheshimiwa Rais Kikwete: “Kufuatia
vifo hivyo, nakutumia wewe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali
Davis Mwamunyange salamu za rambirambi. Aidha, kupitia kwako, naomba
uniwasilishie pole zangu nyingi kwa familia za vijana wetu ukiwajulisha
kuwa moyo wangu uko nao wakati wa kipindi hiki kigumu cha kuwapoteza
wapendwa wao. Naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema,
aziweke pema peponi roho za marehemu.”
Rais
Kikwete pia amemtaka Jenerali Mwamunyange kuwafikishia salamu za pole
Makamanda na askari wote wa Tanzania wanaolinda amani katika Darfur.
Askari
hao wawili ambao ni sehemu ya wanajeshi 850 wa Tanzania wanaolinda
amani katika Darfur na mwenzao mmoja ambaye hajulikani alipo mpaka sasa
walipoteza maisha yao katika ajali ya gari lao kusombwa na maji wakati
wakivuka mto katika Kijiji cha Hamada, eneo la Manawasha, Darfur.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
28 Agosti, 2012
Post a Comment